Viongozi wa dini wachunge ndimi zao


Paschally Mayega's picture

Na Paschally Mayega - Imechapwa 05 October 2011

Printer-friendly version

MWENYEZI Mungu alimuumba mwanadamu kwa mapenzi yake mwenyewe, lakini akamficha siku yake ya kufa. Maisha baada ya kifo yamebakia kuwa siri kwa mwanadamu.

Wengine wameitumia hali hiyo kueneza hofu juu ya kifo miongoni mwa jamii. Kifo, kwa wengine kinaonekana ni kitu cha kutisha. Wapo wanaodhani siku watakapokufa wao, hiyo siku, itakuwa tofauti na siku nyingine.

Wanadhani kitatokea kitu cha ajabu kama jua kuzama mashariki! Ikumbukwe kwamba, ingawa mwanadamu anayapenda sana maisha ya dunia hii, kifo kwake ni lazima. Hivyo busara si kuogopa kifo, bali kujiweka  tayari kwa kifo chema.

Wanaoitamani pepo ya Mwenyezi Mungu hawapaswi kuogopa kifo! Kwenda peponi hakuna njia za panya, lazima kwanza ufe.

Katika mazingira ya uwepo wa Mungu, uhai na kifo ndipo zilipo dini. Matarajio ni kwamba viongozi wa dini zetu wanawaaminisha waumini wao uwepo wa Mwenyezi Mungu, thamani ya uhai wao na umuhimu wa kifo katika kuwarudisha wanadamu kwa Muumba wao.

Hapa kwetu kuna dini nyingi ingawa kubwa ni mbili; Uislamu na Ukristo. Dini iliyo bora ni ile iliyo kiungo chema kati ya Mwenyezi Mungu na waja wake.

Muumini mwema ni yule anayemcha Mungu na mwenye kuelewa kuwa kila kiumbe kilichopo hapa duniani – hata wanadamu wenye dini tofauti na yake – vimeumbwa na Mwenyezi Mungu. Kudhani viumbe vingine vina mapungufu au dhaifu ni kumkosoa Mungu mwenyewe. Wewe ni nani hata umtoe makosa Mungu wako?

Tunapoanza kuongea udini katika nchi yetu lazima tuwe na tahadhari kubwa kwa sababu maamuma waliishaleta machafuko makubwa katika historia ya dunia hii kwa kisingizio cha dini. Maamuma wanaweza kuwa waumini au viongozi wa dini yeyote.

Dini, kama ilivyotafsiriwa katika kamusi ya Kiswahili Sanifu iliyochapishwa na Oxford toleo la pili ni; ‘1. imani inayohusiana na mambo ya kiroho kwamba kuna Muumba ambaye aliumba ulimwengu huu na kwamba ndiye mtawala wa kila kilichomo; 2. Mfumo fulani wa imani hii na njia ya kuabudu, kusali na kuheshimu/ kutii huyo Muumba kama vile ukristo, uislamu au ubuda”.

Katika muktadha huu utaona kuwa dini zetu hizi zimepokewa na vitu tunavyoweza kuviita viambatanisho. Vitu hivyo kwa mfano utamaduni, mavazi, vyakula, vinywaji, nyimbo na namna ya kuziimba. Wengi wamechukulia kama ndivyo dini yenyewe. Hapana.

Kuna wakati padri anapofanya ibada lazima aimbe. Akiimba anaimba vile vile wanavyoimba mapadri wengine duniani kote. Waumini wengine hudhani kuimba huko kwa padri ndiyo ukristo wenyewe. Hapana.

Ukristo ni dini. Vivyo hivyo Imamu akiimba huimba sawa na Imamu wengine wanavyoimba. Wengine hudhani huo ndio uislamu wenyewe. Hapana. Uislamu ni dini.

Nimelazimika kujadili jambo hili la dini kwa sababu linaashiria hali mbaya huko tunakoenda. Na katika hili baadhi ya viongozi wetu wa dini ndio wahusika wakuu wa kutaka kuleta vurugu za kidini nchini mwetu.

 Kufuatia gazeti hili kuandika, Fatuma, yule  mkuu wa Wilaya ya Igunga jina lake ni la Kiislamu, lakini kwa sababu uislamu si jina, Fatuma yule si mwislamu, ndugu yangu mmoja kupitia simu na 0658 656753 alinitumia ujumbe ufuatao:
“DC. Kimario sio Muislamu. Sasa MwanaHalisi mmetangaza vita na Waislamu. Wewe na Kubenea mna...(tusi) na CHADEMA na padri Slaa.” Huyu alimtusi pia Joster Mwangulumbi akikerwa na makala iliyosema, “Je, serikali ina ndoa na wakristo?”

Ujumbe kama huu hauwezi kunisukuma kutoa angalizo lolote. Mtu anapofika kutukana mhurumie! Akili yake imefika mwisho wa kufikiri. Usimjibu. Usije ukafanana naye.

Viongozi wetu wa dini wasipokuwa waangalifu katika matendo na maneno yao dini zao zitaendelea kuzalisha maamuma ambao kwa kufanya kama alivyofanya huyu ‘ndugu yetu’ watadhani wanaitetea dini yao!

Huenda huyu alikuwa akiitikia tamko la Mufti, Sheikh Mkuu wa Tanzania Issa bin Shaaban Simba aliyesema, “Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania linalaani kwa nguvu zake zote kitendo alichofanyiwa mama Kimario, kwani si tu kwamba kimemdhalilisha na kumfedhehesha mama huyo, pia kitendo hicho kinaashiria dharau ya hali ya juu kwa utamaduni wa Kiislamu. Waislamu tuko macho kuhakikisha kuwa udini unaoendeshwa na CHADEMA unakemewa ipasavyo ili kulinda hali ya utulivu na amani Tanzania”.

Kaimu Sheikh wa mkoa wa Tabora Ally Kondela alisema, “Waislamu tunatamka wazi  hatuna imani na chama  hicho, viongozi tunaomba waislamu wote wasikipigie kura CHADEMA na tunaomba wananchi wapenda amani wasikipigie kura.”

Matamko ya viongozi namna hii ndiyo yanayozalisha maamuma kama huyu ndugu yetu. Hawa viongozi wa dini zetu wameacha kuhubiri maneno ya Mwenyezi Mungu na sasa wanatumiwa na wanasiasa. Ni hatari kwa ustawi wa dini zao. Lazima tuwakemee.

Tusiwaruhusu hata kidogo kuzitumia dini zetu kwa maslahi yao! Kuwaachia viongozi kama hawa waendelee ni kudhalilisha dini zetu. Hawa na waliosema “Kikwete ni chaguo la Mungu” ni lazima wakataliwe na waumini kwakuwa wamekwisha chakachuliwa. Wamekuwa mateka wa wanasiasa. Hakuna dini inayoruhusu utumwa huu.

Kizazi tulichonacho ni cha Dot.Com. Utandawazi, Sayansi na Teknolojia ndivyo vinavyotawala. Masheikh, wachungaji, mapadri na maaskofu wasipolielewa hili mapema ni hatari kwa maisha ya dini zao.

Kung’ang’ania mpaka leo na kudhani kwamba Mungu anaelewa lugha mbili tu, Kilatini kwa wakristo na Kiarabu kwa waislamu ni umaamuma wa hali ya juu. Sawa na kiongozi anayeendelea kuwaaminsha waumini wake kuwa divai siyo pombe kuwa wakati vijana siku hizi wanasomea kemia.

Dini zinapaswa kuleta na kulea amani kwa ajili ya watu wote. Zinapoanza kuwa chanzo cha mitafaruku katika jamii kwa sababu ya viongozi kununuliwa ni hatari kwa maisha ya dini hizo. Muda hautapita nazo zitapita.

0713334239, ngowe2006@yahoo.com
0
Your rating: None Average: 2 (1 vote)