Vita Dhidi ya Ufisadi: Nafasi ya vyombo vya habari


Rehema Kimvuli's picture

Na Rehema Kimvuli - Imechapwa 15 July 2008

Printer-friendly version

UFISADI ambao umegeuka 'wimbo wa majanga' nchini una mizizi katika awamu za kwanza za utawala hasa awamu ya tatu ya Rais Benjamin Mkapa.

Hii ni kutokana na kashfa nyingi za ufisadi kuwa zimeanzia katika awamu hiyo na kuendelea awamu ya sasa ya Rais Jakaya Kikwete.

Kwa mfano, wizi wa fedha za akaunti ya madeni ya nje (EPA) kwenye Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ulifanyika wakati Mkapa akiwa madarakani.

Mikataba ya kuchimba madini pamoja na mikataba ya kufua umeme kama ule wa IPTL, nayo iliingiwa kabla ya utawala wa sasa. Mkataba wa IPTL ulifungwa wakati wa utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi.

Unaweza kujiuliza kwa nini basi ufisadi haukugundulika au kupigiwa filimbi wakati huo wa awamu ya tatu.

Kuna tofauti ya staili ya utawala kati ya Mkapa na Kikwete, ingawa wote wanatoka chama kimoja – Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Tofauti hiyo ni kwamba serikali ya sasa imeonyesha uvumilivu kwa tuhuma na shutuma zinazotolewa na wananchi.

Malalamiko ya wananchi kupitia vyombo vya habari, yamekuwa yakipokewa serikali; hata yanapokuwa makali na machungu, na bila ya vyombo vya habari kudhalilishwa au kukemewa na rais.

Kuna mambo mawili muhimu. Kuna kukubali kupokea taarifa na kuzifanyia kazi. Ingawa hakuna ushahidi hadi sasa kuwa Mkapa na Kikwete wanapishana katika kutekeleza wanayoambiwa na wananchi, Mkapa alikuwa anatumia mno vitisho.

Ni Mkapa aliyesuta na kufokea waandishi wa habari wa Tanzania akiwaita 'uchwara.' Hali hii, si tu iliwatisha waandishi wa habari, kwa kauli ya rais, moja kwa moja walikuwa wamedhalilishwa.

Kudhalilishwa kwa waandishi husambaa hadi kwa wamiliki wa vyombo vya habari; na wamiliki wanapokosa ujasiri, basi nao hufyata na serikali huendelea kutunisha msuli na kufanya inavyotaka bila ya hata taarifa zake kuripotiwa.

Ndivyo ilivyokuwa wakati wa Mkapa. Kipindi cha ongezeko la uwekezaji kutoka nje pamoja na ubinafsishaji ndicho mara nyingi, na popote duniani huandamana na vituko vya wizi na ufisadi usiomithilika.

Serikali ya Kikwete imekuwa tofauti kidogo. Ingawa baadhi ya viongozi wake wanachukia matendo mabaya ya serikali kuanikwa, yeye hajaonyesha kutaka kudhibiti kauli za wananchi kupitia vyombo vya habari.

Ni tabia hii ya utawala wa Kikwete iliyofanya taarifa nyingi kupatikana na hivyo kuanikwa. Kuna jambo jingine lililosababisha kukua na kusambaa kwa taarifa za ufisadi.

Wananchi wamepata mwamko zaidi. Kupatikana kwa mwamko kumefanya wananchi waseme kinachowakera; wadai haki zao; wapiganie uhuru zaidi wa maamuzi na walioko maofisini wamejisikia vizuri watoe taarifa zinazoendeleza ufisadi nchini.

Kwa hiyo, wakati staili ya utawala katika awamu ya tatu ilisaidia serikali kuficha ufisadi, mlipuko wa taarifa za ufisadi katika awamu ya nne umetokana na uwazi kidogo ulioshinikizwa na wananchi wanaotaka kujua hili na lile.

Ni kwa mtindo huo kashfa kama ile ya kampuni ya Richmond, ilifahamika. Kukua na kupanuka kwa taarifa za ufisadi katika mkataba wa kufua umeme kati ya Shirika la Umeme (Tanesco) na Richmond kulitokana na mazingira haya.

Mkataba huu ulilalamikiwa na baadaye kuthibitishwa kuwa utoaji zabuni kwa kampuni hiyo ulikuwa umegubikwa na upendeleo na hivyo kukiuka taratibu.

Mchakato wa zabuni ulihusisha aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa ambaye, baada ya uchunguzi wa Kamati Teule ya Bunge, alilazimika kujiuzulu.

Mawaziri wengine wawili, Nazir Karamagi na Dk. Ibrahim Msabaha, walijuzulu pia kutokana na kashfa hiyohiyo.

Hivyo ndivyo pia kashfa nyingine zitakavyogundulika, kuanikwa na kufuatiliwa. Lakini kilicho muhimu hapa ni kupatikana kwa upenyo wa kupitishia habari na taarifa ambako hasa ndiko kunaleta mabadiliko.

Kupatikana kwa taarifa juu ya ufisadi ni muhimu. Anayeziba upenyo wa taarifa anaweza kuitwa adui wa umma. Kwani ni taarifa hizi zinazoshinikiza hatua ya kuondoa kile kinachoudhi au kuumiza wananchi.

Ufisadi unachochea umasikini wakati Taifa lina raslimali nyingi. Unaongeza gharama za kuendesha nchi; unafanya maisha ya wananchi kuwa magumu kutokana na kuongezeka kwa gharama za bidhaa muhimu.

Kukosekana kwa elimu na vifaa vya elimu; dawa katika zahanati na hospitali; miundombinu ya kijamii, kwa mfano maji safi na salama na barabara; vyote vinatokana na utumiaji ovyo na ufisadi wa raslimali za nchi.

Ni ufisadi, kama ilivyo rushwa, unaodhoofisha utawala, kwa mafisadi kudai wamewaweka watawala mfukoni na kutamba kuwa wao ndio wanatawala. Kwa hapa, utawala bora huwa ndoto kustawi.

Yote haya yana maana kuwa wananchi ndio wanaobeba mzigo wa gharama unaotokana na matendo ya ufisadi. Hilo ndilo linaleta umuhimu wa kuibua taarifa za ufisadi haraka iwezekanavyo ili uweze kushughulikiwa mapema.

Ni kwa njia hii pia taifa linaweza kuzuia upotevu wa fedha na raslimali za nchi; ikiwa ni pamoja na kuziba mianya ya kuingia katika madeni yasiyo lazima.

Utoaji taarifa juu ya rushwa na ufisadi mwingine ndio njia kuu ya mapambano ya kusafisha jamii. Kusiwepo wanaokingiana kifua. Wanaofichiana maovu. Wanaoendelea kuumiza wananchi waliowachagua na kuwaingiza madarakani.

Hili si jukumu la vyombo vya habari peke yake. Ni la wananchi mmojammoja na hasa watawala ambao lazima wachukuwe hatua za kuangamiza adui wa maisha na ustawi wa jamii.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: