Viongozi wanapokuwa manyang'au


Joseph Mihangwa's picture

Na Joseph Mihangwa - Imechapwa 18 February 2009

Printer-friendly version

USIRI, ukimya, kulindana, kujikosha, kutokiri ukweli, kutowajibika, kukosa uzalendo na kuweka maslahi binafsi mbele, ndizo sifa mpya zinazokumbatiwa na kutetewa na kada ya juu ya uongozi wa Tanzania.

Wakati tuliomo ni wa utandawazi (utandawizi), rushwa na kuporomoka kwa maadili ya uongozi; ni wakati wa viongozi wasiokuwa na imani kwa lolote watendalo.

Hizi ni enzi za viongozi wanaopima wakati sio wa kutumikia wanaowaongoza, bali kwa kuangalia saa na kalenda kuona walichovuna au kupora katika nchi inayougua umasikini wa kulazimishwa.

Pamoja na kulipwa mishahara minono, marupurupu makubwa na pensheni nzuri ili watumikie kwa wema, uadilifu na tija; viongozi wanaonekana kuemewa na mzigo wa tamaa kwa kujiingiza katika biashara na ukurugenzi wa Bodi za Taasisi za ulaji.

Viongozi tunaozungumzia hapa ni pamoja na wabunge, wakuu wa mikoa, mawaziri, watendaji wakuu wa idara na taasisi za umma na viongozi wa vyama vya siasa.

Kuna utata mkubwa kwa viongozi kuwa wakurugenzi wa taasisi binafsi na za umma, kiasi kwamba ushiriki wao katika shughuli unazingirwa na wingu zito la migongano ya kimaslahi.

Kwa nchi inayoendeshwa kwa misingi ya nguvu ya chama tawala badala ya nguvu ya umma, ambapo maslahi binafsi ya viongozi ndiyo yanayopewa kipaumbele zaidi ya maslahi ya jumla ya umma,  hapawezi kuwa na mipaka ya nini kiongozi afanye na kipi asifanye, kwa sababu hana hofu ya kuhojiwa au kuwajibishwa.

Mbaya zaidi ni pale chama tawala kinapogeuka kokoro la viongozi wenye pesa chafu, zenye sumu kwa umma; kwamba kumhoji kiongozi mchafu, tena kada wa chama, inatafsiriwa kuwa ni kukihoji au kukidhalilisha chama, na hivyo utaitwa ni mpinzani!  Matokeo yake ni kujenga utawala wa kinyang’au usio na tija, wala maslahi kwa wenye nchi.

Kufutwa kwa Azimio la Arusha mwaka 1992 kule Zanzibar, lililoweka bayana utamaduni wa taifa, maadili na miiko ya uongozi, kumeitumbukiza nchi katika shimo la ulafi na ukoloni mamboleo unaoitwa “utandawazi;” usiojua maadili, uzalendo wala umoja wa kitaifa.

Haiwezekani kiongozi kutumikia mabwana wawili bila kuathiri utii kwa mmoja.  Kiongozi hawezi kuwa mjumbe wa Bodi wa Makampuni ya ulaji, na wakati huohuo kuwa kiongozi wa wanyonge bila kuwatelekeza wanyonge hao.

Kwa mfano, kuendelea kuwakamua wananchi kwa mishahara na marupurupu manono kwa wadhifa ulionao, ni njia nyingine ya kuwakamua na kuwatelekeza.

Kama sivyo, kwa nini wizi mkubwa wa fedha za umma (EPA), kupitia makampuni ya Deep Green, Mwananchi Gold, Kiwira Coal Mines, Meremeta, TICTS, IPTL, Richmond/Dowans na mengine unapapaswa papaswa tu, kama si kuwalinda viongozi waliokuwa wakurugenzi wa makampuni hayo?

Kwa nini tunapata kigugumizi kuipitia upya mikataba ya uwekezaji katika Sekta ya Madini, kama si hofu ya kuumbuka kwa viongozi wanaofungwa nira na makampuni ya ulaji?

Viongozi hao si tu kwamba wanakiabisha chama tawala (ambacho hawaamini itikadi yake na serikali yake), bali pia wanawatukana Watanzania waadilifu walioiweka serikali madarakani.

Watanzania wema, na wenye kuitakia mema nchi yao, hawawezi kuruhusu viongozi wao wa juu kuwa watumishi wa wafanyabiashara na walanguzi wengine, wanaokuja nchini kwa jina la uwekezaji.

Viongozi wa juu wanashikilia dhamana ya taifa lenye kuheshimika; ndiyo maana linaingia gharama kuwahudumia kwa jasho la walala hoi wa  nchi hii, ili kuhakikisha kwamba hawaishi kwa kubangaiza

Wananchi hawajahoji kuhusu “mashangingi”, posho, pensheni na mishahara minene kwa sababu wanaamini kwamba hao waliowatuma kwenda “mbali” kuhemea kwa kujinyima, ili walete kilicho kingi nao wapate kushiba, watawaheshimu waliowatuma.  Kinyume chake ni usaliti mkubwa.

Hivi, linapotokea suala tete au kashfa inayohitaji uamuzi wa bunge au serikali juu ya makampuni ya wafanyabiashara au taasisi za umma ambazo wao ni wajumbe au wenyeviti wa bodi, wafanyeje?

Kwanza, wanapashwa kukaa kando ili kampuni au taasisi wanazoongoza zijadiliwe.  Na kama kutaonekana dalili za kashfa zinazowagusa kama wajumbe wa bodi za makampuni hayo, wanapaswa kujiuzulu sawia, kwa sababu wananchi hawakuwatuma kwenda kushiriki kwenye matendo ya ulaji, kinyume cha sheria za nchi.

Kuendelea kwao kubakia katika nafasi za utumishi wa umma, ni kiburi, ujasiri wa kifisadi na kulindana kusikowakilisha matakwa ya umma.

Na kama hali hii itaruhusiwa kuendelea, kuna hatari kazi ya viongozi wa ngazi za juu itakuwa ni kufukuzia nafasi katika makampuni yanayokuja kupora utajiri wa nchi, na kulindwa kwa ushawishi wa vigogo waliomo kwenye bodi za makampuni hayo.

Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Na. 13 ya 1995, iko wazi kuhusu jambo hili. Kifungu cha 6(d) kinasema, “Kuhusu maslahi binafsi, viongozi wa umma wasiwe na maslahi binafsi, zaidi ya yale yaliyoruhusiwa na Kanuni za Maadili,  ambayo  yataathiriwa moja kwa moja au kwa kiwango kikubwa na shughuli za serikali wanazoshiriki”.

Je, kwa kiongozi kushiriki ukurugenzi wa kampuni inayohujumu uchumi wa nchi, si kuathiri vibaya shughuli za serikali?

Na kwa nini wasijing’atue mara moja wanapobainika kufanya hivyo?  Mbunge wa Tabora mjini anapotetea kampuni ya reli (TRL) iliyoboronga, anamsemea nani?

Ukweli ni kwamba, viongozi wetu wanaojirahisi na kukubali “heshima” hiyo ya kuwa wakurugenzi au wenyeviti wa makampuni ya kigeni ni mamluki wakubwa, waliokubali kujiunga na mibaka–uchumi ya kimataifa kufilisi nchi. 

Hili wanalijua, bali ni unafiki na ujasiri wa kifisadi tu unaowabakiza huko kwenye nafasi hizo za undumila kuwili na zinazokinzana.

Kama wanaona kwamba wamewekeza vya kutosha katika makampuni hayo mumiani, badala ya walivyowekeza kwa maendleo ya wananchi, basi wawarejeshee wananchi dhamana yao. 

Nchi haiwezi kusonga mbele kwa kuongozwa na watu wenye kutaka kuwa na vidole katika kila chungu kwa maangamizi ya uchumi wa nchi.

0
No votes yet