Viongozi wa watu nongwa za nini?


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 25 July 2012

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

KATIKA kujadili mada “Polisi wavunja sala ya kuombea maiti” wa ajali ya mv Skagit, washiriki wa jukwaa la mawasiliano kimtandao zanzibaryetu.wordpress.com ni kama wanashangilia.

Wanasema sasa hali inaonesha dhahiri uwanja wa mapambano umepanuka. Au nguvu za kupambana, kati ya dola na wananchi zimejijenga zaidi ya ilivyokuwa.

Wanazungumzia mapambano hasa, siyo utani – militancy.

Siamini kama hawajatulia. Naona wametoa hitimisho hili baada ya kufikiria sana hali inayojijenga kwao.

Wamefikiria mwenendo wa utendaji wa Polisi. Aidha, wameangalia namna kundi kubwa la vijana linavyoishi ndani ya ufukara mkubwa.

Bali pia wameangalia namna familia nyingi zinavyoatilika kihali kwa sababu hazina kipato cha kutosha – walichonacho kinazidi kudhoofu, huku gharama za maisha zikiendelea kupanda kiroketi.

Huo ni upande mmoja. Ni upande wa jamii. Upande wa watawaliwa.

Hawa wanaonekana upande wa wananchi ambao kimsingi, ndio wenye dhamana ya uongozi wa nchi yao – Zanzibar.

Kuna upande wa pili ambao wanamawasiliano hawa wameutizama vilevile. Hitimisho lao ndio linathibitisha walivyodurusu vizuri sayansi-jamii na sayansi-siasa.

Wanayaona matatizo. Nitayataja tunavyoendelea.

Tuhamie upande wa pili wa jambo hili – Serikali na viongozi wake, hasahasa wale waandamizi ambao wanaandika sera, sheria na kanuni za utendaji serikalini.

Viongozi wa serikali ndio wenye majukumu ya kurahisisha taratibu za watu wale wa kundi la wengi, kujipatia maendeleo na kukidhi matarajio yao kimaisha.

Nazungumzia maisha ya chuki na hasira. Naona yanazidi kujitengeneza. Wananchi wasio nacho wanaongezeka hivyo; wakati wakubwa wenye nacho, ambao ni wachache, pia wanaongezeka.

Mshindano, mtifuano na msongamano. Kwa sababu tofauti hii ya mapato na staili ya kuishi inaletwa na mwenendo wa uchumaji nchini; lakini ikichangiwa sana na tabia ya serikali kwa watawaliwa, hatari inajengeka.

Kundi la kwanza linajumuisha watu waliochoka kuishi ovyo. Watu wamechoka kuishi maisha ya kubahatisha. Ndivyo inavyoonekana na wanavyoonekana.

Vipi nyinyi mabwana wakubwa, mwacheza mayenu huku wenzenu wakiishi kwa kutegemea mlo mmoja usiotimu kwa siku?

Wanaumia kiafya na hawazalishi kwa kiwango cha kuweza kuchangia katika maendeleo ya taifa. Haya si maisha.

Mifano ya kuchoka ipo mingi. Oneni pakitokea sababu ya watu kukusanyika, inatumika vilivyo. Kila mtu atakaribia hapo aone kuna nini.

Hapo hutokea wachotaji njuruku mifukoni. Hili limekuwa jambo sasa mitaani. Ubakaji mifuko ya watu unashamiri. Umeingia madukani watu wanaponunua vitu.

Wizi umefurtu ada kwenye masoko. Wizi kila mahali siku hizi; hata ule wa mashambani uliozoeleka, umeongezeka sana na wakulima wanalalamika.

Wale wanaokusanyika wakiona kamera mbele yao, huzidisha mcharuko na kupayuka. Ukweli hawapayuki pale, wanaeleza malalamiko yao kwa njia ile rahisi.

Kuzungumza na kamera ya mwanatelevisheni, redio na mwanagazeti, ndiyo staili mjarab kwa watawaliwa kuwasiliana na watawala. Wanaamini, na kweli, ujumbe utafika haraka.

Watu wa Zanzibar wanajuana sana. Wamo ndani ya Jeshi la Polisi, ndani ya Jeshi la Wananchi, ndani ya Intelijenti. Wamo mote humu.

Likibuniwa na kupangwa wanajua. Wanajua siku gani mipango ya kuhujumu au kupambana na raia itatekelezwa. Wanajua. Kwa vipi wasijue, ilhali ndugu na rafiki zao ni watumishi humo!

Wazanzibari wanajuana bwana. Na hili viongozi wakuu wa dola wanapaswa kulitambua vizuri.

Kuna tatizo la watu kuchoka umasikini. Watu wanakosa chakula. Kuna tatizo la vijana kusaga meno kwa kukosa ajira.

Sasa kuna tatizo la watu wa hali hii kuangushwa na serikali yao. Haitoi huduma kama ilivyoahidi. Haina mkazo katika kujenga uchumi mpana ambao matokeo yake yatagusa mafukara.

Kwanini wanamawasiliano wa mtandaoni wakasema nguvu za kupambana dola na raia zinazidi kujijenga? Wanaona namna askari wa serikali wanavyodharau raia.

Sasa askari wameamua kugeukia raia na kuwafanya kama wafanyavyo mabondia kwa gunia la mazoezi – kamata, piga, kanyaga, pondaponda.

Haiwezekani asilani. Wananchi ni binadamu muhimu na kwenye nchi zenye viongozi wanaojua kwanini wapo madarakani, ndio wenye hatamu ya kuongoza nchi yao. Wao viongozi ni wawakilishi tu.

Lakini mbona hata Katiba ya Zanzibar inazungumza vizuri jambo hili? Sura ya Pili na Sura ya Tatu za katiba hii ya 1984 iliyorekebishwa kwa Toleo la 2010, zinatambua haki mbalimbali za wananchi kama zinavyotambua wajibu wa serikali.

Mtindo wa serikali kukandamiza wananchi hauna maana yoyote. Kama una maana basi ni wa serikali yenyewe kujitafutia shari.

Umma una nguvu nyingi. Nguvu za umma ni kuliko risasi na mizinga. Wangeshinda watawala wa Tunisia, Libya, Ivory Coast. Haya yanasemwa mtandaoni.

Serikali inapoagiza askari kushambulia wananchi wanaopata “chakula” cha roho kutoka kwa walimu wao, kwa wapenzi wao kiimani, haina inachotafuta bali chuki.

Mjue nyinyi viongozi mnawajenga watu kuchukia serikali. Na mazoea ni kwamba inapokuwa serikali inayochukiwa tayari imeangusha watu, chuki zinakua zaidi.

Viongozi wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) waache kudanganyana kwamba haitakuwa lolote wakiendelea kukubalia polisi kupiga watu.

Hakuna kisingizio chochote kinachostahili kuifikisha hapo pa kuthubutu kukosa busara na kukanyaga mazulia misikitini na kutawanya watu wanaosikiliza mawaidha.

Pale wanapoona kwa muda sasa muito wa viongozi wa Uamsho unavuta watu wengi, viongozi wanapaswa kukaa na kutafakari, ni kwanini?

Wajiulize kuna nini katika nchi; na wajiulize mara mbili zaidi kunani ndani ya serikali waliyopewa dhamana kuiongoza?

Mwenendo wa kukwepa uwajibikaji na mahali pake kukatoka amri za kimabavu, narudia ni kujitafutia shari.

Viongozi hawapaswi kuongoza watu kama majuha. Wana akili zao. Wasio nazo wako Kidongo Chekundu. Ila, wanapata tiba ya maana kule?

Wale wagonjwa waliopo hospitali kuu na za mikoani wanatibiwa ipasavyo? Walioko mashambani, baharini na misituni wanasaidiwa ili wazalishe zaidi?

Kuna usawa katika kusomesha watoto? Usawa katika kuwapatia ajira upo? Usawa katika kuwapandisha ngazi watumishi upo? Fursa zikipatikana zinagawiwa sawa?

Leo kimezama chombo, serikali imewajibika kuokoa watu? Saa ngapi imefikisha vyombo vya kuokoa? Haya ndio mambo ya viongozi kukaa na kutafakari. Acheni kumsingizia muumba. Basi zitupeni akili alizowapa na uwezo aliowajenga wa kufikiri.

Hivi viongozi mmekaa mkajiuliza mpaka lini mtaanika marehamu wa ajali viwanja vya Maisara? Mnajiuliza? Au mnaona ni sawa tu? Mmeona wapi hili?

Viongozi wenye moyo na fikra sahihi wanatakiwa kufikiria haya na kurekebisha haraka siyo “tuta tuta tuta.” Aibu kwenu.

Wapo vijana wakorofi. Sawa hata Marekani, nchi tajiri, wapo. Hawajulikani walipo na wanapotendea ukorofi wao?

Iweje kudhibiti kikundi cha vijana au hata watu wazima kugharimu watu wenye akili zao wanaopata elimu na taarifa kwa walimu wao?

Si haki serikali kuendesha watu. Wanajiendesha. Wanachagua watakacho, wanaamini waaminicho. Serikali iaminishe watu kwa jambo jema. Watu wasipolitaka basi. Ya nini nongwa?

0
Your rating: None Average: 4 (2 votes)