Vitambulisho vya taifa: Ni kweli au ‘magirini’


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 23 June 2012

Printer-friendly version
Gumzo la Wiki
Dickson Maimu

SAKATA la mradi wa vitambulisho vya taifa lingali bichi. Sasa limeibuliwa upya na Dickson Maimu, mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya vitambulisho vya taifa (NIDA).

Amenukuliwa akisema, mamlaka yake imesitisha uzinduzi wa mradi huo kwa sababu ya matatizo yaliyojitokeza.

Baadhi ya matatizo hayo, ni “hitaji la kutambua uingizaji anuani za makazi na kufanyika kwa usajili wa pamoja kati ya NIDA na  Tume ya Taifa ya  Uchaguzi (NEC).

Tatizo jingine, amesema ni kuweka picha kwenye kitambulisho cha uraia na kubainika kwa matumizi ya cheti kimoja kwa watu wengi.

Hivi karibuni NIDA iliripoti vyeti 248 kutumiwa na zaidi ya mtu mmoja katika Jeshi la Wananchi (JW); na vyeti vingine 700 kutumiwa na zaidi ya mtu mmoja katika jeshi la polisi.

Mradi wa vitambulisho vya taifa ulipangwa kuzinduliwa Mei mwaka huu. Walengwa wa kwanza, ni wafanyakazi wa serikali katika miji ya Dar es Salaam na Zanzibar.

Wengine ni maofisa wa vikosi vya ulinzi na usalama – polisi, magereza, uhamiaji na usalama wa taifa – kote nchini.

Kumekuwa na madai kutoka watu mbalimbali, kuwa mradi huu ulibuniwa mahususi na baadhi ya wanamtandao wa Rais Jakaya Kikwete, mara baada ya kiongozi wao kuingia madarakani.

Hiyo si hoja ya maana sana. Lakini kuna madai kuwa ulibuniwa “…kuneemesha baadhi ya watu.”

Kuna waliofananisha mradi huu wa vitambulisho na ule mradi wa kitapeli wa kufua umeme wa dharula ulioletwa na kampuni ya Richmond Development Company (LDC) na dada zake Dowans Holdings SA na Dowans Tanzania Limited (DHL).

Kama hivyo ndivyo, na kwa wingi wa mabilioni ya shilingi ya kuufanikisha, basi huu utakuwa ulaji wa miaka nendarudi.

Utakuwa basi mradi wa kula hata bila kushika jembe, kupanda, kupalilia na kuvuna. Unaweza hata kula bila kunawa. Ni sawa na mradi wa kufua umeme wa dharula wa Richmond Development Company (LDC).

Awali serikali ilisema mradi huu utagharimu Sh. 152 bilioni. Baadaye ikasema hadi unakamilika utachukua kiasi cha Sh. 250 bilioni.

Lakini sasa, kuna kila dalili kuwa utaweza kuchota, kutoka hazina ya taifa, zaidi ya Sh. 400 bilioni. Sababubu ni nyingi mno.

Leo hii ukisoma nyaraka mbalimbali za serikali na kumbukumbu za bunge – hansard – utabaini haraka jinsi viongozi wa serikali walivyobuni mradi huu gizani.

Utaona hata baadhi yao walivyotanguliza mbele maslahi binafsi. Kwa mfano, aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani, Lawrence Masha alituhumiwa mapema kuingilia mchakato wa zabuni.

Alidaiwa kukutana na wakuu wa kampuni ya Sagem Securite ya Uswisi, ambayo ilikuwa moja ya wazabuni.

Tuhuma zilikuwa kwamba Masha alikwenda kinyume cha sheria ya Mamlaka ya Usimamizi wa Ununuzi serikalini (PPRA) ya mwaka 2004 na kinyume cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya 1995 na Kanuni 101 (6).

Katika mchakato wa vitambulisho vya taifa wa mwaka 1998, Masha akiwa wakili kutoka kampuni ya IMMMA Advocates, aliwakilisha moja ya kampuni zlizoshiriki katika zabuni ya vitambulisho na kuingia katika mgogoro.

Mteja wa Masha aliishinda serikali. Lakini pamoja na madai hayo kuwekwa wazi, serikali ilimkingia kifua Masha.

Akijibu maswali ya papo kwa papo bungeni, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alitaka wabunge wavute subira ili mchakato huo ukamilike kwanza; ndipo anayetaka kuhoji afanye hivyo.

Pinda alikuwa akijibu swali la aliyekuwa mbunge wa CHADEMA jimboni Karatu, Dk. Willibrod Slaa.

Alisema, “…mheshimiwa Slaa umetuwahi, lakini jambo hili linafanyiwa kazi. Ingekuwa  vizuri ukasubiri mpaka mchakato huu umalizike ndipo ulete madai kama haya… ingesaidia sana. Lakini sasa, mchakato huu haujafika mwisho…”

Dk. Slaa alikuwa anataka kujua sababu za Masha kuingilia mchakato wa zabuni kinyume cha sheria ya PPRA na hatua ambazo serikali imemchukulia waziri wake.

Kusema watu wasubiri mradi ukamilike ndipo wakosoe, kulilenga kunyamazisha wananchi waliokuwa wanataka kuzuia mipango ya serikali na washirika wake kuchota fedha za umma.

Lakini leo mradi haujakamilika na tayari zimeonekana kasoro nyingi na ambazo ni vigumu kuziondoa mara moja.

Hadi sasa, hakuna anayefahamu kilichosababisha Pinda kumkingia kifua Masha. Inawezekana ni mwendelezo uleule wa utamaduni wa kulindana ambao umezoeleka kwa viongozi wa CCM, au ni sehemu ya uchafu huu.

Angalia mfano huu: Serikali imeingiza mabilioni ya shilingi katika mradi huu bila maandilizi. Kukosekana kwa maandalizi, ndiko kulikotoa mwanya kwa baadhi ya watendaji wa serikali na viongozi wake, kutafuta utajiri kwa mgongo wa vitambulisho vya taifa.

Baadhi ya makampuni yaliyopewa zabuni ya upembuzi yakinifu, hayakuwa na sifa ya kufanyakazi hiyo. Hayakuwa na uwezo kifedha, ujuzi wala utaalamu.

Waliojiita mameneja wa mradi, ndio sasa wamejipa kazi ya ushauri kwenye mradi. Baadhi yao ni watumishi wa serikali kutoka wizara za mambo ya nje na ofisi ya rais (Utumishi).

Huko walikotoka wamejilipa mabilioni ya shilingi kwa wanachoita, “Ushauri kwenye mradi.” Wanafahamika hata kwa majina na sasa, wamepewa ulaji mwingine kupitia NIDA.

Hivyo ndivyo makubaliano ya 13 na 18 Novemba 2004  yanavyoeleza. Nyaraka zinaonyesha katika kile kinachoitwa, “Utekelezaji wa mpango wa vitambulisho vya taifa - 2004 hadi 2014,” kundi la kampuni hizo zimepewa kazi ya ushauri katika menejimenti ya mradi.

Angalia mfano mwingine: Vitambulisho vya taifa vimebuniwa bila kufanyika kwanza uhakiki wa nani raia wa Jamhuri ya Muungano na yupi si raia. Serikali haiwezi kusema kazi hiyo inafanywa na NIDA.

Taasisi hii haina nyezo za kufanyakazi hii kubwa. Haina mamlaka.  Kazi ya utambuzi wa nani ni raia na yupi si raia, yaweza kufanywa kwa uthabiti na wakala wa usajili wa serikali wa vizazi na vifo (RITA).

Lakini RITA pamoja na kupigiwa chapuo na wananchi wenye dhamira njema na fedha za umma, haikupewa kazi hii na serikali. Sababu zinaweza kuelezwa vema na wahusika wenyewe.

Badala yake, katika kufanikisha “mradi wake,” NIDA imeweka sharti dogo tu – anayetaka kitambulisho cha taifa – awasilishe kwa ofisa wa chombo hicho, kivuli cha cheti cha kuzaliwa au kivuli cha hati ya kiapo kinachothibitisha uraia wa mwombaji. Basi! Hiyo inatosha kumfanya akabidhiwe kitambulisho.

Mara baada ya kuwasilisha nyaraka hizo, taarifa za mwombaji huingiziwa kwenye daftari la utambuzi. Wenyewe wameita, “daftari la kielektroniki.” Kazi imekwisha. Mwombaji anasubiri kukabidhiwa kitambulisho.

Siyo kazi ya NIDA kufanya utafiti wa uhalali wa nyaraka zilizowasilishwa kwake. Wala siyo kazi ya NIDA kufanya utambuzi wa nani raia na yupi siyo raia. Nani anaishi “kimagumashi” na yupi anaishi kihalali. Nani yupo nchini na anafanyakazi kwa mujibu wa sheria na yupi ameingia mtaani kutengeneza nyaraka feki na kujipatia kazi.

Aidha, siyo kazi ya NIDA kujua nani anatumia cheti cha marehemu na yupi anatumia cheti chake. Nani yuko hai; yuko wapi na anafanya nini; na nani amekufa na amezikwa lini na wapi.

Hizo siyo kazi zake. Kazi ya NIDA ni kugawa kitambulisho kwa yeyote, ili mradi amewasilisha nyaraka hizo kwake.

Kama NIDA haiwezi kufanya kazi ya utambuzi wa raia, nani atafanya kazi hiyo kabla ya kitambulisho kutolewa? Atafanya kwa gharama zipi? Nje ya bajeti ya Sh. 250 bilioni au kutahitajika mabilioni mengine kufanya kazi hiyo? Haya ni maswali yanayohitaji majibu.

Kipi kilichoifanya serikali kushindwa kufanya uhakiki wa raia wake kabla ya kuanza kutoa vitambulisho? Si vema kwanza ingewatambua na kuwafahamu?

Ingejua huyu amezaliwa wapi. Baba yake ni nani. Mama yake ni nani. Babu yake ni nani. Je, anastahili kupewa kitambulisho au hastahili?

Katika mazingira ya sasa, kitambulisho kinaweza kutolewa hata kwa asiyehusika. Wala sharti la kuwasilisha kivuli cha cheti cha kuzaliwa au hati ya kiapo, haiondoi uwezekano wa wasiokuwa raia kupata kitambulisho.

Hilo likitokea na kwa hakika litatokea, mradi huu utakuwa uthibitisho wa utapeli uliokuwa unapigiwa kelele tangu mwanzo.

Wale waliokuwa wanaupigia debe wataishia kufunika nyuso zao kwa aibu. Tuombe Mungu tusifike huko.

Kuna hili pia: Katika maeneo mengi ya nchi, hakuna anuani za posta. Nyumba nyingi hazina namba, wala hazitambuliwi na “mfumo wa kielektroniki” wa daftari la NIDA.

Hata katika miji mikubwa kama Dar es Salaam, Mwanza na Mbeya, hakuna hata mitaa iliyopimwa. Hakuna anuani za makazi. Kilichopo ni ujenzi holela.

Hivyo hivyo, katika maeneo mengi ya wilaya. Hicho kinachoitwa daftari la wakazi, hakuna anayejua hata jalada lake lilipo hivi sasa.

Je, huo utambuzi wa wanaostahili kupewa kitambulisho unaweza kufanyika vipi? Nani ataufanya? Kwa gharama zipi? Ni hizi zilizotengwa kwenye bajeti ya vitambulisho au nyingine?

Vilevile, serikali imesema mradi wa vitambulisho vya taifa uende sambamba na uandikishaji wapigakura katika daftari la NEC.

Lengo ni kupunguza gharama kwa serikali na usumbufu kwa wananchi. Kwamba hatua hiyo itasaidia kuondoa usumbufu pale mtu mmoja kuitwa na watu walewale kujiandikisha mara nyingi ndani ya kipindi kifupi.

Lakini serikali hiyohiyo haisemi lolote juu ya matatizo makubwa yaliyomo ndani ya daftari la wapigakura.

Kinachoitwa na NIDA “kukamilika kuwekwa kwa mfumo wa kuruhusu kuingizwa kwa kumbukumbu za NEC kwenye kitambulisho cha uraia,” siyo kinacholalamikiwa.

Malalamiko ya wananchi yanahusu udanganyifu ndani ya daftari la NEC. Yanahusu kunyimwa haki yao ya msingi ya kushiriki uchaguzi na kuthaminiwa kwa kura zao.

Ndani ya daftari kuna maelfu ya wananchi walioandikishwa mara mbili. Mamia wengine, majina yao hayaonekani ingawa walikwenda kujiandikisha. Wengine majina yanaonekana, lakini picha zilizopo, siyo zao.

Kuna taarifa za kuondoa majina ya wapigakura; kuongeza majina ya wengine na kuonekana, angalau kwa namba moja ya shahada isiyokuwa na jina mbele yake.

Hata idadi ya wapigakura nchini na wale wanaotajwa na NEC katika uchaguzi mkuu uliopita, inapingana na idadi ya watu waliomo ndani ya daftari lenyewe, idadi ya takwimu za idadi ya watu nchini na hata mazingira halisi ya nchi.

Angalia kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu iliopita. Awali NEC ilitangaza kuwapo wapigakura 20,137,303 kabla ya kuipunguza idadi hiyo hadi wapigakura 19.6 milioni.

Wakati idadi hiyo ikistukiwa na vyama vya siasa, NEC ilidai waliojitokeza siku ya uchaguzi walikuwa 8,626,283 (42.8%); wapigakura zaidi ya 11,511,020 (57.2) hawakujitokeza kupiga kura.

Lakini ukiacha hayo kuna hili pia: Hivi kulikuwa na umuhimu wa kutumia mabilioni yote haya ya shilingi, tena katika kipindi hiki kigumu cha anguko la uchumi wa taifa, kwa “kazi” hii inayoanza kuonekana kama kupeana ulaji?

Hivi hili lisingeweza kusubiri hata miaka 20 ijayo?

Au ni kweli taifa linahitaji vitambulisho vya uraia kuliko nishati ya umeme? Linahitaji vitambulisho kuliko kuboreshwa kwa huduma kwenye hospitali zake za umma? Linahitaji vitambulisho kuliko kuziboresha shule zake za msingi, sekondari na vyuo vya elimu ya juu?

Taifa linahitaji vitambulisho kuliko kulipa madaktari, walimu na kuwapa mikopo wanafunzi wa elimu ya juu? Mbona taifa hili limekuwapo bila vitambulisho vya taifa kwa miaka 50 sasa?

Taifa linahitaji vitambulisho kabla ya kuboresha kilimo? Kitambulisho cha taifa, kina faida gani kwenye taifa la wajinga na ambalo watu wake, wanakufa njaa? Tujadili.

0
No votes yet