Viongozi wa dini wasivuruge utaifa


editor's picture

Na editor - Imechapwa 02 June 2010

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

MOJA ya misingi mikubwa aliyoiweka mwasisi wa taifa hili, hayati Mwalimu Julius Nyerere ni wa wananchi kuishi pamoja, kufanya kazi popote na kusaidiana bila kujali rangi, dini wala kabila.

Alitaifisha asasi zote za kidini—shule na vyuo—zilizokuwa zinamilikiwa na madhehebu ya dini ili zitumike kwa watu wa rangi zote, makabili yote na dini zote.

Mwalimu Nyerere alijitahidi kueleza sababu za hatua hiyo na viongozi wote wa dini walimwelewa; umoja na mshikamano ulijengeka ukawa mkubwa bila kujali dini na tuliaminiana.

Lakini kuanzia mwishoni mwa miaka ya 1980 yeye akiwa amestaafu, tulianza kumomonyoa msingi huo na kupandikiza ubinafsi kupitia makabila na dini.

Kwa mfano ilitungwa sheria kwamba sikukuu za kitaifa na za kidini zikiangukia Jumamosi au Jumapili zifidiwe kwa kupumzika siku za kazi. Hii ilitupunguzia siku za kufanya kazi za uzalishaji badala ya kuongeza.

Tunashukuru kwamba ilikuja kufutwa. Lakini bado viongozi wa dini wakawasilisha maombi mengine ya kumiliki asasi zilizotaifishwa.

Ndiyo, shule zilizokuwa zimetaifishwa ili ziweze kutumiwa na watu wa dini zote, rangi na makabila yote zikarejeshwa kwa madhehebu ya dini. Haikutosha, kila dini ikataka haki zaidi katika uongozi wa serikali.

Mihadhara ya kukashfu dini moja dhidi ya nyingine ikaanza na kuota mizizi, ukosoaji wa serikali kwa misingi ya dini ukaendekezwa na wakaanza kuhesabu kuna watumishi, wabunge, mawaziri, viongozi wangapi Wakristo au Waislamu katika kila awamu.

Takriban vyuo vikuu na shule zote za madhehebu zimekuwa kama seminari za Kikristo au Kiislamu kwani huchukua zaidi wanafunzi wa dini husika.

Kadhalika ukosoaji wa serikali una misingi ya udini.

Mathalani, ni katika uongozi wa serikali ya awamu ya pili, Waislamu walivunja mabucha ya nguruwe ya Wakristo, na ni katika awamu ya tatu Waislamu walidai kunyanyaswa.

Katika awamu ya nne tumeshuhudia Wakristo wakitoa kile walichoita Mwongozo wa Wakristo katika uchaguzi mkuu na Waislamu wakajibu kwa kutoa wa kwao.

Halafu tumeshuhudia Waislamu wakianzishiwa utaratibu wa kuweka akiba benki kwa misingi ya dini hiyo huku Wakristo wakiachwa waanzishe benki yao.

Kama vile ni mashindano, Wakristo wamekuja na jipya. Katika taarifa ya hivi karibuni, wameitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ibadili siku ya uchaguzi mkuu ili isiwe Jumapili.

Sisi, tunapodurusu mambo haya yote, kwa mapana na marefu, tunaona serikali inarasimisha juhudi za kuwagawa watu kwa misingi ya dini jambo ambalo ni hatari kwa mustakabali wa taifa letu. Madhara ya kila kundi kujali zaidi dini kuliko utaifa ni makubwa.

Tunajiuliza, hivi siku moja tu ya Jumapili katika kipindi cha miaka mitano inaathiri imani ya watu hadi wasahauliwe na Mungu wao? Kuna athari gani zilizopatikana hadi sasa kwa kufanya uchaguzi siku hiyo?

NEC ikikubali maombi hayo, itakuwaje Waislamu wakipinga? Tumeambiwa kuwa NEC na Waislamu wamekataa, hivi Wakristo hawatashiriki uchaguzi huo? Je, haya ndiyo maelekezo ya waraka wa uchaguzi wa Kikatoliki?

Tunapenda kuwashauri viongozi wote wa dini—Wakristo na Waislamu—kwamba nchi hii ni yetu sote hivyo kwa kila jambo wanalofanya, wapime upande mwingine utaathirika vipi.

Maana ni kwa njia ya kuvumiliana ndipo tunaweza kushirikiana kulijenga taifa badala ya kutengana.

0
No votes yet