Vikwazo, mizengwe katika kupiga kura


John Rwekanika's picture

Na John Rwekanika - Imechapwa 06 October 2010

Printer-friendly version
Gumzo

SWAWABU Swaibu (20), hatapiga kura mwaka huu. Hakujiandikisha. Ni kama Novat Katageywa (22) aliyejiandikisha lakini amehamia sehemu nyingine.

Wawili hao ni kama maelfu ya wanafunzi wa vyuo vikuu nchini ambao hawatakuwa walipojiandikishia; hivyo hawatapiga kura.

Swaibu hakujiandikisha kupiga kura kwa kuwa alikuwa masomoni Uganda. Aliporudi nchini akaambiwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) tayari imemaliza kuandikisha na kuboresha daftari la wapigakura.

Kijana Swaibu ni mkazi wa kata ya Ibwera, kijiji cha Ibwera, kitongoji cha Rubungo ambako waandishi wa habari wa Klabu ya Waandishi ya Kagera (KPC) wanachunguza sababu za wananchi wengi kutojiandikisha na kutopiga kura hata wanapokuwa wamejiandikisha.

Analaumu tume kwa kufanya kazi kwa kipindi kifupi na wakati unapokaribia uchaguzi tu; vinginevyo angeweza kujiandikisha.

“Kama ambavyo kila siku kuna wanaokufa na wanaozaliwa, kila siku kuna wanaofikisha umri wa miaka 18,” anasema Swaibu na kuuliza iwapo watumishi wa NEC hukodishwa kwa mwaka mmoja tu na tena karibu na uchaguzi.

Naye Katageywa wa kata ya Ibwera, kijiji cha Ibwera, kitongoji cha Rubungo, anasikitishwa na jinsi atakavyoshindwa kupiga kura mwaka huu.

Alihamia hapa baada ya kupata kibarua cha kuchunga ng’ombe lakini baada pia ya kujiandikisha kupiga kura mjini Muleba.

Alipo sasa ni kama kilomita 70 kutoka alikojiandikishia. Nauli ya kwenda na kurudi – kutoka Ibwera hadi Muleba – ni kati ya Sh. 10,000 na 15,000 ambazo anasema hawezi kuzipata katika mazingira magumu ya kiuchumi aliyomo sasa.

“Tume ingekuwa inaendelea na zoezi la kuboresha daftari la wapigakura wakati nahamia Ibwera, nisingekwama kushiriki uchaguzi,” anasema Katageywa.

Naye Bi. Lazia Biilabake (43), mmoja wa wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ambaye ni mratibu wa elimu wa kata ya Kikomelo, amesema kwa sasa hawezi kutoa uhamisho wa mkazi wa kata yake kwenda kupiga kura kata nyingine kwa sababu zoezi hilo limefungwa.

Wananchi ambao wanakabiliwa na mazingira kama haya ni wengi na wengi wao hushindwa ama kujiandikisha au kupiga kura wakati wamejiandikisha.

Bali waliojiandikisha wana raha zao. Joseph Rafael (72) anasema mbunge aliyemaliza muda wake Bukoba Vijijini “alisahau wananchi wake na ahadi alizotoa.”

Anasema Oktoba anakwenda kupiga kura itakayoleta mbunge mwingine akiwa na uhakika kuwa huyo mpya atakuwa ameona yaliyomsibu aliyeondoka na hivyo “atajifunza kujali.”

Katika maeneo ambako mwandishi huyu alitembelea katika jimbo la Bukoba Vijijini, mbunge aliyemaliza muda wake, Nazir Karamagi anabebeshwa lawama lukuki.

Hawa wanasema aliahidi kuwapelekea umeme; wale wanadai aliahidi kuwapa fedha za kuanzisha SACCOS; wengine wanasema aliahidi fedha za kuanzisha miradi ya kuwasaidia vijana wasio na ajira waishio vijijini.

Katika vitongoji vya Kikomelo, Ruzinga, Mbungwe, Kihumulilo, Kamiza, Kashabele, Nyamabale na Buyango; na katika vijiji vya Ibwera, Rubungo na Kalonge, madai na tuhuma vimezagaa.

Hali hii ya kutegemea zaidi misaada na kujenga imani kwa ahadi nyingi za kiongozi, inatajwa kuwa chanzo cha wananchi kukata tamaa kwamba hawakusaidiwa na hivyo kususia kujiandikisha au kupiga kura.

Viongozi wa serikali za vijiji na vitongoji nao wana mchango wa kipekee katika kuwezesha au kukwamisha uandikishaji wa wapigakura na katika zoezi la kupiga kura.

Katika kata za Ibwera na Kikomelo, viongozi wamemweleza mwandishi huyu kuwa wanabaguliwa kimaslahi, hivyo hawatawaamsha wananchi kwenda kupiga kura tarehe 31 Oktoba.

Wales Kakila (42), mwenyekiti wa kitongoji Rubugo, Kijiji cha Ibwera kata ya Ibwera, amesema hatajiingiza katika shughuli za kuhamasisha waliojiandikisha kupiga kura.

Anasema hatafanya hivyo kwa kuwa tume “haitutambui katika shughuli hiyo. Kama ingekuwa inatambua basi ingetupatia walau posho kidogo ya kujikimu.”

Amesema siyo kazi ndogo kutembelea kaya 150 katika kitongoji chake na kuongeza, “Kama nikilazimishwa sitafanya kazi hiyo na kama ni kupoteza uenyekiti sitajali, kwani nalipwa nini” aliuliza.

Mara nyingi wenyeviti wa vitongoji na mitaa hupewa majukumu na msimamizi msaidizi wa Kata, kusambaza vipeperushi vya kuhamasisha wapigakura juu ya haki za wapigakura pamoja na vipeperushi vinavyozuia kutoa na kupokea rushwa.

Viongozi wa vitongoji ndio wako karibu na wasimamizi wasaidizi kwenye ngazi ya kata na huona wasimamizi hupata posho kiasi gani wakati wa kuelekea uchaguzi.

Kwa mfano, mwandishi ameambiwa kuwa wasimamizi wasaidizi wanapokea posho ya Sh. 10,000 kila siku kuanzia tarehe 8/8/2010 mpaka 5/11/2010.

Hii ni mbali na malipo ya posho za semina zisizopungua Sh. 50,000 kila wanapohudhuria; huku mishahara yao ikiwa palepale.

Hali hii, miongoni mwa viongozi wa ngazi ya chini na inayochukua sura ya mgomo baridi, haiwezi kusaidia wananchi kujiandikisha wala kwenda kupiga kura siku inapowadia.

Tatizo jingine linaloweza kuleta kero kwa waliojiandikisha na kusababisha wasipige kura, ni foleni ndefu ambako wazee, wajawazito na hata waliochoka kwa ulevi, huona vigumu kusimama kwa saa nyingi.

Mzee Joseph Raphael na bintiye Sylivia wanapendekeza kuwepo vituo vingi vyenye wapigakura wachache ili kupunguza mchoko na kurahisisha zoezi la kupiga kura.

Kuendelea kuwepo kwa chama kimoja madarakani kwa miaka mingi – sasa ni miaka 50 – kumefanya baadhi ya wananchi kusema, “Nakwenda kuchagua nani? Si walewale? Hata nisipoenda.”

Mazingira ya walewale na yaleyale, yamejenga tabia ya kuchagua kwa mazoea tu kwa madai kuwa “serikali imesema.”

Ofisa mmoja mstaafu aliyesema hahitaji kutajwa jina gazetini alisema katika mjadala na vijana kwenye kitongoji cha Kikomelo, “Chagueni ninyi. Wamenifanyia nini cha maana? Mwaka huu ndio hawanioni kabisa,”

Jambo jingine ambalo mstaafu huyo amesema ni kuhusu tabia na mwenendo wa viongozi.

Amesema, “Ikitokea wakawepo viongozi serikalini ambao hawajali; wasio makini, wanaouza ardhi, misitu, madini na anga ya nchi, wananchi wanaanza kufikiri kuwa hawana haja ya kuchagua wezi.”

Hali hii inaweza kufanya watu wasijiandikishe au waliojiandikisha wasipige kura kwani hawaoni, miongoni mwa wagombea, anayewapa matumaini ya kuondokana na shida zao, amesema.

“Inafika mahali wananchi wanaona siasa haziwezi kuwaondoa pale walipokwama; labda nguvu za kijeshi. Huku ni kukwama kiakili; lakini ndiko wanakofikishwa na kwa hiyo hawapigi kura,” amesema mstaafu huyo.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu: 0784834070 na imeili: rwekanikajohn@yahoo.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: