Waandishi hawa wanahitaji msaada


Meddy Mulisa's picture

Na Meddy Mulisa - Imechapwa 20 April 2011

Printer-friendly version
Raymond Owamani, enzi za nguvu zake

WAANDISHI wawili wa habari, Raymond Owamani na Benjamin Rwegasira, ni wagonjwa. Wanahitaji msaada wa haraka.

Msaada wa kwanza ni kutafuta kujua kinachowasumbua. Msaada wa pili ni kuwatafutia tiba. Ikibidi kuwapeleka hospitalini.

Wiki chache kabla ya uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka jana, waandishi hao wa mkoani Kagera, walikumbwa na ugonjwa ambao haujathibitika.

Raymond Owamani ni mfanyakazi wa Radio Free Afrika na Star TV.  Anaishi Kashabo, Kata ya Hamugembe, katika Manispaa ya Bukoba

Owamani alianguka ghafla pembezoni mwa mji wa Bukoba akiwa anakwenda kazini; kupoteza fahamu. Alikimbizwa hospitali ya mkoa mjini humo ambapo alilazwa.

Siku chache baadaye, mwandishi mwingine, Benjamin Rwegasira wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), naye alikumbwa na ugonjwa unaofanana na ule uliompata Owamani. Naye akalazwa katika hospitali ya mkoa.

Kinachoshangaza wengi mjini Bukoba na vijini wanakotoka waandishi hao, ni kukumbwa na ugonjwa wenye dalili zilezile, wakati mmoja na kwa watu wanaofanya kazi moja.

Waandishi wote wawili wana dalili za kupata ganzi usoni, kupooza mkono au mguu.

Wote wawili wana dalili za kutoongea na kutoelewa mambo; kutoona vizuri; kutokuwa na uwezo wa kutembea; kuwa na kizunguzungu na kuumwa kichwa kwa muda mrefu bila kukoma.

Dalili nyingine ni kujisikia kuwa na homa; kuwa na kichefuchefu na hata kutapika.

Hivi sasa wametoka hospitalini. Kila mmoja amelala nyumbani kwake. Hawana uwezo wa kutembea. Wamepoteza uwezo wa kuongea. Hawana uwezo wa kipato kujisaidia wao na familia zao.

  Taarifa za kuaminika zinasema tangu waandishi hao walipokumbwa na maradhi hayo, hawajapata msaada wowote kutoka kwa waajiri wao.

Mwandishi mmoja mjini hapa amenukuliwa akisema, “Hii ndiyo njia yetu sote. Wahaya husema, ‘mlo wako ni mguu wako. Kama huwezi kutembea na kujitafutia, utakufa tu,’ hakuna cha nilikuwa nimeajiriwa na fulani.”

Hata simu za waandishi hawa za mkononi hazipatikani. Inalazimu kupitia simu za ndugu na marafiki wa karibu wanaoeleza hali zao.

Hadi sasa, miongoni mwa madaktari ambao mwandishi huyu ameonana nao katika hospitali ya serikali mjini Bukoba, hakuna aliyekubali kueleza ni ugonjwa gani uliowapata waandishi hao.

Mhariri: Gazeti hili limepata simu ya kijana mmoja aitwaye Edwin (0684175695) wa mjini Bukoba. Kupitia kwake lilimpata Owamani ambaye alisema ameanza kupata nafuu.

Akiongea kutoka nyumbani kwake, Hamugembe, mjini Bukoba, juzi Jumatatu, Owamani alikuwa hasikiki vizuri; sauti ilikuwa ikikatikakatika na hatimaye kupotea.

Taarifa nyingine zinasema mwandishi Benjamin Rwegasira alipelekwa Loliondo kupata kikombe cha “babu” na baada ya hapo alikwenda mjini Mwanza. Hali ya afya yake haikuweza kufahamika.

0
No votes yet