Viongozi Afrika genge la waroho wa madaraka


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 15 December 2010

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli
Laurent Gbagbo

KAMA Mungu angewauliza viongozi wa Afrika kupitia umoja wao wa Afrika (AU), amtume nani kwenda kupatanisha mtafaruku wa uongozi nchini Ivory Coast, lingekuwa swali gumu.

Maana angeuliza viongozi ving’ang’anizi kama Laurent Gbagbo aliyeshindwa uchaguzi, lakini akajitangaza rais. Viongozi wengine wameingia madarakani kwa vita.

Viongozi wangekula sambusa wakamaliza bila kumpata afaae kutumwa maana wote ni waroho wa madaraka.

Tazama, Robert Mugabe amekaa madarakani miaka 30 na alipokataliwa kwa kura amegoma. Teodoro Obiang Nguema Mbasongo ameng’ang’ania kwa miaka 29, Hosni Mubarak 29, Paul Biya 28, Zine Al-Abidine 23, Yowerri Museveni 23, Omar Al-Bashir 20, Idris Derby 18, Yahya Jameh 15 na Denis Sassou Nguesso miaka 13.

Muammar Gadaffi aliyeko madarakani kwa miaka 41  hatarajiwi kuitisha uchaguzi. Hayati Omar Bongo baada ya kukaa madarakani kwa miaka 42, akarithisha mwanawe, Ali Bongo, aliyetangazwa mshindi kwa asilimia 42 wa uchaguzi na Mahakama ya Katiba.

Baada ya upinzani kupinga matokeo hayo, Mahakama ya Katiba ilihesabu upya kura. Ikamtangaza tena kwa kupata asilimia 41.79.

Kwa hiyo, uamuzi wa viongozi wa AU kumtuma Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki ulionekana nafuu.

Mbeki ndiye alihangaika na mgogoro wa Zimbabwe ya Mugabe bila mafanikio hadi akamwachia mrithi wake, Jacob Zuma.

Mugabe alimpuuza Mbeki kwani hata yeye kwa kutumia hila, alijitahidi bila ya mafanikio kubaki madarakani. Mbeki alitajwa kupanga njama kushinikiza Zuma afunguliwe kesi ya ufisadi katika ununuzi wa silaha mwaka 1999 na hata kesi iliyofunguliwa kwamba Zuma alibaka binti wa rafiki yake tena mwenye ukimwi.

Ilidaiwa lengo lilikuwa kumchafua asikubalike ndani ya African National Congress (ANC) na hivyo asiteuliwe na chama hicho kuwania urais. Kesi zote mbili zilitupwa.

Hata ulipotokea mgogoro wa mwanzo Ivory Coast, Mbeki alitumwa, lakini ‘hakufanikiwa’ kwani Alassane Ouattara alikosa haki yake. Sasa kwa nini AU imeamua kumtuma tena? Bila shaka haina viongozi wasafi wanaoweza kumnyooshea kidole Gbagbo.

Gaddafi amekuwa madarakani Libya tangu mwaka 1969 baada ya kumpindua King Idris. Nguesso amekuwa rais wa Jamhuri ya Congo tangu mwaka 1997. Aliwahi kuwa rais mwaka 1979 hadi 1992 alipotupwa katika uchaguzi wa vyama vingi.

Baada ya kukaa kama mpinzani kwa miaka mitano, Nguesso alirejea madarakani 1997 vilipomalizika vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoondoa utawala wa Rais Pascal Lissouba. Mwaka 2002 akaitisha uchaguzi akashinda, lakini anatawala roho juu kutokana na ushindi wa kutatanisha katika uchaguzi wa mwaka 2009.

Awali Idris Derby aliyekuwa mkuu wa majeshi, alishirikiana na Hissène Habré katika vita vya wenyewe kwa wenyewe na mwaka 1980 Habré akawa rais, lakini maswahiba hao wakahitilafiana. Vikazuka vita mwaka 1989.

Akisaidiwa na vikosi vya Libya na Sudan, mwaka 1990 Derby akamng’oa Habre na kujitangaza rais wa Chad hadi sasa.

Labda Jose Eduardo dos Santos wa Angola. Lakini na yeye madai kuwa alishinda uchaguzi wa mwaka 1992 kwa asilimia 49 yalimchafua hadhi na mpinzani wake mkuu hayati Jonas Savimbi alipinga.

Jambo zuri kwake ni kwamba amepitisha katiba mpya inayotaka rais kukaa vipindi viwili tu.

Museveni wa Uganda aliingia madarakani baada ya vita vya msituni mwaka 1986, Paul Kagame wa Rwanda aliingia baada ya mauaji ya kimbari mwaka 1994. 

Museveni pamoja na Mugabe ambaye alipigania uhuru wa Zimbabwe kutoka kwa Waingereza, wanajiona wanayo haki ya kula nchi vyovyote vile.

Mwai Kibaki? Rais huyo wa Kenya anahusishwa na machafuko yaliyotokea baada ya uchaguzi mkuu wa 2007.

Kibaki amekuwa kiongozi wa chama cha upinzani tangu mwaka 1991. Mwaka 2002 alichaguliwa rais wa tatu baada ya kujaribu bila mafanikio mara mbili; mwaka 1992 na mwaka 1997.

Lakini madudu aliyoyafanya katika uchaguzi mkuu wa pili mwaka 2007 hayaelezeki akaishia ‘kujitangaza’ na kuapishwa kuwa rais usiku wa Desemba 30, 2007.

Hapo ndipo ulipozuka mzozo na machafuko yaliyoenea nchi nzima ambayo yalipomalizika, kiasi cha watu 1,000 walikufa. Ni hapo rais Jakaya Kikwete alionekana shujaa kwani ndiye ‘aliyesuluhisha’ na kuwezesha kuundwa kwa serikali ya pamoja akishirikiana na Raila Odinga, aliyesadikiwa kuwa ndiye alishinda uchaguzi.

Kwa hiyo, Mungu angeweza kumtuma tena Kikwete kupeleka ujumbe mwingine wa amani Ivory Coast kama alivyofanya Kenya?

Hilo lingekuwa chaguo jingine gumu kwani ipo tofauti kubwa kuhusu Kikwete kutoka mwaka 2008 hadi mwaka 2010.

Mwaka 2008 alikuwa kipenzi cha Watanzania kufuatia ushindi wa asilimia 82 katika uchaguzi mkuu wa 2005, lakini ushindi wa asilimia 61 alioupata mwaka huu, umepingwa na chama kikuu cha upinzani – CHADEMA.

Hivyo, Kikwete sasa ni mtuhumiwa wa ushindi unaolalamikiwa.

Katika mgogoro wa Kenya mwaka 2008 ilikuwepo timu ya wasuluhishi chini ya Kofi Annan iliyoteuliwa na AU. Alifika kukwamisha mpira wavuni baada ya kazi kubwa iliyofanywa na Annan akishirikiana na Benjamin Mkapa na Graca Machel baada ya Askofu Desmond Tutu kutengeneza ‘mapito’.

AU yatanzika

Mbeki amerudi mikono mitupu. Jumuiya ya Uchumi ya Afrika Magharibi (Ecowas) imemtambua Ouattara kuwa ndiye rais halali, sawa na walivyoamua Umoja wa Mataifa. Sasa vipi AU?

Mtanziko wa AU unatokana na utamaduni wa miaka ya hivi karibuni wa viongozi au wagombea kutoka vyama vikongwe kung’ang’ania kubaki madarakani bila ya kujali uamuzi wa wananchi kupitia kura zao kama ilivyotokea Kenya na Zimbabwe.

Wameacha uadilifu na kuwa genge la waroho wa madaraka wanaolindana kila mwenzao anapoangushwa na mpinzani. Mungu asingeweza kumtuma mroho wa madaraka kupatanisha mroho mwenzake.

0
No votes yet