Vita ya mafisadi imeanza kushinda


Stanislaus Kirobo's picture

Na Stanislaus Kirobo - Imechapwa 22 September 2009

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

MAFANIKIO ya vita dhidi ya ufisadi yameanza kuonekana. Ni kwa sababu umma umeanza kuelewa na kuunga mkono mapambano haya. Hii ni hatua kubwa katika kufanikisha vita hii.

Hakuna anayeweza kubisha kwa nguvu za hoja kwamba ni pesa tu walizopata kwa njia za kifisadi ndizo zinazowawezesha mafisadi kuonekana wanatamba hadi sasa.

Kwa maneno mengine, wanatumia pesa kuinunua haki na uhalali wa kuendeleza mapambano, ingawa wana hoja dhaifu mno.

Kwa mfano, magazeti mengi uchwara yaliyozuka wakati wa kilele cha mapambano sasa "yamepungua" na mengine yamekufa.

Kielelezo cha hili ni kwamba wahariri wa magazeti hayo hukubali kutumika kwa malipo kutoka kwa mafisadi, na kama hakuna malipo, basi hakuna magazeti, na hakuna mahali pa kupitishia hoja zao dhaifu na potofu.

Pia wapo baadhi ya waandishi waandamizi na wahariri wa magazeti yanayoheshimika ambao huandika habari na makala za kuwatetea mafisadi makusudi katika masuala kadhaa. Tayari baadhi yao nao wameanza kurudi nyuma kwa sababu ileile – pesa zinaanza kukauka.

Pamoja na hayo yote, wiki iliyopita wapiganaji wa ufisadi walipata ‘msaada’ mkubwa kutoka sehemu moja ambayo ingawa ilikuwa inatarajiwa haikufikiriwa kuwa ungekuja mapema kiasi hicho na kwa namna ile.

Unaweza ukasema kwamba "msaada" huu pia ulikuja kwa hisani ya chama tawala – Chama Cha Mapinduzi (CCM), kutokana na udhaifu mkubwa wa viongozi wake wakuu ambao wanazidiwa nguvu na mafisadi ambao walionekana kufanikiwa kukiteka chama.

Magazeti kadha yalieleza kwa undani kilichojiri katika kikao cha halmashauri Kuu ya chama hicho (NEC) kilichofanyika Dodoma mwishoni mwa mwezi uliyopita ambapo baadhi ya wajumbe waliandaliwa kumsulubu na hata kutishia kumfukuza uanachama Spika wa Bunge, Samwel Sitta.

Dhambi yake kubwa, kama ilivyoelezwa, ni kutoa uhuru kwa wabunge kujadili kwa mapana mustakabali wa taifa lao; na kulindesha Bunge bila upendeleo na hivyo kuhatarisha uhai wa chama hicho.

Kwa kauli ya baadhi ya wajumbe akiwamo mkongwe wa mizengwe, Kingungo Ngombale- Mwiru, Spika Sitta alikuwa anaruhusu mijadala na hoja zilizokuwa zinaiweka serikali mahali pabaya.

Madhambi haya ya Sitta pia yalitajwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Tanzania Bara, Pius Msekwa, katika barua aliyowaandikia mabalozi hapa nchini katika kuhaha kufafanua kilichojiri, walipohoji nia ya NEC kumuweka kiti moto Sitta.

Ufafanuzi wa Msekwa bila shaka ulikuja kutokana na vitisho vya kukatiwa misaada na wafadhili hao hao kutokana na jinsi serikali inavyoiendesha vita dhidi ya ufisadi kwa njia ya kubabaisha babaisha tu.

Msekwa hakuwa anawaambia mabalozi ukweli, au tuseme hakwenda kwa undani zaidi katika ufafanuzi wake, kwani kiini hasa cha kusulubiwa Sitta ni msimamo wake kuhusu ufisadi.

Mijadala na hoja nyingi alizokuwa anaziruhusu Bungeni ni zile zilizokuwa zinawatuhumu baadhi ya maofisa wa serikali na viongozi wengine, wa sasa na wa zamani, kwa ufisadi. Kiini cha mtafaruku wote uliojiri katka sakata la Sitta ni hili tu. Mengine ni porojo.

Na kwa bahati nzuri mabalozi si wajinga, wanajua kila kitu kinachoendelea katika nchi hii, hususan ndani ya utawala, na hasa katika suala la ufisadi kwani nchi wanazoziwakilisha. Wao ni wadau wakuu katika kuchangia fedha za bajeti na miradi mingine, wasingependa kuona pesa zao zinatafunwa na wachache.

Kitu kilichowashtua sana mabalozi ni pale ilipotangazwa, baada ya kikao cha NEC, kwamba Sitta na kikundi cha wabunge kadha wa chama hicho ambao wako mstari wa mbele dhidi ya ufisadi hawatakiwi na watashughulikiwa.

Kwa hivyo hali inayojitokeza sasa hivi (kauli ya Katibu Mwenezi wa CCM, John Chiligati akimsifu Dk. Harrison Mwakyembe (mbunge wa Kyela) kwa kazi nzuri anayofanya; huku Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba akimfuata Sitta na kummwagia sifa majukwaani tena ndani ya jimbo lake, na kuomba wapiga kura wamchague tena eti kwa vile anafanya kazi nzuri aliyotumwa na chama, ni unafiki wa hali ya juu, lakini pia ishara kwamba wapambanaji hawa wakijipanga vema, mafisadi watakwama.

Maana viongozi wale wale ndio walioongoza vikao vilivyowasulubu wabunge hao na Spika, na ndio waliotoa matamko ya chama kwamba ni halali kwa chama kuwashughulikia kwa sababu wakiaibisha nje ya vikao vya chama.

Huu urafiki wa ghafla kati yao hauna lolote. Ni unafiki mtupu, na njia ya kuwadhulumu wabunge hao. Hata hivyo, wananchi wana imani kwamba wabunge hao wanajua wanachofanya, na wanajua janja ya viongozi wao wanaotoa kauli za kujikanganya, huku wakitafuta upenyo wa kuwamaliza ‘wabaya wao’ kisiasa.

Na hiki kigeugeu cha akina Makamba ni ishara kwamba pesa za mafisadi zina ukomo. Haziwezi kununua kila kitu na haziwezi kumnyamazisha kila mtu. Kwa kutazama mbali, tunaweza kusema hii ni ishara ya ushindi dhidi ya mafisadi.

0
No votes yet