Waandishi na serikali: Nani anaingilia mahakama?


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 25 July 2012

Printer-friendly version

BAADHI ya wahariri na waelekezaji wengine katika tasnia ya habari, wamekuwa wakikariri kuwa jambo au shauri likiwa mahakamani, basi mwandishi hastahili au hapaswi kuandika lolote juu yake.

Hili limetesa waandishi wengi walioamini kuwa kwa kuandika lolote watakuwa wanaingilia mahakama. Ndimara Tegambwage ni mmoja wa waelekezaji katika tasnia hii. Yafuatayo ni maoni yake kama yalivyochotwa kutoka mtandao wa Mabadiliko juu ya mgomo wa madaktari na juhudi za serikali kufunga akili na midomo ya wananchi.

NIMEKUWA nikieleza na hata kuelekeza, tofauti na baadhi ya wenzangu katika uandishi, kwamba jambo lililoko mahakamani linaweza kuandikwa. Kwa nini?

Kwamba jambo liko mahakamani, hakuzuii mambo mengine kutendeka juu ya hilohilo na nje ya mahakama. Dunia haisimami kwa kuwa jambo liko mahakamani.

Mwenendo wa kilichosababisha kuwa mahakamani hausiti au kufutika eti kwa kuwa tayari kuna shauri mahakamani. Hamu na haki ya kujua haviondoki eti kwa kuwa jambo liko mahakamani. Hapana!

Sheria haikuzuii na hasa haipaswi kukuzuia kuandika mlolongo wa matukio nje ya mahakama unaohusu watu wenye shauri lililoko mahakamani.

Matukio nje ya mahakama yaweza kutoa nuru zaidi juu ya wahusika katika shauri na hata juu ya shauri lenyewe. Taarifa juu ya matukio haya zaweza kuwa za msaada kwa wakili wa utetezi na wakili wa upande wa mashitaka.

Wakati (taarifa hizo) zinaweza kumpa mmoja nuru zaidi juu ya kilichotendeka, zaweza pia kumpa mwingine nuru juu ya kujenga ngome.

Hakimu au jaji anahitaji hoja mshibano na ushahidi mwanana (kama inavyowasilishwa mahakamani na siyo kama inavyosimuliwa nje). Uamuzi wake haupaswi kuongozwa au kutawaliwa au kufungwa na taarifa za magazeti, redio, televisheni au chombo chochote kile cha kutoa taarifa au habari.

Umadhubuti wa hakimu au jaji; hekima, uaminifu wake kwake binafsi na kwa kazi yake juu ya kesi iliyoko mbele yake, havipaswi kupanguliwa na taarifa za nje ya hoja zilizoko mahakamani kwa madai kuwa "zimeathiri maamuzi."

Tuna ushahidi ambako baadhi ya mahakimu na majaji madhubuti wamepuuza na kutupilia mbali madai ya kuathiriwa na vyombo vya habari wakiuliza, "Una uhakika na unaamini kuwa mimi siwezi kufanya kazi hii; siwezi kuwa na maoni na siwezi kuona haki mpaka niambiwe na vyombo vya habari?"

Hili lina maana kwamba kupogoka; kuangalia sheria kwa makengengeza na hata kutoa upendeleo wa waziwazi na uliofichika, ni shabaha, tena ya makusudi, ya hakimu au jaji na siyo kuathiriwa na taarifa za chombo cha habari.

Twende kwa serikali. Taarifa ya serikali ambayo iliahidiwa (juu ya mgomo wa madaktari); kama ingekuwepo, isingeingilia shauri lililoko mahakamani.

Haikuwepo au kuna kilichoingia katikati na kusababisha wasiitoe, ambacho ni wao pekee wanaokijua. Kwamba serikali haitatoa taarifa kwa kuwa imegundua shauri lake na madaktari liko mahakamani, ni sababu ya kizembe mno kutolewa na mamlaka.

Na kama serikali inaweza kusahau ilichofanya juzi tu, basi hii ni barua kwa umma ya kuomba kuaga ikulu.

Sheria haizuii wala kufunga, kwa mfano serikali, kutoka na taarifa inayosema: "Tumepata fedha za kutosha. Sasa madaktari watalipwa nusu ya wanachodai. Hapa tutapata pa kupumulia na kuendelea na majadiliano."

Sheria ipi itazuia hili. Sheria yaweza kununa iwapo serikali itatoka na kusema, "Mtakoma. Msimamo wetu ni uleule, liwalo na aliwe!"

Hili halikubaliki mbele ya hekima, achilia mbali mahakama. Huwezi kwenda mahakamani kuomba nafuu; ukarudi kesho yake kukaza nguvu ya amri ya kukupa nafuu; na kesho yake ukatoka kifua mbele, kwa kutumia nafuu ileile, kuwakomalia wale uliozuia, na isivyo haki, lakini ilivyo halali kisheria.

(Hapa) utakuwa umetumia nguvu ya mahakama kujinufaisha binafsi na utakuwa unajigamba kana kwamba umeweka "mahakama mfukoni."

Inawezekana serikali "imegundua kweli" kuwa inakwenda kufanya madudu. Ikaacha kutoa taarifa. Imejichanganya kwa kuwa imechanganyikiwa.

Hiyo ilikuwa  Alhamisi 28 Juni 2012, wakati nikijadili mtandaoni. Lakini nililoandika la kutumia “nguvu ya mahakama kujinufaisha binafsi…kana kwamba umeweka ‘mahakama mfukoni,” ndilo lilitokea baadaye.

Serikali ya Rais Jakaya Kikwete imekwenda mahakamani. Ikaomba nafuu. Ikapewa. Ikatoka mbele. Ikawakomalia madaktari. Ikaanza kuwashambulia. Kuwafukuza kazi kabla ya kile ilichoita “shauri kuu kusikilizwa na kumalizwa.”

Haya basi, siyo matumizi sahihi ya nafuu ya mahakama. Serikali ilikuwa na uwezo wa kufanya iliyofanya bila kutumia nguvu ya mahakama. Haikuhitaji ruhusa ya mahakama kufukuza madaktari.

Kwahiyo, serikali imeonyesha jinsi ilivyohitaji mahakama kufunga mikono, miguu na midomo ya madaktari, ili yenyewe (serikali) ipate nafuu na kuweza kuwacharaza wagomvi wao. Huku ndiko kuingilia mahakama.

Hapa ndipo vyombo vya habari vinajikuta vimetwishwa jukumu la kupaza sauti za wananchi na madaktari; na hata sauti ya mahakama – kupinga  matumizi mabaya ya mhimili mwingine wa dola (mahakama); tena kwa sababu dhaifu.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)