Vurugu Mara husabishwa na nini?


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 01 June 2011

Printer-friendly version
Gumzo la Wiki

MAPIGANO, vurugu na mauaji ya raia mkoani Mara husababishwa na nini? Hili ndilo swali linaloumiza vichwa vya wananchi wengi wenye kutaka amani ya kweli.

Kumbukumbu zinaonyesha mapigano mkoani Mara yametokea mara kwa mara chanzo kikiwa ugomvi wa mipaka ya maeneo ya makazi ya koo mbalimbali ziishizo mkoani humo na wakati mwingine chanzo kikiwa wizi na unyang’anyi wa mfugo hasa ng’ombe.

Aidha, historia inaonyesha kumekuwapo vurugu kubwa na mapigano mkoani Mara kila baada ya miaka kumi. Vilevile, vita za koo zimekuwa kati ya koo ndogo na koo kubwa tofauti na safari hii ambapo vurugu imewahusu polisi wanaoua raia kwa kisingizio cha kuvamiwa mgodi.

Vurugu za kwanza kubwa mkoani Mara zilianza miaka ya 1972 na 1974. hicho kilikuwa kipindi cha operesheni vijiji. Watu walikuwa wanahamishwa na kurundikwa katika vijiji vya ujamaa.

Mzozo huu ulianzia wilayani Serengeti ambapo watu wa kabila la Waikoma, Wangoreme, Wanata na Waisenye waliungana kuwapiga Watimbaru, Wanyabasi wa Tarime na Kenya na Wakira wa Tarime na Kenya ambao walihamia huko ili waondoke wilayani humo.

Vurugu hizo zilisababisha makundi ya wezi wa mifugo ya Wairegi, Wanyamongo, Wanyabasi na Watimbaru kutoka Tarime kuvuka mto Mara na kuingia wilayani Serengeti kuhakikisha ndugu zao hawaonewi wala kuhamishwa.

Serikali nayo iliingilia kati. Ikakifunga chuo cha polisi Moshi na kupeleka makuruta wote Mara pamoja na askari wengine wa FFU kutoka karibu mikoa yote Tanzania. Chanzo cha vurugu za 1972 hadi 1974 kilikuwa wizi wa mifugo uliosababishwa na wahamiaji kutoka Kenya walioungwa mkono na wezi wa mifugo wa Tarime na Serengeti.

Miaka kumi baadaye vurugu tena zikafumuka. Hii ilikuwa kati ya mwaka 1982 na 1985. Vurugu hizi zilikuja kujulikana kama vita ya “Nyamaganya” mtu aliyekuwa bingwa wa kutengeneza bunduki na risasi.

Kama ilivyokuwa mwaka 1972 vurugu hizi zilianzia wilayani Serengeti. Kipindi hiki kulikuwa na bunduki nyingi sana mkoani Mara. Vita na vurugu hizi zilipotulia wanaume wengi kutoka Mara walihamishiwa Kusini hasa Mtwara, Lindi na Ruvuma na haieleweki watu hao waliishia wapi.

Tofauti na inavyosemwa na watu wengi kuwa bunduki hizo zilipatikana kwenye vita ya Kagera – 1978 hadi 1980 – ukweli ni kwamba bunduki zile zilitoka nchini Ethiopia ambako Wasomali wa Ogaden walikuwa wakipigana kutaka kujitenga.

Wasomali wa mkoa wa Kaskazini Mashariki mwa Kenya wenye makao makuu Wajir walipata bunduki kutoka Jijiga nchini Ethiopia wakashirikiana na Wakurya wa Kenya mpakani na Tanzania na kuzibadilisha kwa ng’ombe zilizokuwa zikiibwa mkoani Mara hasa Serengeti na Tarime.

Mwanzoni bunduki moja ilibadilishwa kwa ng’ombe watano. Baadaye vita ilipochacha kabisa mwaka 1983 bunduki moja ilifikia kubadilishwa kwa ng’ombe 30, wenyewe Wakurya wanaita idadi hiyo “ekihingo” yaani idadi ya ng’ombe wanaotosha kuoa mke mmoja.

Polisi wa Tanzania walisombwa kutoka mikoa yote lakini kwa sababu siku zote polisi hufurahia matatizo yaendelee kwa sababu wanabaki eneo la vurugu wakilipwa posho. Vurugu hazikwisha mapema mpaka pale lilipoingia jeshi na kufanyia mazoezi kule wilayani Serengeti kuwaonyesha Wakurya nguvu yao.

Muulize mtu yeyote jeshini leo hii atakuambia kitu kinachoitwa “operesheni ngombe.” Wanajeshi wengi walihamishwa vikosi vyao, wa mashariki wakenda Kusini wa Kusini wakajikuta Magharibi huku wa Mashariki hasa Brigedi ya Nyuki ikajikuta Kanda ya Ziwa.

Wakati huu ndipo alipopelekwa mkoani mMara wilayani Serengeti mtu anayitwa KUBEHA ambaye alifanya mambo yasiyotamkika. Machache yanayotamkika ni kuwalazimisha watoto (wamura) kucheza ngoma ya iritungu uchi na dada na mama zao! Hadi leo sikuwahi kuwasikia watetezi wa haki za binadamu walkilisemea hili.

Baadaye Mara ikatulia kwa miaka mingine kumi hadi miaka ya 1994 – 1995 enzi ya Mkuu wa Mkoa Joseph Butiku kulipozuka mzozo wa kugombea ardhi baada ya kufa siasa ya ujamaa na watu kurejea mahameni kwao walipotoka enzi ya operesheni vijiji.

Huu ndio wakati Wanyamongo walipojikuta wakipambana na ndugu zao wa damu Wairegi upande wa Kaskazini na Wanyabasi na Watimabaru upande wa Kusini. Kwa upande wao Wanchari wakawa na kibarua kigumu kupambana na Walenchoka upande wa Kaskazini na Wakira upande wa Mashariki.

Ikimbukwe kwamba Wanchari na Wanyamongo ni koo ndogo sana lakini zinazojihami kupindukia ili kulinda maeneo yao. Pia ieleweke kwamba mipaka ya gunguri (kata) na kata iliwekwa na mkoloni mmoja DC Ingram ambaye aliwapa kila koo eneo lao.

Kwa sababu hiyo Tarafa ya Inchugu (Tembo) wanakaa Wanchari na Wakira, Inchage (Pundamilia) wanakaa Watimbaru na Wanyabasi, Ingwe (Chui) wanakaa Wairegi na Warachangwe maarufu kama Wanyamongo siku hizi) huku Inano wakikaa Wasweta, Wahunyaga na Wamera kila koo kata yake.

Vurugu za 1994- 1995 zilisababishwa na serikali hasa polisi kwa kushindwa kutenda haki. Wakati huo kulizuka wimbi la Wakurya wa Kenya waliokuwa wamehamishwa kutoka mbuga ya Masai Mara wakihamia Tanzania maeneo ya wazi yaliyohamwa 1973 – 1974 enzi ya operesheni vijiji.

Wakira na Walenchoka kutoka Kenya na Serengeti walihamia Bunchari na kuzua mzozo na Wanchari walioona mipaka yao inaingiliwa. Kwa upande mwingine Wairegi kutoka Kenya walihamia Nyamongo na kukalia eneo lililokuwa likiitwa gunguri Nyabikondo na kuanzisha vijiji vya Genkuru na Gibaso.

Wahamiaji hawa waliungwa mkono na koo zao za Walenchokla, Wakira kwa upande wa tarafa ya inchugu na Wairegi waliwaunga mkono Wairegi wenzao kutoka Kenya. Waungaji mkono walichanga ng’ombe nyingi sana zikapelekwa Tarime na Musoma walipo watawala kuzima kelele za Wanchari na Wanyamongo.

Kampeni ya ukusanyaji mifugo kuchangia au kuwahonga wakuu wa wilaya, wakuu wa polisi wilaya, mkuu wa mkoa, mkuu wa polisi mkoa na hata wasaidizi wao zilitanguliwa na kauli ya “talusya ebinto twitanele ekyalo” ikimaanisha toeni mali tupiganie nchi isichukuliwe na wapinzani wetu.

Na kweli kelele zilizimwa kwa hongo ya ng’ombe, wenyewe Wanyamongo na Wanchari wakachukua silaha kuhami maeneo yao maana polisi na serikali kwa ujumla haitendi haki na kuzua vurugu kubwa ikihusisha kama kawaida ya vurugu za namna ile unyang’anyi, wizi wa ng’ombe na uchomaji moto nyumba.

Hoja kwamba serikali ndiyo chanzo cha vurugu mkoani Mara na hasa Tarime ni kufumbia macho mambo ya kweli yanayowakera raia. Mfano rahisi ni vita baina ya Wanchari na Wakira.

Vita hii imekuwa ikisababishwa na Wakira waliotoka Kenya na wilayani Serengeti walikofukuzwa kutokana na vita za awali baina yao na Wanyabasi wa Serengeti.

Wahamiaji hawa wanakalia maeneo yaliyo wazi ya vijiji na kata za Wanchari lakini hawataki kushirikiana nao wala kushiriki maendeleo kwa sababu eti wao ni Wakira na hivyo wanataka waanzishe vitongoji vya Wakira na watawaliwe na wongozwe na viongozi kutoka vijiji jirani vya Wakira.

Hii ndiyo sababu Wasukuma, Wajita, Waluo na makabila mengine wakihamia Ukuryani hawabughudhiwi kwa sababu wao hawana haja na hawataki kuanzisha himaya za makabila yao ndani ya koo za Wakurya.

Utashangaa eneo la Bunchari Wakira na Walenchoka wanasakwa lakini Waluo, Wajita, na Wasukuma ambao ni wengi tu mkoani Mara hawaguswi.

Na hao wanaosakwa kwa kukataa kutii matakwa ya Wanchari wanakimbilia Tarime na Musoma wanahonga ngombe na majibu yanayorudi ni kwamba Tanzania ni moja mtanzania yuko huru kuishi popote! Hoja kwamba wanakataa kutawaliwa na Wanchari bali wanatka kutawaliwa kuytoka bukira huku wakiishi Bunchari haizungumzwi tena.

Upande wa Nyamongo hali ni hiyo hiyo. Tofauti ni kwamba baada ya vita ya muda mrefu serikali ilihalalisha makazi ya wahamiaji haramu kuwa vijiji vya Genkuru na Gibaso na baadaye kuvipa kata ya Gorong’a. lakini pia ugomvi wa Wanyamongo na Wairegi huwa haudumu. Wanapigana asubuhi jioni wanaoana. Ni ndugu wa damu kama walivyo Wanyabasi na Watimbaru.

Ushahidi wa serikali kuchangia ugomvi wa koo unaonekana vizuri kama mtu akiangalia mipaka ya tarafa za Ingwe na Inchage ambapo kimeanzishwa kitongoji cha Mwala ndani ya eneo la kijiji cha Matongo tarafani Ingwe lakini kwa sababu wao ni Wanyabasi imelazimishwa kuwa kitongoji kile ni cha kijiji cha Nyarwana cha Wanyabasi wa tarafani Inchage.

Hakuna malalamiko ya Wanyamongo yaliyosikika polisi wala kwa Mkuu wa Wilaya baada ya hongo ya ng’ombe na pesa kwa wakuu wilayani na mkoani.Wanyamongo wanachotaka si kwamba watu wa Mwala wahame bali watu hao watii amri za mwenyekiti wa kijiji cha Matongo eneo wanakokaa na si Nyarwana kwa Wanyabasi wenzao.

Hebu fikiria mtu anakaa kwenye kijiji na kata yenu lakini hawajibiki kwenu na wizi ukitokea yeye hamwezi kumwita kwa sababu tu ni Mnyabasi na kwamba yeye anatii amri za viongozi wa katani kwao wanakoishi Wanyabasi wenzake?

Hata Wanchari hawataki kuwafukuza Wakira bali wanawataka wahame kule walikojitenga kwenye eneo la Wanchari na waje wajumuike nao waishi pamoja na kule waliko kuwe eneo la kuchungia mifungo na kilimo. Wahamiaji Wakira hilo hawalitaki bali wanadai Tanzania ni moja!

Mwaka 2004 na 2005 ikiwa baada ya miaka mingine kumi vurugu tena zilizuka mkoani Mara safari hii zikihusisha Wanyabasi na Wairegi. Hii ilikuwa mara ya kwanza katika historia kwa koo kubwa za Wakurya kupigana. Wanyabasi ni wengi wanapatikana Kenya na Tanzania na Wairegi ni wengi nao wanapatikana Kenya na Tanzania.

Zamani ilikuwa vita baina ya koo ndogo za Wanyamongo, Wanchari na Wahunyaga wakipigania ardhi na koo kubwa za Wakira, Walenchoka, Wairegi na Wasweta. Siku zote katika migogoro ya kikoo wilayani Tarime serikali imekuwa ikunga mkono koo kubwa kupitia kwa wasomi wao waliopo Dar es Salaam.

Katika vita hiyo Wairegi wa Tanzania walivamia Wanyabasi wa Tanzania na kuiba ng’ombe na kwenda kuzificha kwa Wairegi wenzao waliopo Kenya na hali kadhalika Wanyabasi walipojibu mapigo walikwiba ng’ombe kwa Wairegi Tanzania na kwenda kuzificha kwa Wanyabasi wa Kenya.

Hata hivyo miamba hii miwili sasa imekubali suluhu na amani imerejea. Tangu kuanzishwa uchimbaji dhahabu Nyamongo kuanzia miaka ya 1997 – 1998 Wakurya walianza kuwa wamoja lakini wanapigwa na polisi.

Uhasama sasa umekuwa baina ya raia na Polisi walioajiriwa na serikali lakini wanalipwa na mgodi Tshs 80,000 kwa siku wanapokuwa zamu. Mbele ya macho ya raia polisi wa Tarime wameajiriwa na mgodi na wanalipwa na mgodi kuwaua wao.

Ugomvi wa koo umeanza kufifia. Hawaendekezi tena ukoo kupigana na ukoo mwingine unaosaidiwa na polisi. Sasa wamebaki kuhesabu maiti za vijana wanaopigwa risasi na polisi kwa kisa cha eti kuvamia mgodi na kupambana na polisi wanaolinda mgodi. Ajabu ni kwamba wapambanaji hao wanapigwa risasi za mgongoni wakikimbia!

Ni muhimu kusisitiza tena kuwa tofauti na ilivyokuwa huko nyuma, hivi sasa Wakurya hawapigani wao kwa wao. Wanapigwa risasi na kuuawa na polisi.

0
No votes yet