Waagizaji mafuta wakwaa kisiki


Aristariko Konga's picture

Na Aristariko Konga - Imechapwa 30 June 2009

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli

WAAGIZAJI mafuta kutoka nje ya nchi sasa wanakabiliwa na kigingi. Wanapaswa kuagiza mafuta kwa pamoja ili kudhibiti bei za kuruka za nishati hiyo nchini.

Huu ni uamuzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) ambayo sasa inaanzisha utaratibu mpya wa uagizaji mafuta. Makampuni yote yanayofanya kazi hiyo sharti yaingize nishati hiyo kwa pamoja.

“Serikali kupitia EWURA inaandaa utaratibu wa uagizaji wa mafuta kwa wingi na kwa pamoja, kwa kutumia mfumo wa zabuni, ambapo waagizaji watashindana ili kupata bei nafuu kadri inavyowezekana. Sambamba na kupunguza gharama za uagizaji katika ununuzi, gharama za usafiri pia zitapungua,” anasema Mkururgenzi Mkuu wa EWURA, Haruna Masebu.

Ili kupata bei nzuri za mafuta hapa nchini, serikali kwa kushirikiana na EWURA imeandaa utaratibu wa kampuni zote kununua mafuta kwa wingi na kwa pamoja, kwa kuwa ni njia bora ya kuingiza nishati hiyo hapa nchini.

Ili kufanikisha jambo hilo, 26 Januari mwaka huu, EWURA ilikamilisha mchakato wa kumpata mtaalam mshauri, ambayo ni Kampuni ya Petroleum Development Consultants Limited (PDCL) ya Uingereza.

“Mtaalam anaendelea na kazi ya kuandaa namna bora ya kutekeleza utaratibu wa kuagiza mafuta kwa pamoja, ikiwa ni pamoja na taratibu zinazohusika, ikiwamo kuandaa rasmu za mikataba kati ya wadau mbalimbali na kanuni za uendeshaji wa mfumo huo,” anasema Masebu.

Mnamo 24 Aprili mwaka huu, PDCL iliwasilisha EWURA rasimu ya awali ya ripoti ya utekelezaji wa mpango huo, na EWURA iliandaa mkutano wa kupata maoni ya wadau, uliofanyika 12 Mei, mwaka huu.

Aidha, kampuni hiyo iliwasilisha rasimu ya mwisho, ambayo imesambazwa kwa wadau mbalimbali. Mkutano wa pili wa wadau ulitarajiwa kufanyika wiki iliyopita kujadili rasimu, ambapo maoni na mapendekezo yangekusanywa na kuzingatiwa na mshauri huyo, kabla ya kukamilisha ripoti hiyo wakati wowote kuanzia sasa.

Mfumo wa uingizaji nchini bidhaa za mafuta kwa pamoja, unalenga kupunguza hitilafu zilizobainika kwenye utafiti uliofanyika Agosti 2007, ambao ulishirikisha wadau mbalimbali.

“Utaratibu wa sasa, wa kila kampuni kuagiza mafuta yake kutoka nje, unasababisha gharama kubwa za usafiri, msongamano wa meli bandarini, na kusababisha ada za ucheleweshaji wa meli pamoja na kuhamishia gharama za makampuni mama kwa watumiaji wa nishati hiyo hapa nchini,” anasema Masebu.

Sekta ya mafuta hapa nchini inaweza kuelezewa kwa kuzingatia vigezo vitano: uingizaji, upakuaji, utunzaji, usafirishaji na uuzaji rejareja.

Kuhusu uingizaji mafuta hapa nchini, Tanzania ndiyo inayoingiza bidhaa zote za mafuta, kiasi cha tani 1.7 milioni kwa mwaka, kwa ajili ya soko la hapa nchini.

Bandari za Tanga na Mwanza pia hutumika kuingiza bidhaa hizo wakati mafuta mengine huingizwa kwa njia za malori kutoka Kenya, kwa kupitia mipaka ya Sirari, Namanga na Horohoro.

Tangu ukiritimba wa uagizaji mafuta uondolewe Januari 2000, kila kampuni imekuwa ikiagiza mafuta kwa kuangalia mahitaji yake. Kutokana na hali hiyo, bei za mafuta zimekuwa zikipangwa kutokana na nguvu ya soko.

Inakadiriwa kuwa matumizi ya mafuta hapa nchini kwa mwaka 2007 pekee yalifikia tani 1.7 milioni.

Hata hivyo, makampuni ya mafuta yaliripoti kuwa kiasi cha mafuta kilichoingizwa kilikuwa ni meta za ujazo 1.3 milioni kwa mwaka 2007.

Kwa hiyo ni wazi kwamba kiasi chote cha mafuta yanayoingizwa nchini hakielezwi. Zaidi ya mafuta yanayotumiwa hapa nchini, mengine husafirishwa kwenda nchi za jirani ambazo hazina bandari. Hivi sasa kuna makampuni 25 yanayoingiza mafuta nchini kwa ajili ya soko la nchini au kwenda nchi za jirani.

EWURA imebaini matatizo kadhaa yanayojitokeza katika mlolongo wa kusafirisha mafuta. Mojawapo ni mparaganyiko unaojitokeza katika uingizaji mafuta unaosababishwa na kila mmoja kujiagizia mafuta yake, utaratibu ambao ni chanzo cha bei kubwa.

Tatizo lingine ni msongamano wa mizigo huko Kurasini, Dar es Salaam, na kusababisha gharama kubwa.

Mparaganyiko wa kiasi cha mafuta kinachoingizwa kupitia milango mingi ya Dar es Salaam, Tanga, Sirari, Ziwa Vikctoria na Mtwara ni tatizo lingine. Uingizaji nishati hiyo kwenye vituo hivyo vingi hufanya kazi ya usimamizi kuwa ngumu katika kubaini ubora na wingi wa mafuta yaliyoingizwa.

Tatizo lingine ni ubovu wa mara kwa mara wa mita zinazotumika kupata matokeo ya sampuli za mafuta, na kisha kuziruhusu meli kupakua mizigo.

Lakini pia mambo mengine yanayohusu nguvu ndogo ya pampu zinazotumika kutoa mafuta kutoka kwenye matanki yanachangia kwenye orodha hiyo ya matatizo.

Kuhusu hifadhi ya mafuta, EWURA wanasema kuwa mafuta yaliyosafishwa yanafikia tani 550,000. Tani 91,820 zinamilikiwa na kampuni ya TIPER ya Dar es Salaam na zinazosalia humilikiwa na makampuni 20 yanayojihusisha na nishati hiyo.

Tani 320,000 za mafuta huhifadhiwa Dar es Salaam na humilikiwa na makampuni 10. Hifadhi nyingine mbili zenye uwezo wa kutunza tani 72,000 za nishati hiyo bado zinajengwa.

Kuna malalamiko miongoni mwa wanunuzi wadogo kuwa watunzaji wakubwa wa mafuta huwatoza bei kubwa wakati huuziana kwa bei nafuu wao kwa wao.

Utaratibu huu mpya wa uagizaji mafuta unalalamikiwa na makampuni yanayoingiza mafuta nchini. Hii ni kutokana na udhibiti wa ubora, bei na hata usafirishaji nchini na nje ya nchi.

Januari hadi Juni mwaka huu, bei za mafuta ya aina zote nchini zimekuwa zikipanda ingawa si kwa kasi kubwa kama ilivyokuwa mwaka 2007. Kupanda huko kumeelezwa kunatokana na sababu mbili kuu:

Kwanza, ongezeko la bei za kununulia mafuta kwenye soko la dunia. Petroli imepanda kwa asilimia 46.31, dizeli asilimia 11.98 na mafuta ya taa asilimia 6.42.

Pili, ni mfumuko wa bei kupanda na kufikia asilimia 13.3 hapa nchini na kushuka kwa thamani ya sarafu dhidi ya dola ya Marekani.

EWURA imekuwa ikifuatulia mwenendo wa bei za mafuta kuanzia soko la dunia hadi kwenye vituo vya mafuta hapa nchini. Ili kukabiliana na upandaji bei holela, mamlaka hiyo imekuwa ikitoa bei elekezi.

0
No votes yet