Vitambulisho kama RADA


Joseph Mihangwa's picture

Na Joseph Mihangwa - Imechapwa 04 March 2009

Printer-friendly version

NI hadithi ya kenge. Hasikii hadi damu imtoke masikioni. Hivyo ndivyo walivyo viongozi wengi wa Tanzania.

Yale ya rada sasa yanafanana na ya vitambulisho vya kitaifa. Ni nyumba ya “bwana haambiliki.”

Waingereza walishindwa kukubaliana iwapo kweli nchi masikini kama Tanzania, ilihitaji rada ya kuongoza ndege ya thamani ya mabilioni ya shilingi.

Walivutana iwapo Tanzania, pamoja na umasikini wake, ilihitaji rada mbovu, tena ya kununuliwa kimya kimya na kwa mwendo wa kuruka.

Waziri Mkuu wa Uingereza wa wakati huo, Tony Blair, alikwaruzana na mawaziri wake – Waziri wa Fedha, Gordon Brown (sasa Waziri Mkuu), na Waziri wa Misaada ya Maendeleo ya kimataifa, Short Clare ambao hawakutaka Tanzania inunue mzoga.

Hapa nchini, kelele zilizopigwa na wenye kuitakia mema nchi yao, vikiwamo vyombo vya habari, wabunge, wachumi na wasomi wengine zilipuuzwa.

Ni miaka kumi sasa ya kujitahidi kulindana na kunyamazishwa suala la rada. Chunga jinsi vigogo wanavyobubujikwa jasho kutokana na uchunguzi unaofanywa na kikosi cha Uingereza cha Upelelezi wa Makosa Makubwa ya Jinai (SFO).

Ufisadi kwa staili ya ununuzi wa rada ungali unajirudia nchini. Angalia sakata la mradi wa vitambulisho vya taifa. Hapa watawala wanasema wanaweka mbele maslahi ya chama kilicho ikulu.

Hivi majuzi katika suala la kulinda mtuhumiwa wa kuingilia mchakato wa zabuni ya vitambulisho, mzee Kingunge Ngombale-Mwiru, alisikika akitoa kauli zinazolinga na kusema heri chama kibakie lakini, potelea mbali watu na taifa.

Eti waziri mtuhumiwa, Lawrence Masha wa Wizara ya Mambo ya Ndani, alindwe ili chama kisipate pengo kwa kupoteza waziri na hiyo ikawa kashfa ya kukipunguzia mbwembwe. Ni kauli zinazofanana na zile za kutetea rada.

Benki ya Dunia, Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO) na Shirika la Misaada la Kimataifa la Uingereza (OXFAM) walilaani hatua ya Uingereza ya kutaka kuiuzia Tanzania rada aghali na mbovu.

Tony Blair alitamani kulinda kampuni ya BAe ya jimboni kwake ambayo ilikuwa ipunguze wafanyakazi 250 kutokana na kufilisika. Mzigo akaivisha Tanzania.

Lakini Machi 2002, Rais Benjamin Mkapa, alitoa tamko akiwa Australia, “Hakuna hata mmoja ambaye amenipa hata chembe ya ushahidi kuhusu rushwa…Kandarasi hii imekamilika, na hakuna jingine tena.”

Leo Mkapa anajisikiaje mbele ya umma wa Tanzania. Uko wapi mkweche wa rada alioutetea kwa nguvu zote? Anajisikiaje anapoona waliokuwa viongozi wateule wake wanaumbuliwa kwa kuficha mabilioni ya shilingi ughaibuni?

Mkweche wa rada ulifuatiwa na mkweche wa ndege. Iko wapi ndege ya rais ambayo wananchi waliambiwa afadhali wale nyasi lakini inunuliwe?

Yuko wapi Shaileth Vithlani, kiungo kikuu cha miradi hii ya kitapeli? Si ametoroka nchini huku wahusika wakimwangalia?

Ni majuzi tu tumeona jaribio jingine la kutaka kupora Watanzania kupitia mradi wa vitambulisho wa thamani ya Sh. 200 bilioni. Waziri anadaiwa kuifanyia upatu kampuni ya nje ya Sagem Securite.

Kumbe tutaendelea kuzama: Ni mkondo uleule wa miradi ya umeme ya IPTL, Richmond/Dowans na makampuni mengine. Lakini ipo siku damu zitawatoka kenge masikioni; hapo ndipo watakaposikia.

0
No votes yet