Viongozi wa dini msile njama na CCM


Padre Baptiste Mapunda's picture

Na Padre Baptiste ... - Imechapwa 19 May 2010

Printer-friendly version
Mtazamo

KONGAMANO la siku mbili lililokutanisha viongozi wa dini na serikali jijini Dar es Salaam wiki iliyopita, haliwezi kupita bila kujadiliwa.

Viongozi hao walikutana kujadili kile kinachoitwa Sheria ya Gharama za Uchaguzi. Serikali imekuwa ikiwatuhumu viongozi wa dini kuwa “wanajiingiza katika siasa.”

Mfano hai, ni kauli za viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) walizozitoa katika mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) mwishoni mwa mwaka jana, ambapo NEC ililituhumu Kanisa Katoliki kwa kutoa waraka wa kichungaji unaokosoa serikali na chama kilichopo ikulu.

Waraka huo ulikuwa unataja sifa za viongozi wanaostahili kuchaguliwa katika uchaguzi ujao. Viongozi wengi waliopo sasa hawana sifa hizo.

Hata hivyo, kauli ya viongozi wa CCM ilijibiwa kwa kishindo na Mwadhama Polycarp Kardinal Pengo wa Kanisa Katoliki, katika misa ya kuaga mwili wa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza, Anthony Mayalla.

Kadinali Pengo aliwakemea wanasiasa na kusema serikali haiwezi kulichagulia kanisa kauli za kuwasiliana na waamini wake.

Kutokana na hali hiyo, kila mwenye akili timamu anajua kuwa kinachofanywa sasa na CCM ni kutaka kujikosha kwa kujionyesha kuwa inawapenda viongozi wa kidini, wakati ukweli ni tofauti.

Watawala wamekuwa wanakerwa na kauli za viongozi wa dini, hata pale wanapokemea maovu katika jamii na ndani ya serikali.

Hali inakuwa mbaya zaidi pale viongozi hao wa dini wanapohubiri uadilifu katika nyumba za ibada, au wanapotaka watawala waache kugeuza uongozi mradi wa kuchumia tumbo.

Serikali inajua kuwa dini ni suala nyeti, na kwamba katika maeneo mengi ikiwamo hapa Kenya, dini imetumika kunyosha watawala.

Hivi sasa, tayari rasimu ya katiba mpya imeingia dosari baada ya viongozi wa madhehebu ya dini kushikilia msimamo wa kuikataa.

Hivyo hivyo, kwa Tanzania ni muhimu viongozi wa dini kuwa kama wenzenu wa Kenya. Ni kwa kufanya hivyo tu, ndiko kunakoweza kuishikisha adabu CCM.

Kila mmoja anajua maovu ya CCM. Anajua kuwa tayari chama hiki kimepoteza sifa ya kutawala. Kimedharau wananchi na kimehama kutoka katika misingi yake ya asili ya kuwa chama cha wakulima na wafanyakazi.

Viongozi wa CCM wamekimilikisha chama chao kwa matajiri, jambo ambalo limechangia serikali kushindwa kutekeleza ahadi zake za kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania.

Katika mazingira haya, viongozi wa dini wana wajibu mkubwa wa kufanya unabii, maana nchi inazidi kudidimia. Lakini hili litawezekana tu, iwapo hawatakubali kuhongwa au kuweka na serikali mikataba itakayowafunga.

Ni lazima viongozi wetu wafahamu kuwa nchi inaelekea kubaya; miaka mitano ijayo hali itakuwa mbaya zaidi kama tutaendelea na serikali hii kwa mtindo huu wa sasa.

Viongozi wa dini waongoze mapambano ya kuleta mabadiliko katika nchi.

Wasiwe sehemu ya kuendeleza ufisadi. Wasiwe sehemu ya kulea maovu na wala wasikubali kuwa sehemu ya kunyamazia vitendo vya rushwa.

Hakika, wanajua kuwa bila yao kusimama imara, Tanzania isingekuwa hapa ilipo leo. Waitumie semina hiyo kuiambia serikali ukweli, kwamba imeshindwa kutawala. Imeshindwa kutetea wananchi wake dhidi ya wanaoitwa “wawekezaji.”

Itakuwa ni aibu kubwa kwao kama watakula njama na CCM na kukubali kupoozwa makali yao. Wakifanya hivyo, watakuwa wamesaliti taifa.

Hata hivyo, bado siamini kuwa Kardinali Pengo, kiongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Alex Malasusa, kiongozi wa Kanisa la Kiangilikana, Askofu Valentino Mokiwa, Zakaria Kakobe, Method Kilaini, Norbert Mtega, na wengineo, watakubali kuisaliti nchi kwa maslahi binafsi.

Ni kwa sababu moja. Wako karibu na waamini na viongozi waliopo; wanajua kinachotendeka. Wanafahamu kwamba kiongozi bora hapatikani kwa kununua uongozi, bali kwa ridhaa ya wananchi kupitia sanduku la kura.

Wanajua kuwa ndani ya CCM kiongozi anapatikana kwa wizi na ununuzi wa kura; vitendo hivyo ni dhambi.

Mwandishi wa makala hii yupo katika Idara ya Mawasiliano ya Umma, Chuo Kikuu cha CUEA, Nairobi, Kenya; amejitambulisha kuwa msomaji wa MwanaHALISI.
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: