Vitisho ni aina ya ufisadi


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 01 July 2008

Printer-friendly version

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amesema bungeni kuwa hawezi kusema lolote juu ya kampuni ya Meremeta kwa kuwa shughuli zake zinahusiana na ulinzi na usalama; kwa hiyo ni 'siri.'

Naye Waziri, Phillip Marmo aliongezea mwishoni mwa mjadala kuhusu bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, kuwa mtu akikutwa na nyaraka za siri za serikali 'atashitakiwa kwa kosa la jinai.'

Naibu Spika, Anna Makinda, alishindilia msumari kwa kusema, 'Najua wabunge wanajua kuwa wana kinga humu ndani, lakini ukikamatwa nje na nyaraka hizo shauri yako.'

Sasa tujadili. Kwanza, tukubaliane kuwa kauli hizo ni kombora la vitisho lililoelekezwa kwa wabunge wanaotafuta au wanaopokea kile kinachoitwa 'nyaraka za siri za serikali.' Mlengwa mkuu ni mbunge wa Karatu (Chadema), Dk. Willibrod Slaa.

Raia mwema anayetawaliwa na serikali iliyo wazi, iliyojaa uadilifu, inayowajibika, inayolinda mali na uhai wa watu wake; inayotambua haki na uhuru wa wananchi – kuviheshimu na kuvilinda – atahitaji nyaraka za serikali kwa kazi gani?

Geuza swali hili. Raia mwema anayetawaliwa na serikali isiyo wazi, isiyo na uadilifu wa kutosha, isiyowajibika; isiyolinda mali za taifa; isiyoheshimu na kulinda uhuru wa wananchi kwa misingi ya usawa, atakosaje kutafuta kiini cha tabia hiyo ili kujua jinsi ya kupigania mabadiliko?

Tuchukue mfano wa kampuni ya kuchimba dhahabu, Meremeta. Kampuni hii imekuwa katikati ya shutuma nyingi za kuchota au kuchotewa mabilioni ya shilingi kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Katika hatua nyingine, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) amekiri kuwa kampuni hiyo haijawahi kukaguliwa na serikali, miaka saba tangu itajwe kuwepo.

Hata Msajili wa Hazina amepata kusema kuwa Meremeta haimo katika orodha ya mali za mashirika ya umma.

Leo Pinda anasema taarifa juu ya Meremeta ni za siri kwa kuwa zinahusu ulinzi na usalama; na kwa kuwa pia zinahusu jeshi. Hapa ndipo penye mgogoro.

Serikali inagoma kuzungumzia makampuni mengine; kwa mfano Tangold, Green Finance, Deep Green, Kiwira Coal Mines ambayo yamebebeshwa tuhuma.

Serikali inakataa kueleza uwezo wake wa kununua au kufukuza makampuni ya kufua umeme ambayo yamekamua taifa kidhalimu kupitia gharama zake za nishati hii.

Serikali imebakia kulalamika juu ya uharamia wa kiuchumi unaoendeshwa na wanaokamua maliasili na raslimali nyingine za nchi.

Ukimya, kauli zinazopingana na vitisho vya serikali, ni njia nyingine za kukwepa kuhojiwa na kukwepa kuwajibishwa.

Kwamba Pinda anadai kampuni ya Meremeta inahusika na jeshi, kama ndivyo au iliwahi kuwa, haina maana kwamba wananchi wanyimwe taarifa za kampuni hiyo.

Chukua mfano huu. Ninajua aina ya silaha zilizomo katika majeshi ya Uganda, Kenya, Burundi, Rwanda, Zimbabwe, Msumbiji, Tanzania, Zaire na nchi nyingine. Siri iko wapi? Vyanzo vya elimu hii vipo.

Wenzetu wanajua hata bei ya silaha hizo, kubwa na ndogo, kwenye soko halali la silaha na kwenye 'soko la mitaani.' Siri iko wapi? Vyanzo vya elimu hii vipo.

Wengine tunajua wachuuzi wakuu wa silaha za kivita na hata washirika wao katika serikali mbalimbali na maajenti wadogo wa silaha ndogondogo katika nchi za Maziwa Makuu na sehemu nyingine za Afrika na Ulaya. Vyanzo vya elimu hii vipo. Siri iko wapi?

Meremeta ina siri gani za kuangamiza nchi? Hata kama ina uhusiano na jeshi, nani kauliza siri ya kijeshi ya kuhatarisha ulinzi na usalama? Hata ununuzi wa silaha siyo siri.

Wanachotaka wabunge ni kujua nani mmiliki halisi wa Meremeta. Kwa nini hesabu za kampuni hii zisikaguliwe na serikali? Mapato yake ni kiasi gani? Yanatumika wapi? Kwa nini ichotewe fedha kutoka BoT? Mbona vijiji jirani na mgodi havinufaiki na maliasili yao? Siri iko wapi hapa?

Wabunge hawataki kujua ramani za wapiganaji. Lakini linapokuja suala la ununuzi wa silaha na zana nyingine, sharti wabunge wajue kwamba jeshi la nchi yao halitapeliwi.

Kuna uwezekano mkubwa wa kutumia kile kinachoitwa 'siri za jeshi' kukwepa kutoa maelezo au kukwepa wajibu.

Inapobidi sharti wawakilishi wa wananchi waambiwe MIPANGO ya jeshi; lakini siyo mbinu na mikakati ya kijeshi. Jaribu kuona tofauti kati ya mipango, kwa upande mmoja, na mbinu na mikakati ya jeshi, kwa upande mwingine.

Ndio maana nasema baadhi yetu tunajua silaha ndogo hadi kubwa za nchi nyingi; matumizi yake na gharama zake. Tusichojua ni mbinu na mikakati ya majeshi katika kuzitumia. Wabunge hawataki kujua mbinu wala mikakati.

Wabunge na hata askari wenyewe, wanataka kuwa na taarifa zitakazoepusha wizi, ufisadi na matumizi mabaya ya jina, silaha na vifaa vya jeshi letu. Uwezekano wa kufanya ufisadi nyuma ya pazia la jeshi, upo tena ni mkubwa.

Katika mazingira haya ya kuficha kila kitu; kiwe chema au kibaya; kunapokuwa na woga utokanao na kutenda au kutotenda au kutenda isivyo; basi taarifa, kwa njia ya nyaraka sahihi za wahusika, zitatafutwa kwa udi na uvumba.

Kuna maamuzi mengine yanafanya hata mtu mwenye uelewa mdogo ajenge mashaka; vipi viongozi wazalendo wanaweza kufanya maamuzi katili kwa watu na nchi yao?

Kwa kuwa wahusika hawasemi, basi sharti nyaraka zitafutwe ili kusaidia wananchi kujua kilichotendeka na nani alikitenda, ili wapate elimu ya kufanyia kazi katika mahusiano yao na watawala.

Kuna mambo matatu muhimu ya kuzingatia. Kwanza, taarifa nyingi zinazoitwa za siri ni za 'ukombozi.' Wanaozitoa hawalipwi bali wanaona fahari katika kupigania haki na uhuru wa wengi.

Pili, vitisho hukomaza na huzaa mbegu isiyoshindika. Labda tufanye zoezi: Kati ya aliyeficha siri za kuangamiza nchi na aliyezifichua kwa kutumia nyaraka sahihi; nani asulubiwe?

Tatu, kama serikali ina siri, sharti ihakikishe inatunza siri zake. Hili ni muhimu hata mbele ya mahakama. Si wajibu wa wabunge au vyombo vya habari kutunza siri za serikali.

Kinachohitajika: Serikali ijibu hoja. Ikibanwa ijitetee. Ikishindwa ikubali. Isahihishe. Iombe radhi. Isonge mbele. Huo ndio ustaarabu katika utawala bora. Vitisho iwe mwiko.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: