Vitisho dhidi ya maisha ya Obama vyaongezeka


Zakaria Malangalila's picture

Na Zakaria Malangalila - Imechapwa 28 October 2009

Printer-friendly version
Rais Barack Obama

GAZETI la The Boston Globe la nchini  Marekani, limeripoti kuwapo kwa ongezeko la vitisho dhidi ya maisha ya Rais wa nchi hiyo, Barack Obama.
 
Likinukuu ripoti ya Bunge la Marekani – Congressional Research Service – kuhusu suala hilo, ripoti ambayo bado haijatolewa rasmi, gazeti limesema kwamba maisha ya Obama yapo hatani.

Vitisho hivyo vinatokana na kuongezeka kwa vitisho dhidi ya maisha yake, ongezeko ambalo halijapata kutokea kwa marais wa nchi hiyo katika vipindi vyao vya mwaka wa kwanza madarakani, katika muda wa karibu miongo mitatu sasa.
 
Sambamba na ongezeko hilo la vitisho, ripoti hiyo imesema kuwa kuna ongezeko la makundi ya chuki (hate groups) dhidi ya Obama; ongezeko la chuki dhidi ya utawala wake, hali ambayo imepelekea idara inayoshughulikia na ulinzi wake (US Secret Service) kuelemewa na kazi ya kumlinda.
 
Vitisho hivyo hutumwa kwa njia za barua pepe, mitandao ya tovuti (websites), blogu mbali mbali, ujumbe wa simu za mkononi, na hata kupitia barua za kawaida.
 
Hata hivyo, msemaji wa idara hiyo, Ed Donovan amesema kwamba kwa kawaida huwa hawatakiwi kuzungumzia masuala hayo kwa undani, na hasa katika kutaja tarakimu zozote kuhusu habari inayozungumzwa.

Lakini kutokana na umuhimu wa maisha ya rais, wameamua kuliweka jambo hilo wazi ili wananchi waweze kufahamu maisha ya rais wao.
 
Aidha Donovan amekanusha kuwapo kwa ongezeko kubwa kama inavyotajwa, ingawa amekiri kwamba vitisho dhidi ya maisha ya Obama vimekuwapo tangu wakati wa kampeni za uchaguzi za mwaka jana na pia baada ya kuapishwa.  
 
Kuongezeko kwa vitisho dhidi ya Obama kumeripotiwa pia na chanzo kimoja cha televisheni ya CNN ambacho kimemnukuu afisa mmoja wa US Secret Service kwamba vitisho vya kutaka kumuua Obama vimeongezeka kwa asilimia 400.

Anasema hali hiyo inazidi hali yoyote iliyokuwapo huko nyuma kuhusu vitisho kwa marais. Linatoa mifano kadhaa kuthibitisha vitisho kwa rais Obama vimekuwa vikubwa mno.
 
Likitoa mifano, gazeti la Boston Globe limesema siku mbili kabla ya Obama kuwasili katika hafla ya kuchangia pesa huko San Francisco , California, mtu mmoja alikamatwa na kushitakiwa kwa kosa la kutuma kwa njia ya barua pepe, ujumbe mkali uliojaa chuki za kibaguzi wa rangi, ambao pia ulimtishia kumuua Obama na familia yake.
 
Vilevile mtu mwingine aliweka kura ya maoni katika mtandao wa Facebook ukitaka kujua iwapo wapo watu ambao wako tayari kuona Obama anauawa.
 
Mtangazaji mmoja wa CNN aliyefanya mahojiano na mtu mmoja katika mtandao huo wa televisheni, alistushwa aliposikia mhojiwa wake akisema kwamba yuko tayari kuuangusha kwa nguvu utawala wa Obama.
 
Na katika mahubiri ndani ya kanisa lake lililoko Cleveland katika jimbo la Ohio, mchungaji mmoja wa kanisa la ‘ Faithful Word Baptist Church ” Steven Anderson, alisema asingesikitishwa kama angemuona Obama anayayeyuka katika maji ya chumvi kutokana na msimamo wake wa kuunga mkono utoaji wa mimba.
 
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Idara ya Mahakama (Justice Department) ilimtaja Steven Joseph Christopher, kuwa anashitakiwa kwa kuweka ujumbe katika mtandao wa tovuti akisema kuwa anapanga kumuua Obama mjini Washington, kwa kumtoa kafara.  
 
Steven Joseph Christopher ambaye anasadikiwa kuwa ni mfuasi wa kikundi cha kibaguzi cha wazungu weupe kiitwacho Ku Klax Klan (KKK) alisema, “Siyo kwamba simpendi sana Obama, kwani anaongea vizuri tu … lakini nafanya hivi kwa manufaa ya taifa langu na watu wetu.”
 
Aliongeza, “Na siyo kwamba mimi ni mbaguzi wa rangi, la hasha! Bali nitamuua Barack kwa sababu siko tayari kuona Wayahudi wakiendelea kuwaburuza Wamarekani ili wafuate matakwa yao.
 
Kwa ujumla, vitisho dhidi ya Obama viliaanza kumuandama tangu atangaze azma yake ya kugombea urais takriban miaka miwili iliyopita.
 
Idara ya usalama ina bajeti ya Dola 1.4 billioni kwa mwaka kwa ajili ya kumlinda Rais, Makamu wa Rais na familia zao na viongozi wa nchi za nje wanapokuwamo nchi humio kwa ziara rasmi za kiserikali, na pia mtu yoyote tule ambaye Rais ataamuuwa apatiwe ulinzi.

0
No votes yet