Viongozi wetu maskini wa fikra


Paschally Mayega's picture

Na Paschally Mayega - Imechapwa 16 November 2011

Printer-friendly version

IMEANDIKWA katika kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu, “Tumeshikwa lazima tushikamane. Hakuna nguvu yoyote duniani inayoweza kuishinda nguvu ya wananchi waliokata tamaa na kuamua kuwa sasa basi! Liwalo na liwe! Nguvu ya wananchi wenye haki hushinda vita yoyote duniani.”

Hivi karibuni Rais wa Baraza la Maaskofu Mhashamu Yuda Thadeus Ruwa-ich, alisema, “Matumizi ya silaha ama jeshi hayawezi kamwe kuleta amani na ufumbuzi wa matatizo ya nchi. Kutumia mabavu kwa kudhani kuwa ndiko kutaleta utulivu ni kujindanganya na badala yake usalama wa nchi utatokana na uadilifu na ukweli wa wale wote wanaopewa dhamana ya uongozi.”

Fikra nzito huwa hazipotei hivi hivi tu, huendelea kusumbua na binadamu katika jamii huzipuuza bila kujua kuwa ni kwa hasara yake mwenyewe. Mfano ni ya haya yaliyojidhihirisha katika Jiji la Mbeya wiki iliyopita.

Kumbe Polisi na silaha zao si lolote si chochote kwa wanaotetea haki yao. Siku mbili mfululizo mapambano yalilindima katika Jiji la Mbeya huku wanamgambo na polisi wakivurumishwa kwa mawe. FFU walipowatupia mabomu ya machozi walikwepa.

Wakapoteza imani kwa viongozi wa serikali. Amani pekee na imani ya wananchi ikawa kwa Mbunge wao, Joseph Mbilinyi maarufu kama Mr. Sugu ambaye aliwaambia, “Tulieni wanawema”. Wakaisikia sauti thabiti, wakatulia.

Msarafa wa Rais Jakaya Kikwete ulipopigwa mawe Mbeya mwaka 2008 nilimshauri kuwashikisha adabu viongozi wanaomwakilisha sio waliotupa mawe. Kwa nini wawafikishe wananchi mahali waamini kuwa shida zao haziwezi kusikilizwa mpaka aende rais mwenyewe?

Baba hakunisikiliza. Akawasikiliza wapiga porojo waliomwambia kuwa eti wale walikuwa wemelewa. Mlevi gani anakuwa na shabaha?

Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akiwa katika ziara mikoa ya Kusini aliambiwa na mkuu wa mkoa mmoja kuwa hawatasimama katika kijiji kinachofuata kwa kuwa wananchi wake ni wakorofi.

Mwalimu alipofika alisimama akapanda juu ya gari aina ya Landrover akahutubia. Alipoingia ndani ya gari kuendelea na safari akasema, “Gavana (mkuu wa mkoa) wananchi wa hapa hawana matatizo. Wenye matatizo ni ninyi viongozi wao.”

Sheria halali za nchi lazima zilindwe na ziheshimiwe na wote. Na ni katika uelewa huu yazingatiwe pia maneno ya baba wa Taifa mwalimu Nyerere alipowaunga mkono wananchi wa Biafra walipoiasi serikali yao ya Nigeria. Alisema, “Dola zinaundwa kuwatumikia watu; Serikali zinawekwa kuwalinda raia na dola dhidi ya maadui wa nje na wahalifu wa ndani. Ni kwa sababu hizi basi ndipo watu husalimisha haki na nguvu zao za kujilinda kwa serikali ya dola ambayo wanaishi. Lakini vyombo vya dola na madaraka ya serikali, vinapogeuzwa dhidi ya wananchi, basi majeruhi wanayo haki ya kuchukua madaraka waliyosalimisha na kujitetea wenyewe.” Mbeya wameonyesha njia.

Kwa haya yaliyotokea Mbeya, wamachinga wa mikoa yote, wanafunzi wanasomea mavumbini na wale wa elimu ya juu walionyimwa mikopo, wazee wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, wafanyakazi wa kima cha chini na walimu waliopigika, wananchi waliodhulumiwa ardhi yao yenye madini na wageni kwa msaada wa serikali, na wote wanaonyanyaswa na jeshi la polisi kwa kubambikiwa kesi, sasa wanajua kwamba hakuna mtu atakayekuja kuwakomboa.

Lazima watajikomboa wao wenyewe. Watafanikiwa tu ikiwa wataachana na tofauti zao za kiitikadi, kidini, kikabila au kikanda. Nchi na raslimali zilizomo ni mali ya wote.

Akiwasilisha muswada wa marekebisho ya sheria mpya ya manunuzi ya umma ili waruhusiwe kununua ndege, meli, mabehewa na vichwa vya treni vilivyotumika, Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkullo alidai wamefikia hatua hiyo kutokana na gharama ya vifaa vipya kuwa kubwa na kutopatikana kwa urahisi.

Kwake uhai wa Watanzania watakaotumia mikweche hiyo sasa umo kwenye gharama na siyo ubora wa vifaa.

Vitu kama ndege, treni hatukuwa navyo? Vilienda wapi? Nani aliwahi kuona risiti ya mauzo ya mali zetu hizi?

Mkulo anawasilisha muswada huo huku akijua hata wakati walipokuwa wananunua vitu vipya walikuwa wakidanganya. Mfano ndege chakavu iliyonunuliwa kutoka kwa bepari mmoja akiitwa George Hallack. Iliweza tu kuruka na kufika Dar es salaam, haikuweza kuruka tena. Ndipo ikabadilishiwa matumizi, wakaifanya hoteli.

Kwakuwa maadili yalizingatiwa sana wakati ule kuliko sasa, aliyekuwa waziri wa mawasiliano na uchukuzi Augustine Mwingira alipoteza kazi yake.

Mwingine ni aliyeleta kivuko chakavu, akidai kipya alikuwa Mustafa Nyang’anyi. Kivuko kingine chakavu kilinunuliwa katika utawala wa Rais Kikwete kwa ajili ya Mto Kilombero na waliokwenda kuzindua waliondoka bila kuagana baada ya kunusurika kuzama.

Sasa Waziri wa Uchukuzi, Omary Nundu anapofoka akitaka wahalalishiwe kununua vifaa vilivyotumika lengo watakapoua wasilaumiwe? Haya siyo mawazo ya kimaskini tu bali ni mawazo ya kishetani. Wako radhi waue Watanzania lakini malengo yao yatimie.

Wabunge wanawaachia wananchi maswali. Mbunge wa Mbozi Magharibi, David Silinde anauliza, “Baba wa taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikuwa na kitu gani mpaka akaweza kununua ndege mpya, meli mpya halafu sisi tunashindwa?”

Sisi hatushindwi. Sisi ni raia walewale wa Nyerere, wa Ali Hassan Mwinyi, wa Benjamin Mkapa na sasa wa Kikwete. Angekuwa jasiri Silinde angeuliza Nyerere alikuwa na kitu gani mpaka anunue vitu vyote hivyo halafu Kikwete anashindwa? Angempa changamoto Rais Kikwete ajibu. Lakini sasa haijulikani anaulizwa nani.

Mchungaji Peter Msigwa Mbunge wa Iringa mjini akichangia bungeni alisema, “Tanzania sio masikini bali ina watu wenye fikra masikini”

Siyo sahihi kujumuisha Watanzania wote japo kajiingiza na yeye. Angekuwa jasiri angesema, “Tanzania sio masikini bali viongozi wake wana fikra  masikini”

Mbunge mmoja alisema, “Tuache kufikiri tukiwa ndani ya masanduku. Sisi si masikini kwa sababu nchi yetu ina utajiri mwingi. Tunayo gesi nyingi sana. Tuiwekee dhamana tukakope pesa tununue ndege, meli na treni na tukarabati bandari zetu kuimarisha ukuaji wa uchumi huku tukiwasomesha watoto wetu katika mazingira ya kupata elimu bora na wa elimu ya juu wakiwezeshwa kuipata bila nyanyaso na tuboreshe huduma za jamii.”

Mbunge huyo alipuuzwa na wapuuzi! Madhara yake ndiyo haya. Waziri mkuu, Mizengo Pinda anasema maandamano yanamnyima usingizi, bosi wake anasema kelele za mlango hazimnyimi usingizi!


0
Your rating: None Average: 4 (1 vote)