Vitambulisho vya taifa kwa nini?


Stephen Gidamarirda's picture

Na Stephen Gidamarirda - Imechapwa 25 January 2011

Printer-friendly version

RAIS wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa aliwahi kuasa; “Nchi mskini kama Tanzania ni lazima iwe na vipaumbele katika mipango yake ya maendeleo.”

Alichomaanisha Mkapa ni umuhimu wa mipango ya maendeleo ya nchi kuendana na vipaumbele na uwezo wa kutekeleza mipango yenyewe.

Mipango iliyozingatia vipaumbele itaondoa tabia ya kuwepo mipango mingi kwa pamoja lakini utekelezaji wake ukawa mgumu kutokana na uwezo mdogo wa kibajeti.

Kadhalika, mipango ya nchi inapaswa kuhimiza serikali kujenga uwezo wa kujitegemea kabla kuamini kuwa inaweza kutekelezaji kila mipango kwa kutegemea misaada na mikopo.

Ushauri unatekelezeka?

Tangu ilipoingia madarakani Desemba 205, serikali ya awamu ya nne inayoongozwa na RaisJakaya Kikwete imebuni mipango mingi ya kulitoa taifa katika umaskini unaozidi kukithiri kwa watu walioko mijini na vijijini.
 
Kuna mipango ya kugawa vyandarua bure, ruzuku ya pembejeo za kilimo na mifugo. Mipango inayoelekeza wananchi kujitegemea, inalazimisha wananchi wenyewe kushirikishwa ili wajenge imani kwa mipango hiyo.

Kwa mtizamo wangu, mradi wa vitambulisho vya taifa hauonekani kama unakwenda katika mwelekeo wa kusaidia nchi kuondokana na umasikini.

Je, ni kweli kwamba kwa mpangilio wa mahitaji ya nchi kwa kuyapa kipaumbele stahiki kulingana na umuhimu, uzito, uhitaji na ulazima, zamu ya vitambulisho imefika?

Takwimu zinaeleza kuwa asilimia 12 ya Watanzania ndio wanaopata huduma ya nishati ya umeme. Maana yake, asilimia 88 ya watu wanaishi kwa kutegemea nishati mbadala ikiwemo kutumia kuni.

Ripoti ya serikali inaonyesha kwamba shule nyingi nchini hazina nyumba za walimu na maabara; vijiji vingi havifikiki kwa kukosa barabara; huduma ya maji bado haijaenea vya kutosha mijini na vijijini.

Vilevile ripoti inaonyesha askari polisi wengi bado wanaishi kwenye vibanda vya bati maarufu kama ‘fulsuti’ huku hospitali na vituo vingi vya afya vikikosa dawa na vitanda.

Matatizo ya upatikanaji wa huduma nzuri za kijamii yanaendelea wakati viongozi wa serikali wakisema yanatokana na ukosefu wa fedha.

Katika mazingira kama hayo, hivi kweli vinahitajika vitambulisho vya taifa kuliko huduma za afya, nyumba za polisi na walimu, umeme, barabara nzuri au pembejeo na zana za kilimo?

Ni wapi kilio cha kutaka vitambulisho vya taifa kimetoka? Sababu zake ni nini hasa?

Ni takriban miaka 50 sasa watu wanaishi bila ya kuwa na vitambulisho vya taifa. Je, kukosekana kwake kunaweza kuwa chanzo kimojawapo cha umaskini wa watu?

Hapana. Kama ni kudhibiti uingiaji holela wa wageni unaodaiwa kuchangia ongezeko kubwa la uhalifu nchini, mbona maumivu hayo ni ya kujitakia?

Serikali ndiyo inafanya uratibu wa kuangalia ni mgeni gani kutoka wapi anastahili kukaribishwa nchini. Wengi wao wanaruhusiwa kuishi na kufanya kazi nchini kwa mgongo wa uwekezaji. Hawa hupokewa kwa shangwe na vigelegele.

Matokeo yake ni kama haya ya kuilipa kampuni yenye utata ya Dowans Sh. 94 bilioni kama fidia baada ya mkataba wa kuzalisha umeme wa dharura kuvunjwa na serikali.

Vitambulisho vya uraia vingezuia vipi uhalifu huo ambao kumbe tunaona namna unavyosaidia baadhi ya watu wakubwa kunufaika kutokana na udhaifu wa viongozi wakuu serikalini?

Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha, ameingia kwa mkwara kwenye wizara hiyo kwa kutaka vitambulisho vya taifa viwe tayari ndani ya miezi sita kuanzia 2 Desemba 2010. Hicho kwake ndiyo kipaumbele namba moja.

Kwa nini Sh. 250 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya mradi wa vitambulisho vya taifa zisielekezwe kwenye maeneo mengine muhimu kwa jamii kama vile ujenzi wa nyumba za askari polisi, umeme vijijini, vitanda vya wagonjwa hospitalini, nyumba za walimu na maji safi na salama?

Nani amesahau wabunge wa Tanzania walivyoshiriki, miaka kadhaa iliyopita, kuwatafutia hati za kusafiria wanawake wa Kisomali?

Nani hajui raia wa nchi jirani wanavyokaribishwa na kuhifadhiwa na viongozi wa maeneo ya mipakani tena baadhi yao walitumika kwa makusudi kusaidia ushindi wa chama fulani?

Mbona vitambulisho tayari tunavyo vya kupigia kura? Shahada za kupigia kura zimekuwa zikitumika kutambulisha raia na maeneo wanayotoka. Hivi vinavyoitwa vitambulisho vya taifa vitatambulisha nini cha zaidi?

Zaidi ya yote tuna vyeti vya kuzaliwa ambavyo tangu na baada ya uchaguzi mkuu vimeanza kutolewa kwa ‘promosheni’ achilia mbali vitambulisho vya benki na vya wafanyakazi. Mtanzania kwa sasa anaweza kuwa na vitambulisho hata vinne mkononi.

Hivi vyote havitoshi kumtofautisha Mtanzania na Mnyarwanda au Msomali?

<p> Mwandishi wa makala hii ni &nbsp;mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma &nbsp;(UDOM) anayesomea shahada ya uzamili kuhusu maendeleo. Anapatikana kwa simu: &nbsp;0787149846 na imeili: stephensamhenda@yahoo.com</p>
0
No votes yet