Waarabu wamtosa Bashar al-Assad


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 25 July 2012

Printer-friendly version

RAIS wa Syria, Bashar al-Assad amebanwa kila upande; ndani vita vikali na nje Umoja wa Nchi za Kiarabu unataka ajiuzulu.

Tamko la Umoja wa Nchi za Kiarabu limekuja katikati ya mapambano makali ya silaha kati ya majeshi ya serikali na waasi katika viunga vya jiji la Damascus na mji wa pili kwa ukubwa wa Aleppo.

Hali ikiwa hivyo, upinzani umesema mapambano hayo ni ishara kwamba “wako kwenye milango ya ushindi” huku jeshi la waasi la Free Syrian Army (FSA) likitamba utawala wa Assad umeparaganyika.

Jijini Brussels, Umoja wa Nchi za Ulaya (EU) uliongeza vikwazo dhidi ya utawala wa Assad na kupiga marufuku silaha kwenda Syria na kwamba zitakuwa zinafanya upekuzi katika meli na ndege zinazoshukiwa kubeba silaha hizo, wanadiplomasia wamesema.

Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa juzi baada ya kikao chao cha Doha, Qatar, mawaziri wa Umoja wa Nchi za Kiarabu umemtaka Assad "kuachia madaraka” na wakaahidi kwamba yeye na familia yake watawasaidia “watoke salama”.

"Kuna makubaliano hapa juu ya haja ya kumtaka Rais Bashar al-Assad ajiuzulu haraka,” alisema Waziri Mkuu wa Qatar, Sheikh Hamad bin Khalifa Al-Thani alipozungumza na waandishi wa habari saa chache baada ya kumalizika mkutano huo.

Umoja wa Nchi za Kiarabu umekwenda mbali zaidi na kutaka Jeshi la Waasi na upinzani kuandaa serikali ya mpito yenye misingi ya umoja wa kitaifa “ikishirikisha baadhi ya watu kutoka serikali ya sasa” bila kutaja nani hasa kutoka serikali ya sasa.

Hofu imetanda katika nchi za Magharibi baada ya ripoti kueleza kwamba Assad anaweza kutumia silaha hizo za maangamizi ili kuiokoa serikali yake.

Sheikh Hamad amemtaka Assad "kuacha kuangamiza na kuua watu badala yake achukue maamuzi magumu” aachie madaraka aliyoshikilia tangu mwaka 2000.

Aidha, mataifa ya Kiarabu yametaka ufanyike mkutano usio wa kawaida wa Baraza la Umoja wa Mataifa ili kuweka mipaka ya “ukanda salama” nchini Syria.

Umoja wa Mataifa ulitangaza Jumapili kuwa “utamtia hatiani” ofisa yeyote wa Syria atakayehusika kuruhusu matumizi ya silaha za kemikali nchini.

Hali imeendelea kuwa tete kwani wananchi wamekuwa wakisikia milio ya bunduki na milipuko mikubwa mapema alfajiri katika maeneo ya Mazzeh yaliyo magharibi mwa Damascus. Taarifa za wanaharakati zinasema walisikia milio ya bunduki katika maeneo mbalimbali ya wilaya katika jiji hilo.

Televisheni ya serikali imeripoti kwamba sghambulizi katika eneo la Mazzeh, “lilifanywa kwa malengo na kwa ghafla."

Mtangazaji alionyesha picha za askari wakifyatua risasi walipokuwa wanaingia katika maeneo jirani na pia wakafanya mahojiano na askari mmoja.

Ripoti inasema, vikosi vya serikali pia "vilitimua mabaki ya askari magaidi eneo la Barzeh," kaskazini mashariki mwa Damascus.

Asasi ya Uchunguzi wa Haki za Binadamu ya Syria, imesema shambulio kali la serikali katika mji wa Barzeh, likiongozwa na “Brigedi ya Nne” iliyo chini ya Maher, mdogo wake Assad, lilisababisha wakazi wengi kutoroka mji.

0
Your rating: None Average: 3.8 (4 votes)