Viongozi wetu mabepari wa Venisi


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 22 December 2010

Printer-friendly version
Wazo Mbadala

HAYA yanayofanyika leo nchini—viongozi wazalendo kushiriki kuitafuna nchi—yalishatokea nchi nyingine na yakaandikwa sana.

Mwaka 1594, mtunzi maarufu wa vitabu wa Uingereza William Shakespeare aliona unyama wa mabepari katika nchi hiyo akatunga vitabu kadhaa kikiwemo cha ‘The Merchant of Venice’.

Mwalimu Nyerere, kwa kuzingatia maudhui ya kitabu hicho, hasa dhamira yake kuelimisha Watanzania juu ya hatari ya ubepari na hila za mabepari (wakoloni) katika jamii aliyokuwa anaijenga, alikitafsiri kitabu hicho na kukiita "Mabepari wa Venisi".

Alitaka viongozi wajali dhamana waliyopewa kutumikia watu; wasishirikiane na wafanyabiashara kujilimbikizia mali kwa njia za kifisadi, wala kuingia mikataba yenye mashari magumu. “Ubepari ni unyama,” alifundisha.

Katika kitabu hicho, Shakespeare anaonyesha mtu mmoja aitwaye Bassonio anamshawishi mfanyabiashara rafiki yake Antonio, kuchukua mkopo wa ducat 300 kutoka kwa bepari Myahudi aitwaye Shyloch. Mkopo unaandamana na masharti magumu.

Mkopo huo ulikuwa kwa ajili ya kumsaidia Bassonio aweze kumuoa binti mmoja mrembo aitwaye Portia.

Kwenye karatasi Antonio angemudu kurejesha mkopo huo kwa wakati; Bassonio angemlipa Antonio ambaye pia angerejesha mkopo kwa Shylock hivyo kukwepa adhabu (riba) ya kukatwa nyama kiasi cha ratili moja kutoka kifuani.

Huo ndiyo mkataba. Kwa hiyo, mtu mwenye wajibu wa kuhakikisha nyama haikatwi ni Antonio mwenyewe siyo Shylock. Shylock atafanyia nini bonge hilo la nyama hiyo ni juu yake.

Antonio alitarajia kulipa deni hilo baada ya kuuza vitu alivyoagiza kutoka nje, lakini maskini, taarifa mbaya ikaja kwamba meli iliyokuwa imebeba shehena ya bidhaa zake imezama baharini. Kijana huyo akafilisika ghafla.

Ilipofika siku ya kulipa deni, Antonio alikuwa hoi bin taaban, kesi ikafunguliwa mahakamani dhidi yake na mawakili wa Shylock walisisitiza mkataba uzingatiwe.

Baada ya jaji kupitia ushahidi na vielelezo kutoka pande zote akasema, “…Shylock unaruhusiwa kukata nyama kiasi cha ratili moja lakini usimwage hata tone moja la damu maana mkataba unahusu nyama siyo damu…”

Tunaweza kutofautiana katika tafsiri maana hiyo ndiyo kazi ya fasihi, lakini Shakespeare alilenga kuonyesha kuna viongozi wanaoingia mikataba ya kijinga kama Antonio.

Kwamba kuna viongozi wa aina ya Antonio wanaokopa fedha kwa niaba ya nchi lakini fedha zinakwenda katika miradi isiyo ya uzalishaji na hivyo kuitia nchi kwenye matatizo makubwa.

Mathalani katika miaka ya mwishoni mwa 1970 nchi ilikopa fedha za kununulia silaha za kumpiga nduli Iddi Amini Dada ili kumrejesha madarakani Milton Obote aliyekuwa amepinduliwa Uganda.

Kati ya mwaka 1985-1995 nchi ilikopeshwa fedha kwa ajili ya kusaidia kufufua kilimo cha zao la mkonge lakini fedha hizo ziliishi kwenye mfuko wa mfanyabiashara wa Kiasia—Chavda.

Huo ndio ulikuwa mwanzo wa ufisadi kuotesha mizizi yake nchini—viongozi wakaanza kuitafuna nchi kwa kuuziana nyumba za serikali na wengine wakajigawia mgodi wa Kiwira.

Wakaanzisha kampuni za kuifilisi nchi Meremeta/ Tangold, Mwananchi, Richmond/ Dowans.

Shakespeare alitaka kuonyesha kwamba wakopeshaji wote hawajali utu, bali fedha na utajiri wao na ili wafikie malengo, huweka masharti magumu kwa wakopaji.

Shylock leo ni kama nchi wahisani, kampuni za madini, kampuni kama IPTL, Richmond/ Dowans. Tanesco iko hoi kifedha, lakini lazima itafute Sh 185 bilioni kuilipa Dowans eti imeshinda kesi dhidi ya Tanesco.

Shakespeare anataka kuonyesha kwamba Antonio na Bassonio ni wawakilishi wa viongozi wa nchi maskini kama Tanzania ambao hawajali masharti wanayopewa.

Shakespeare anaonyesha pia madhara ya ubaguzi wa kidini. Myahudi Shylock aliwahi kukosana na Antonio kwa masuala ya biashara lakini safari hii, bepari huyo anasema ana sababu nyingine ya kumpa masharti ya kutoa mtu roho kwa vile Antonio ni mkristo wakati yeye ni myahudi. Jitazameni wakristo na waislamu bado ni wamoja?

0
Your rating: None Average: 4 (2 votes)