Viongozi Zanzibar hawalindi muungano, bali maslahi yao


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 09 May 2012

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

WAKATI tuliopo, hakuna mtu yeyote mwenye haki ya kuzuia watu kusema. Ni muhimu na haki kwa binadamu kusema anavyojisikia. Zama za “serikali” kuchagulia watu cha kusema zimekwisha.

Katika hali yoyote ile, na hata kama Rais Jakaya Kikwete amesema Watanzania wasijadili kuwepo au kutokuwepo kwa muungano, hakuna kinachosimamisha wananchi kuujadili muungano na hatima yake.

Kwa sababu hiyo, kauli ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohamed Aboud Mohamed kwamba wanaotaka kuelimisha umma kuhusu maoni ya katiba mpya, waombe Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ni kutisha watu.

Hata kama waziri na serikali nzima watasema kauli hiyo imetolewa kwa nia njema, kwa desturi ya viongozi wa Zanzibar, unaposikia kauli kama hiyo basi huwa imelenga kuminya haki.

Desturi kama hii imezoeleka sana. Viongozi hujifanya wanajua kila kitu na kujitia wao ndio wanaona mbele zaidi ya wananchi wanaowaongoza.

Ninaitazama desturi hii kama ishara ya viongozi kujipendekeza kwa Serikali ya Muungano, na hasahasa kwa chama chao – Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Nataja CCM kwa sababu waziri Aboud anamfuata Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, mwana-CCM, kutoa kauli inayoashiria kutisha watu wanaojadili muungano.

Siku zote, viongozi wa Zanzibar hujikweza panapotokea jambo linalogusa uhusiano na Tanzania. Nia ya kufanya hivyo, huwa ni kuonyesha kuwa wanajitahidi “sana” kulinda uhusiano.

Ukweli, wanapofanya hivyo hawalindi muungano, bali wanalinda maslahi yao; wanazidi kupalilia vyeo walivyonavyo.

Ndani ya nafsi zao wanajua kuwa misimamo yao hiyo ya kujitia kulinda muungano kimabavu, inatofautiana na maoni ya wananchi.

Sasa unapokuta msimamo wa wananchi katika jambo hili unatofautiana na ule wa viongozi wao, ujue tunalo tatizo. Lakini, katika hali hii, aghlabu, wenye tatizo huwa ni viongozi. Kwanini?

Asili ya uongozi, ni kuongoza kulingana na matakwa ya wananchi ambao ndio wenye dhamana na uongozi wa nchi yao, ila kwa sababu wao hawawezi kuongoza wote, huitoa dhamana hiyo kwa viongozi wachache.

Kwa hivyo, viongozi wanapaswa kuongoza kwa mujibu wa dhamana waliyopewa na wananchi ambao kikatiba ndio wenye mamlaka ya nchi yao.

Waziri Aboud pamoja na viongozi wenzake wanajua kuwa muungano wa Tanzania ulioasisiwa tarehe 26 Aprili 1964, ndio msingi hasa wa uhusiano uliopo kidola, kati ya Zanzibar na Tanganyika.

Lakini pia, wanajua muungano huu umekuwa ukilaumiwa kuwepo kwake kumeipora Zanzibar mamlaka kwa hata yale mambo ambayo kwa asili ya muungano huu, hayakuwa ya muungano.

Viongozi hao wanajua pia kwamba kwa muda wote wa muungano, miaka 48 sasa, wananchi hawajawahi kupewa nafasi ya haki kusema kama unawafaa au wangependa mabadiliko.

Viongozi wanajua hakika kuwa wananchi wa Unguja na Pemba wamekuwa wakiuchukulia muungano kama kitu kibaya kilichowafunika katika siasa za kimataifa na za ndani ya nchi.

Badala yake, wanaamini muungano huo umetumika kuwaonyesha wao kama ni watu wasiojua siasa njema – wamegombanishwa.

Viongozi wanajua pia kwamba chini ya muungano huo Zanzibar haijanufaika kiuchumi kwa kuwa uchumi si katika eneo linalotazamwa pamoja kimfumo wa muungano.

Hata zile fursa za uchumi wa Zanzibar kukua zimekuwa zikifujwa na upande wa pili kwa sababu msimamizi wa sera na sheria za fedha – Benki Kuu – hawajibiki kwa viongozi wa Zanzibar bali wa Serikali ya Muungano.

Je, wenzetu Ulaya muungano wao unatenga watu wa taifa moja dhidi ya jengine? Asilani abadani, kwa hakika unawaunganisha chini ya Eurozone.

Kwa ufupi, viongozi wa serikali Zanzibar pamoja na wale wa CCM, wanajua kuwa mara kadhaa katika nyakati tofauti mwaka hadi mwaka, Wazanzibari wamekuwa wakiupa muungano majina mabaya.

Muungano kwao ni kama dude linalowanyonya kiuchumi na kiutambulisho mbele ya medani ya kimataifa. Na hili ni kinyume kabisa na Zanzibar ilivyotokana kihistoria. Ikitambulikana hasa.

Hiyo ndiyo hali halisi. Hivi ndivyo namna Wazanzibari walio wengi wanavyouchukulia muungano. Haya siyatungi.

Mjadala ulioanza tangu mapema mwaka uliopita Rais Kikwete alipokuja na wazo la kuanzisha utaratibu wa kuandikwa kwa katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni ushahidi mzuri.

Nilidhani viongozi wetu wameelewa maoni ya wananchi kuhusu muungano na nafasi yake katika kuwasaidia waondokane na mkwamo.

Na hapa napata hofu kwamba ina maana ile mijadala iliyofanyika kupitia asasi mbalimbali za kiraia ni kelele za mlango kwa viongozi wetu? Kwamba hawaoni kuwa wananchi wanatumia haki yao kueleza wanachokiona na kuhimiza wanachokitaka? Haiwezekani.

Hebu niwakumbushe. Wamesahau, Wazanzibari wakiongozwa na Rashid Salum Adiy walifungua kesi Mahakama Kuu ya Zanzibar kutaka serikali iwasilishe “Hati Halisi” ya Muungano kama ilivyosainiwa muungano ulipoasisiwa?

Kwa kumbukumbu zao, Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati ule, Iddi Pandu Hassan, aliieleza nini mahakamani? Alishindwa kuwasilisha.

Alisema yeye hajawahi kuiona na hajui ilipo labda kama wao (walalamikaji) watamsaidia kujua.

Jibu lake linamaana ya kutilia shaka uhalali wa muungano. Mimi ningependa watu waseme. Watasemaje kama wanakwazwa?

Kwa kupenda hivyo, maana yake watu waachiwe haki yao na wapewe uhuru wa kusema wanafikiri nini. Lililo muhimu ni kuwapa wananchi fursa ya kueleza wanachokitaka.

Kwani viongozi wanaogopa kitu gani kuona muungano unajadiliwa kama muungano huo unawahusu watu si viongozi peke yao?

Kama viongozi hawataki watu wajadili muungano na kuamua hatima yake, waakuwa tu wanathibitisha kile kinachosemwa miaka yote, “Wetu ni muungano wa viongozi tu.”

Ni sawa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inayoendeshwa kwa mfumo wa serikali ya umoja wa kitaifa (SUK) imekwepa madai ya kutakiwa iitishe kura ya maoni ili kuwauliza wananchi kama wanautaka muungano na kama wanautaka, uwe wa mfumo gani.

Lakini, viongozi hao wajue kuwa kukwepa huko ni sawa na mtindo wa mbuni kujificha kwenye minjugu akidhani haonekani. Kumbe, shingo yote iko nje.

Na wenyewe wanaahirisha tu tatizo, bali manung’uniko hayatafutika hata baada ya katiba mpya kupatikana. Wananchi watatoa hisia zao tume itapowafikia, na watabaki na maoni yao hata wakipuuzwa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: