Vioja katika uchezeshaji soka


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 20 April 2011

Printer-friendly version

MALALAMIKO ya klabu ya soka ya Simba ya Dar es Salaam dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo hayakuwa miongoni mwa masuala yaliyopangwa kujadiliwa jana na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) jijini Johannesburg, Afrika Kusini.

Kamati ya Nidhamu ya CAF inakutana jana na leo kujadili kesi saba za maamuzi ya upendeleo katika viwanja vya ugenini.

Simba, ikijenga ushahidi katika malalamiko yaliyokuwa yameripotiwa katika mtandao wa Ahramonline, ilitaka ipewe ushindi kwa madai TP Mazembe ilimtumia mchezaji ambaye hakuwa amesajiliwa kihalali, lakini kubwa zaidi kuwepo madai ya upangaji matokeo.

Waamuzi wa Misri waliopangwa kuchezesha mechi hiyo, inadaiwa waliwasilisha malalamiko CAF kwamba walishawishiwa kupewa hongo ili kuipendelea timu hiyo ya DR Congo katika mechi yao dhidi ya Simba ya Dar es Salaam.

Katika malalamiko yao, walidai walitaka kuhongwa dola 10,000 za Marekani sawa na Sh 15 milioni za Tanzania wakati wa mechi ya kwanza jijini Lubumbashi ambako wenyeji walishinda kwa mabao 3-1.

Wamisri
Waamuzi hao walitoa malalamiko katika wiki ambayo Wamisri walifanya vituko. Kwanza mashabiki wa klabu ya Zamalek walisababisha vurugu katika mechi dhidi ya Club Africain ya Tunisia.

Pili, mwamuzi mwingine wa Misri Fahim Omar alifanya madudu katika mechi ya marudiano kati ya klabu ya Dynamo ya Zimbabwe na MC Alger ya Algeria jijini Algiers.

Mwamuzi huyo aliwaonyesha kadi za njano wachezaji saba na akawatoa wawili kwa kadi nyekundu. Dynamo ilipiga frikiki moja wakati MC Alger ilipiga faulo 36. Pia mwamuzi hakujali hata pale wachezaji wa Dynamo walipopigwa vipepsi.

Huo ulikuwa mkakati mzito wa kuhakikisha MC Alger inatumia uwanja wake wa nyumbani kupindua kipigo cha mabao 4-1 kuwa ushindi. Ndiyo, katika mazingira hayo, MC Alger ilishinda mabao 3-0 na kusonga mbele.

Mifano hiyo na mingine inayofuata chini imetolewa kuonyesha kwamba baadhi ya madudu yanayofanywa na waamuzi nchini na duniani kote hutokana na kutoona vizuri kosa, lakini mara nyingi ni kwa sababu ya uelewa mdogo wa Sheria 17 za soka, na rushwa.

Kutokana na uwezo mdogo au rushwa, mashabiki wa soka wamekuwa wakishuhudia waamuzi wakikataa bao la wazi, au kudai bao limeingia wakati mpira haujapita mstari wa goli.

Matukio yapo mengi lakini lililoshangaza watu wengi ni la mwamuzi wa kike Silvia Regina de Oliveira wa Brazil, kukubali bao baada ya mpira kupigwa na mtu ambaye wala hakuwa anacheza dimbani na mpira kujaa wavuni. Silvia alikuwa mwanamke wa kwanza kuchezesha mechi ya ngazi ya juu nchini humo.

Tukio hilo liliwaacha mashabiki na viongozi wa klabu za Santacruzense na Atletico Sorocaba wamepigwa butwaa pale, kijana mmoja muokotaji mpira, alipoingia kupiga uende ulikokuwa unasubiriwa upigwe kolikiki.

Badala yake mpira ulijaa wavuni na mwamuzi huyo, ambaye alikuwa amegeukia mgongo tukio, alipogeuka alikubali kuwa ni bao halali dhidi ya Atletico Sorocaba ambao walitimuliwa uwanjani wakipinga bao hilo.

Katika fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika mwaka 2006 nchini Ujerumani, mwamuzi Graham Poll wa Uingereza alifirikiwa kuwa mmoja wa waamuzi bora ulimwenguni na alikuwa anapewa nafasi kubwa ya kuchezesha mechi ya fainali.

Haikuwa hivyo, alifanya kosa kubwa katika mechi kati ya Croatia na Australia baada ya kutoa kadi tatu za njano kwa mchezaji mmoja kabla ya kumtoa nje kwa kadi nyekundu. Poll hakuchezesha tena kwenye Kombe la Dunia.

Makosa mengine yaliyofumbiwa macho kutokana ama na rushwa au uwezo mdogo ni pamoja na alilotenda Thierry Henry. Mchezaji huyo wa Ufaransa aliushika mpira mara mbili kabla ya kutoa pasi kwa William Gallas aliyepiga bao dhidi ya Ireland lakini mwamuzi Martin Hansson alilikubali bao hilo lililoizuia Ireland kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2010.

Mengine ni kama Bao la Mkono wa Mungu la Diego Maradano Argentina ilipoinyuka England katika fainali za Kombe la Dunia mwaka 1986. Aliyefumbia macho kosa lile ni mwamuzi wa Tunisia, Ali Bin Nasse.

Mwamuzi Jorge Labbadia wa Uruguay ndiye amesaidia ongezeko la kampeni ya kutaka vitumike vifaa kusaidia kuonyesha mpira umeingia ua la.

Mwamuzi huyo alikataa bao la mkwaju wa Frank Lampard ambao ulipiga mwamba wa juu na kuingia ndani. Hadi wakati huo England ilikuwa imechapwa na Ujerumani mabao 2-1 katika Kombe la Dunia 2010 nchini Afrika Kusini na hadi mwisho ubao ulisomeka mabao 4-1.

Makosa ya Labbadia yalimlazimisha Rais wa FIFA, Sepp Blatter kuwaomba radhi wadau, lakini akasema kosa lile lilimshawishi kufungua mjadala kuhusu matumizi ya kifaa cha kugundua goli likiingia.

Lakini katika fainali hizo, mwamuzi wa Italia, Roberto Rosetti, aliruhusu bao la Carlos Tevez katika ushindi wa Argentina wa mabao 3-1 dhidi ya Mexico.

Ushindi nyumbani
Japokuwa timu bora ina uwezo wa kushinda kokote, nyumbani na ugenini, timu zijifunze kutumia vizuri uwanja wa nyumbani kama timu za soka za taifa na vijana chini ya miaka 23 zilivyowapa raha Watanzania.

Mathalani Afrika Kati tayari imeapa kwamba Stars itake isitake, lazima ifungwe Bangui. Wanachojivunia sana si uwezo na kushangiliwa na mashabiki, bali kucheza na waamuzi nje ya uwanja.

0
No votes yet