Viwanda vikubwa vitaondoa umasikini


Joseph Mihangwa's picture

Na Joseph Mihangwa - Imechapwa 07 October 2008

Printer-friendly version

SEHEMU kubwa ya matatizo ya uchumi yanayokabili serikali ya Rais Jakaya Kikwete, yana mizizi katika utendaji wa kazi wa awamu mbili zilizotangulia.

Hapa udhaifu mkubwa uko katika kupanga uchumi kwa maendeleo ya nchi. Na huu ndio mtihani ngumu unaomkabili rais na serikali yake. 

Kuna sura tatu za kuzingatia katika uchumi wa Tanzania na ule wa nchi zote za Dunia ya Tatu.   Kwanza, ni dhaifu wa uchumi.  Pili, kwa sehemu kubwa ni tegemezi kwa fedha kutoka nje. Tatu, kadri utegemezi kiuchumi unavyoendelea, ndivyo uhai kisiasa na kiuchumi utakavyoendelea kuwa tegemezi.

Msingi wa kwanza katika kuondokana na janga hili ni kuasisi kwa makusudi, uhusiano kati ya sekta mbili kuu za uzalishaji – viwanda na kilimo. 

Sekta hizi zinaweza kuendelea tu kwa uhakika kama shughuli zake zitashabihiana na kutegemeana; na si kwa kila moja kuchukua mkondo wake, kama vile kujiingizia fedha za kigeni. 

Uuzaji bidhaa nje kwa ajili ya kupata fedha za kigeni ni jambo muhimu, lakini sharti kuwepo msingi mkuu wa kusimamia hili; kwamba uuzaji nje ufanyike pale tu mahitaji ya ndani yanapokuwa yametekelezwa.

Msingi wa pili ni kuweka uwiano wa ndani kwa kila sekta hizi mbili. Ndani ya sekta ya kilimo kuwe na uwiano kati ya uzalishaji wa chakula na uzalishaji wa (mazao) malighafi za viwanda; kati ya uzalishaji mkubwa na uzalishaji mdogo; kati ya mfumo wa sasa wa uzalishaji na ule wa kale; na kati ya  uzalishaji binafsi na uzalishaji wa umma.

Muhimu zaidi hapa ni kuwa na “kiunganishi” kikuu katika kusukuma mbele maendeleo ya vingine. Hapa kiunganishi kikuu ni uzalishaji wa chakula.  Watu,  ambao ndio rasilimali muhimu, na nguvu ya msingi kwa maendeleo, lazima wale na wale chakula bora kabla ya kupata nguvu ya kufanya mambo mengine.

Msingi wa tatu ni kuwa na uwiano ndani ya viwanda.  Idara muhimu katika sekta hii ni viwanda vikuu (heavy industries)  na viwanda vyepesi au vya kati (light industries). 

Viwanda vikuu vina jukumu la kuvipatia viwanda vya kati mashine za uzalishaji mali. Kwa ufupi, kazi ya viwanda vikubwa ni “kuzalisha mashine za kuzalisha mashine.” Ni viwanda hivi vikuu ambavyo hutengeneza vipuri na kuondoa tatizo la viwanda vya kati kutegemea vipuri kutoka nje.

Viwanda vya kati ni vipi?  Ni sekta ya viwanda inayozalisha bidhaa za walaji kama vile nguo, viatu, pamba nyuzi (ginneries), bia (breweries), zana za kilimo, vifaa vya kupasua mbao, mitambo ya maji na vingine vya aina hiyo. 

Lakini viwanda vya kati pia ni sekta inayogharamia viwanda vikuu; kule ambako inapata mashine na inatoa bidhaa za mlaji kwa watumishi wa sekta zote mbili.  

Siyo tu kwamba ujenzi wa viwanda vikubwa nchini ni muhimu katika kujenga msingi wa mapinduzi ya kiteknolojia na uvumbuzi, bali pia unasaidia kuimarisha uwezo wa nchi katika kudhibiti vizuri mazingira.

Ni viwanda vikubwa, katika mchakato wa maendeleo, vinavyojenga mabwawa, kudhibiti mafuriko na kuhifadhi maji kwa ajili ya umwagiliaji. Aidha, vinarahisisha kupeleka umeme vijijini, hatua ambayo ni muhimu na ya awali katika uwiano bora wa maendeleo ya viwanda, na upunguzaji tofauti ya maisha kati ya vijijini na mijini.

Viwanda vikubwa ni muhimu pia katika kuendeleza mfumo imara wa uchukuzi na mawasiliano. Na kwa sababu ya umuhimu wake katika uchumi, hakuna nchi iliyowahi kuendelea bila ya viwanda vikubwa. 

Ni kutokana na nguvu ya eneo hili, nchi zenye viwanda zimeweza kuzitawala na kuzidhibiti nchi masikini ikiwemo Tanzania.

Serikali ya awamu ya kwanza (Nyerere, 1961 – 1985), ilijenga viwanda vingi vya kati ili kuondoa utegemezi kwa mataifa ya nje. Ilijenga viwanda vya nguo, mbolea, zana za kilimo na vya bidhaa karibu zote za mlaji.

Awamu hii ilijenga pia viwanda vya kutengeneza mashine (Moshi – Machine Tools), viwanda vya kutengeneza magari (Nyumbu), kiasi cha kukaribia kujitosheleza kwa mahitaji ya ndani. 

Leo, viwanda hivyo vyote havipo tena; vilitelekezwa, vikauzwa katika mkumbo wa ubinafsishaji; vikauawa na mabepari wa kimataifa ili kujenga na kuendeleza utegemezi wa Tanzania kwa bidhaa kutoka nje.

Sababu nyingine ni ulimbukeni wa walioko madarakani na ushabiki unaoenezwa nao kwa bidhaa kutoka nje; jambo ambalo linaonyesha kujikana.

Mgogoro hapa siyo juu ya kuporomoka kwa bei za bidhaa za nchi masikini katika soko la dunia; siyo “ubahiri” wa nchi zenye viwanda vikubwa au ubaya wa mfumo wa kimataifa.  Hayo ni matokeo tu na sio chanzo cha kutoendelea. Tatizo ni kushindwa kujenga viwanda vikubwa.

Badala ya kuelekeza rasilimali katika ujenzi wa sekta hiyo muhimu, nchi imejiingiza katika ujenzi wa maghorofa yaendayo mawinguni na majumba ya anasa yasiyozalisha utajiri. 

Kama nchi ingekuwa na watawala wabunifu wa maendeleo ya kweli, majengo ya minara pacha ya Benki Kuu yangejenga viwanda vingapi kwa maendeleo ya uchumi?

Mwalimu Julius K. Nyerere, katika kitabu chake “Binadamu na Maendeleo” anasema, “Maendeleo yasiyokuwa maendeleo ya watu yanaweza yakawapendeza wataalam wa historia wa mwaka 3000; lakini kwetu sisi hayana maana kwani hayahusiani na maisha ya kesho tunayojenga…”

Mwalimu anajenga hoja kwamba ingawa utamaduni wa Misri wa wakati huo ulikuwa na busara na elimu nyingi, haukukawia kuteketezwa na wageni, maana ulikuwa utamaduni wa wachache; wananchi waliobaki walikuwa watumwa walioteseka tu kwa shughuli za kuleta maendeleo ya majengo, ambayo wao wenyewe hawakuyatumia.

Matumizi haya mabaya ya rasilimali yanafanya nchi kama Tanzania ziyapigie magoti mataifa makubwa kuomba mikopo zaidi, na wakati huohuo uchumi hauzalishi vya kutosha kuwezesha ulipaji madeni na riba ya mikopo hiyo.

Misaada ya mabilioni ya shilingi inayomwagwa na kina Rais George W. Bush wa Marekani na kufanya watawala kurukaruka kwa furaha kama ndama, ingekuwa ya manufaa zaidi kama ingetolewa kwa mfumo wa viwanda, kuwezesha taifa kujitegemea.

Ilivyo sasa, ni misaada inayoongeza na kuimarisha utamaduni wa utegemezi. Wanaotoa mikopo na misada hawataki Tanzania iwe na ndoana wala ijue jinsi ya kuvua samaki.

Wanataka kila siku Tanzania na nchi za Dunia ya Tatu zipige magoti langoni mwa tajiri na kuomba samaki. Huu ni utumwa. Je, Mkulo na serikali yake wanakubali kumeza dawa chungu ya kuponya gonjwa hilo?

0
No votes yet