Vitambulisho vimeanza kutafuna wakubwa


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 01 September 2009

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

ZOGO la kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi, sasa siyo tena mgogoro kati ya serikali na Chama cha Wananchi (CUF) pekee. Ni zogo lililotapakaa hadi katika taasisi za serikali.

Taasisi za serikali ambazo kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar zinapaswa kutekeleza majukumu yao kwa kutambua na kujali maslahi ya wananchi, zenyewe tayari zimeanza kutoana macho zikishutumiana.

Kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi, ndicho kinachotoa haki kwa raia wa Zanzibar kuingizwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura (DKWK) la Zanzibar. Hili ni sharti la kisheria lililoingizwa na serikali katika kwa kila Mzanzibari.
 
Mgogoro umepata wahusika zaidi kutoka hao ambao kwa muda sasa wamekuwa wakisikika kutoa kauli za kulumbana kuhusiana na mahitaji hayo. Viongozi wa CUF wakituhumu serikali kupanga mpango wa kunyonga haki za wananchi na serikali kukanusha.
 

Ni baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Khatibu Mwinchande kulalamika kwamba kitambulisho hicho ndio chimbuko la mvutano kati yao na wananchi uliofikia kukwamisha uandikishaji wapiga kura, amejiwa juu.
 
Tofauti na ilivyozoeleka kwamba Tume ikishutumiwa tu na vyama vya upinzani, safari hii imeshutumiwa na taasisi ya serikali inayohusika na usajili wa wananchi na utoaji wa kitambulisho hicho.
 
Idara ya Usajili na Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, iliyoko chini ya Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), ilianzishwa kwa sheria ya Baraza la Wawakilishi ya Mei 2005.
 
Mohamed Juma Ame, Mkurugenzi wa idara hiyo ametupa lawama nzito kwa Tume ya Uchaguzi kwa maelezo kuwa inafanya kazi zake kwa kusikiliza shinikizo za kisiasa.
 
Anasema uamuzi wa Tume kusitisha uandikishaji wapiga kura uliokuwa umeanza kisiwani Pemba tangu 6 Julai, umefanana na tamko la CUF lililotolewa 20 Agosti na washiriki wa kongamano la wadau wa uchaguzi lililofanyika ukumbi wa Karimjee, mjini Dar es Salaam.
 
Mohamed amekuwa akitaja kile anachoita changamoto kwa Tume kwamba hata ikitenda kwa ufanisi kiasi gani, haitaweza kuandikisha wapiga kura wanaofikia 503,895 ambao ofisi yake imewapatia kitambulisho hicho.
 
Lakini sasa Mohamed, ambaye kabla ya kuzuka mgogoro wa kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi alikuwa hajajitokeza hadharani kama mtendaji mkuu wa ofisi inayosimamia usajili na utoaji kitambulisho hicho, anaonekana dhahiri kuishiwa uvumilivu.
 
Ukweli ni kwamba ameanza kukasirika. Na matokeo ya hasira zake, ni kutoa lawama na shutuma kwa yeyote anayeona anajitahidi kueleza ambacho yeye anafikiria si sahihi na hakilingani na matakwa ya utendaji katika idara anayoongoza.
 
Zaidi, naona Mohamed amekwenda mbali sasa. Ameanza kupiga siasa badala ya kusimama katika utendaji wa kitaalam. Alipoinuka na kuanza kutoa mada katika kongamano la wadau wa uchaguzi mkuu Karimjee, alisema siasa si fani yake na kwa hivyo angeeleza mambo ayajuayo kwa kuzingatia takwimu si kauli za kisiasa.
 
Alitakiwa kutoa ufafanuzi wa malalamiko yanayoshamiri ya wananchi kunyimwa kitambulisho kwa sababu za kisiasa, ndipo alipoanza:
 
“Kama nilivyotambulishwa, mimi si mwanasiasa. Sitazungumza siasa hapa bali maelezo yangu yatatokana na takwimu za utendaji wa idara ninayoongoza.”
 
Ameshatishia kumshitaki Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad kwa kile alichosema “ametoa tuhuma kwamba kuna watu wanapatiwa kitambulisho cha Mzanzibari mkaazi Mkuranga na Pangani.”
 
Mohamed ameshatishia kukamata viongozi wengine wa CUF kwa madai kuwa wanahamasisha wananchi kujitokeza kwenye vituo kudai kitambulisho ilhali wapo ambao wameshapatiwa na ofisi yake imeshatoa kitambulisho kwa watu wale zaidi ya 503,000.
 
Ni Mohamed huyu ambaye amekemea mabalozi wa Ulaya, Canada, Marekani na Japan kwamba wametoa tamko la kulalamikia matatizo ya uandikishaji wapiga kura kwa kusikiliza madai ya upande mmoja. Alimaanisha kuwa mabalozi hawakuwa wamefanya utafiti wa kutosha kabla ya tamko lao.
 
Fikiria suala linalohusu serikali, likagombanishe taasisi za serikali. Kwamba mkuu wa idara inayotoa vitambulisho ambavyo vimewekwa kama sharti la kisheria kwa mtu kupata kuandikishwa katika daftari la wapiga kura, anasuguana na Tume ya Uchaguzi, ni jambo la kufurahisha kwa maana ya tatizo liliopo.
 
Msuguano wao umepanua wigo wa tatizo la vitambulisho. Mohamed hajajiegemeza katika kutoa maelezo fasaha ya sababu za kitambulisho kutolewa katika misingi ya kibaguzi, tena ukawa ni ubaguzi wa kisiasa. Hajaeleza.
 
Wakati hajaeleza hilo vizuri, anakemea Tume ya Uchaguzi ambayo mkurugenzi wake, Salum Kassim Ali, ameteuliwa na Rais kama ilivyo yeye.
 
Eti Mohamed, ambaye sasa jina lake limeanza kuwa maarufu ndani ya vinywa vya wananchi wa Zanzibar, analaumu viongozi wa CUF na kuwatishia kuwakamata na kuwashitaki mahakamani kwa uchochezi.
 
Baada ya yote hayo, Mohamed anathubutu kukemea mabalozi wanaofanya kazi kwa uangalifu mkubwa katika nchi wanayoifadhili kwa kila kitu.
 
Hapa panataka tafakuri ya ndani. Lipo jambo. Kwanini ofisa wa serikali ambaye idara yake si katika idara zinazotarajiwa kuwa na watendaji wapayukaji, anarukia mabalozi, watu wanaoheshimika popote duniani?
 
Kwa akili yake Mohamed anataka Wazanzibari waamini leo kuwa mabalozi wanafanya kazi kwa kubahatisha. Kwamba hawana uhakika na wanachokisema; haiwezekani hata kidogo. Hao si mabalozi waliozoeleka namna wanaavyofanya kazi zao.
 
Lakini wakati Mohamed anakemea mabalozi kwa kutofanya utafiti wa kutosha, inafahamika kwamba kumbe walioshatuma maofisa wao hadi kisiwani Pemba na kukagua uandikishaji unavyokwenda.
 
Kwamba mabalozi walitoa taarifa za ndani walipokutana na Rais Amani Abeid Karume na kutoa kilio cha yale yanayofanyika vituoni, inamsuta Mohamed kwamba yeye ndio amekurupuka kuwarukia mabalozi.
 
Walishafanya utafiti wa kutosha ndio maana baada ya kujenga hoja zao za umuhimu wa kukutana na Rais Karume kwenye makao yake mjini Zanzibar, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania, Bernard Membe alikubali kufuatana nao.
 
Na Waziri Membe akafafanua mengi yaliyosemwa katika mkutano wa mabalozi na Rais Karume; huku akitaja kabisa kwamba mabalozi walimweleza mwenyeji wao kuwa wametuma maofisa wao kuangalia hali ilivyo Pemba.
 
Nani sasa ambaye hakufanya utafiti? Ni Mabalozi au Mohamed?
 
Ndo maana nasema wigo wa mjadala wa tatizo la vitambulisho umepanuka. Baada ya Mohamed kutafuta kujivua lawama za uovu unaotendeka, anajikuta mzigo ungali umemuelemea.
 
Umemuelemea kwa sababu sasa hata Tume ya Uchaguzi inayoongozwa na Mwenyekiti Khatibu Mwinchande, imeshasema katika hali ya mtafaruku uliojitokeza, wenyewe wamenukuliwa katika vikao vya ndani wakisema, “Hatuko tayari kubeba takataka za mtu.”
 
Kuna rai imetolewa na wachambuzi katika kutatua mgogoro wa kitambulisho. Watu wasimamishwe gwaride; Mohamed, huyu anayesema ameshatoa vitambulisho 503,895 aite mmoja baada ya mwingine kuona iwapo vitambulisho alivyonavyo vina wenyewe kweli. Wakati utasema!

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: