Viongozi wa dini na kitanzi cha serikali


Padre Baptiste Mapunda's picture

Na Padre Baptiste ... - Imechapwa 05 June 2010

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli

NILICHOTABIRI kitatokea katika mkutano kati ya viongozi wa madhehebu ya dini na serikali, hakika ndicho kilichotokea.

Wiki mbili zilizopita, serikali ilikutana na viongozi wa madhehebu ya dini katika kile kilichoitwa kufafanua Sheria ya Gharama za Uchaguzi iliyosainiwa kwa mbwembwe na Rais Jakaya Kikwete.

Katika mkutano huo, serikali na viongozi wa dini walikubaliana. Kwamba viongozi wa dini wasiweke siasa katika mahubiri yao, huku viongozi wa serikali wakikubali kutoingilia mambo ya imani.

Hata hivyo, makubaliano haya hayawezi kudumu. Ni lazima yatakataliwa kwa vile hayaonekani kuleta tija.

Kwanza, mahubiri ni sehemu ya kazi ya mchungaji au kiongozi wa dini. Kukubali kuyatelekeza ni sawa na kukubali kufunga Mungu mdomo.

Pili, hata serikali inajua kwamba viongozi wa dini hawawezi kunyamaza. Wala hawawezi kuridhia kile ambacho serikali inataka, hasa ikiwa hicho kinachotafutwa kinalenga kudhoofisha imani za wananchi wake.

Hata Bwana Yesu alipoingia Jerusalemu na kuambiwa kuwa wafuasi wake waache kelele, hakukubali. Alisema, “Wakikaa kimya mawe yatapiga kekele."

Jingine lililokubaliwa ni viongozi hao na serikali kukutana angalau mara mbili kwa mwaka.
Kwangu, kukutana si tatizo. Shida yangu ni kipi kinachoongelewa na kwa manufaa ya nani. Je, nani anapanga ajenda? Uwazi wa kinachojadiliwa uko wapi?

Je, kutakuwa na kukosoana kwa uwazi na upendo, au upande mmoja kutaka kurubuni mwingine?

Hii ndiyo hofu yangu na lazima niiseme. Kwamba kuna hatari ya wananchi kupoteza uhuru wao wa kuabudu. Kuna hatari pia ya kujaribu kunyamazisha sauti ya Mungu.

Kimsingi hii si mara ya kwanza kwa serikali kutaka kuangamiza taasisi za dini. Julai mwaka jana, serikali ilitangaza kuondoa misamaha ya kodi kwa bidhaa zinazoingizwa na taasisi hizo nchini.

Hata kile kinachoitwa “laana ya serikali kwa nyaraka za kidini” kililenga kudhoofisha taasisi hizo. Kushindwa kwa mkakati huo ndiko kulikoibua mkutano wa juzi jijini Dar es Salaam.

Hadi sasa sijafahamu undani wa mkutano huo. Sifahamu ulilenga kuelimisha au kulikuwa na jambo lililojificha. Bali najiuliza: Kama lengo lilikuwa kuelimisha, mbona mawaziri ambao ndiyo watetezi wa sera za serikali hawakuhudhuria?

Mbona sababu zilizotolewa kuwa walikuwa na kazi nyingine, hazikuwa na mantiki? Nani mwenye kazi nzito na nyingi kati ya mawaziri na viongozi wa dini?

Ni jukumu la viongozi wa dini kulinda uhuru wao na ule wa waamini wao. Kukubali kuupoteza uhuru huo ni sawa na kuliasi kanisa.

Kama alivyowahi kusema Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, wa Kanisa Katoriki wakati wa misa ya kuaga mwili wa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza, Anthony Mayala, “Serikali haiwezi kuchagulia kanisa kauli za kuwasiliana na waumini wake.”

Hivyo basi, hatua yeyote ya kushindwa kusimamia kauli ya kiongozi huyo, ni sawa na kupoteza unabii ambao viongozi wa dini wameupokea toka kwa Mungu.

Unabii huo ndio msingi wa viongozi wa kidini kuwasha mishumaa na kuimba usiku wa Pasaka, "…Mwanga wa Kristu... tumshukuru Mungu."

Je, kama viongozi wetu wanakubali kuziba midomo yao, kuna maana gani ya kukesha na kuimba wimbo huu? Naomba turudi katika biblia takatifu na kama tutakuwa wa kweli tutabainisha hilo.

Kingine kikubwa na ambacho kimeniacha mdomo wazi, ni hatua ya serikali kutaka kuwasilisha mswada bungeni wenye lengo la “kutambua” mchango wa madhehebu ya dini katika taifa.

Hapa najiuliza: Nani anataka sheria hiyo itungwe – serikali au viongozi wa madhehebu ya dini? Kama ni serikali, imedhamiria nini?

Mbona mchango wa madhehebu ya dini unafahamika. Hospitali za madhehebu ya dini zinajulika, shule za msingi na sekondari zinaonekana na vyuo vikuu; na hata hospitari za rufaa kila mmoja anaziona.

Binafsi, sioni umuhimu wa kuwapo sheria hiyo. Labda kama kuna ajenda nyingine ya siri. Kuikubali sheria hiyo ni kuingiza madhehebu ya dini katika mtego mwingine.

Ni muhimu tuhoji: Nani ataandaa mswada huu na utapitishwaje? Hawa viongozi wa madhehebu ya dini watakwenda huko bungeni kuujadili?

Sasa hicho kinachokataliwa na serikali cha kuingiza dini katika siasa kinatoka wapi? Mbona huko ndiko kuchanganya dini ndani ya siasa?
Chondechonde! Naomba sana viongozi wa madhehebu mjihadhari na sheria hiyo ambayo ninaiona itahatarisha uhuru wa kuabudu na kueneza dini nchini.

Mkikubali, mtakuwa mmejitia kitanzini ninyi wenyewe.

Nionavyo mimi ni kwamba mswada huu utakuwa hatari, si tu kwa ukuaji wa imani na uenezaji wake, bali hata kwa uhai wa demokrasia.

Madhehebu ya dini ni sehemu muhimu sana ya jamii na ukuaji wa demokrasia. Kuwaweka viongozi wa madhehebu ya dini "mfukoni" ni kutaka kutokomeza nchi.

Viongozi wa dini wanamwakilisha Mungu na watu wasio na sauti – wanyonge. Hii ndiyo kazi yetu tuliyopewa.

Mfano hai ni hapa Kenya. Hivi sasa, kuna mchakato wa kupitisha rasimu ya katiba mpya, ambapo madhehebu ya dini yametoa mchango mkubwa.

Ninasema haya kwa mapenzi mema, si kwa sababu ya kuichukia serikali iliyopo madarakani. Ninayasema kwa sababu ya mapenzi mema na ukereketwa wa kizalendo.

Na sababu nyingine ni ile ya kikatiba ya kutumia akili, vipaji vyangu katika kutoa maoni yangu kwa ujenzi wa taifa langu.

Wakati tunapomsubiri Roho Mtakatifu, roho wa kweli (si wa uwongo); wa uhai(si wa mauaji), wa upendo (si wa chuki), na wa umoja; basi tuandae mioyo yetu ili aweze kutujaza mapaji yake saba.
Kazi mojawapo ya Roho Mtakatifu ni kutengeneza dunia upya; basi namtakia roho huyo alitengeneze taifa jipya.

Mwandishi wa makala hii yupo katika Idara ya Mawasiliano ya Umma, Chuo Kikuu cha Nairobi, Kenya. Mjadala wa viongozi wa madhehebu ya dini na rais Kikwete unaendelea.

0
No votes yet