Wabunge na ‘madarasa mawili’


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 25 January 2011

Printer-friendly version
Uchambuzi

JANA wabunge walitarajiwa kuanza mafunzo ya siku 10 mfululizo. Wapya watakuwa wakijifunza: a e i o u za bunge. Wale wa zamani watakuwa wakiambiwa kuachana na mazoea.

Bali uwakilishi haufundishwi. Uwakilishi ni fukuto. Liko ndani ya mbongo na vifua vya wabunge. Ni fukuto lililosukuma wengi kuomba kura; ili wawe bungeni.

Siku 10 za darasa kwa wabunge haliondoi fukuto. Linapaswa kuandaa mifereji ambamo fukuto litapita. Bali darasa laweza kugeuka na kuchukua sura ya kujenga vihunzi, matuta na hata vizibo.

Ikitokea ikawa hivyo, fukuto huwa moto usiopoa. Usiozimika. Uwezao kulipuka. Usio simile. Bunge huchemshwa na kuchemka; na kila lichemkapo, wananchi hufurahia uhai wa hoja na ukaribu wa wawakilishi wao.

Bahati mbaya sikualikwa kuwa mmoja wa watoa mada katika siku 10 za darasa la wabunge. Najua ningealikwa ningepewa somo la “Uhusiano kati ya mbunge na vyombo vya habari.”

Kwa kuwa sikualikwa, najialika kutoa mada hii: “Kilio cha wananchi cha muda mrefu – bomoa ufisadi tupate nafuu!”

Wabunge wanaombwa kuangalia kupanda kwa bei ya umeme na kuhusisha mwenendo huo na mikataba ya kinyonyaji kuhusu nishati.

Wahusishe nia ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ya kuagiza serikali kuchota, bila huruma, mabilioni ya shilingi – kodi za wananchi – kulipa kampuni ya kufua umeme ambayo haifui umeme – Dowans.

Wala hili halihitaji kurudishwa bungeni. Liliishapita pale. Liliishamuliwa. Ni mbongo na koo za wabunge wapenda nchi yao kunena: “Haramu huzaa haramu,” na kwamba jasho na damu ya wananchi havistahili kwenda kwa haramu.

Wabunge wakubali kuwa na madarasa mawili. Wachepuke kidogo. Siyo kutoroka. Kwa dakika chache waingie darasa jingine tuwaonyeshe anayejua mambo; mtu wa kuwaeleza nani alileta wazo la mradi huu wa kufua umeme.

Mtu wa kuwatobolea nani aliandika mradi wa kwanza kwa matumaini kuwa kampuni teule haitahusishwa kwenye mchakato wa zabuni.

Si waje tu waelezwe mchovu aliyekuwa anamaliza muda wake nchini – katika ofisi za fedha nyingi duniani – jijini Dar es Salaam, alivyokuwa amejipangia fungu la sitini wakati wa kuandika?

Wabunge si waje tu na kuelekezwa jinsi ya kutafiti na kujua nani alikuwa amepangiwa kupata senti ngapi kwa kila dola itokanayo na mkataba iwapo mradi ungepita?

Kwani hilo somo haba? Si wabunge waje na kuelekezwa nani alithibitisha kuwa mradi wa awali wa umeme ulikuwa sahihi?

Lakini mambo yalipochacha mtu huyohuyo akaitwa tena na kuthibitisha kuwa huo ulikuwa mradi mbaya/bomu.

Bado yalipoingia mashauri mtu huyohuyo akaitwa kutetea upande aliojua ulistahili kushindwa, tena kwa msaada wake, ili mabilioni ya shilingi yatinge kibindoni.

Haya hayamo katika darasa la spika na katibu wa bunge la siku 10. Hayamo! Haya yamo katika fukuto la mbunge binafsi na wabunge kama kundi la watu wenye uchungu na nchi yao.

Kutinga kwa mabilioni ya shilingi katika mifuko ya wachache ndio chanzo cha kupanda kwa umeme, ongezeko la bei ya mchicha, kupanda kwa nauli na hata kupaa kwa sahani ya ugali kwa wale wala-mara-moja mijini na vijijini.

Dowans ni ileile Richmond. Ni “mambo  mchoromchoro.” Sasa taarifa zimeenea kwamba kampuni moja ya Marekani itanunua Dowans na kuanzia hapo, wamiliki wa kampuni hiyo watajulikana waziwazi na siyo wale wa kubuni.

Marekani inunie Dowans kupeleka wapi? Marekani na skrapu wapi na wapi? Wanataka kuyeyusha vyuma na kutoa uji wa kutengenezea vifaa vingine?

Wabunge wakichepuka, kwa dakika chache kutoka darasa la spika Anna Makinda, watajua nani alikuwa mwenyekiti wa vikao vilivyopitisha Richmond isiyo na fedha, isiyo na utaalam, isiyo na hadhi. Watajua.

Kilio cha wananchi ni kwamba mabilioni ya kulipa Dowans ni mengi. Yataacha pengo. Kuliziba pengo hilo, hakika ni kulia na kusaga meno.

Na uwezo wa kutolipa Dowans upo. Sababu za kutoilipa hakika zipo. Bali watawala hawana nia. Hili ni kundi la kupuuzia lisilo na mashiko kimataifa na lisilo na hadhi ya kuathiri hata mahusiano kati ya Tanzania na nchi au makapuni mengine.

Kwa nini? Kwa sababu historia ya ujio wa Richmond, kupatikana kwa mkataba, udhaifu uliojitokeza na hatimaye kuja kwa Dowans na ilivyoingia katika biashara; vinathibitisha kuwepo ujanjaujanja ambao, kwa misingi ya kibiashara duniani haupaswi kuheshimiwa.

Somo hili kwa wabunge na hasa msisitizo kwamba wabomoe ufisadi ili wananchi wapate nafuu, ndiyo sauti pekee iliayo katika nyika za kisiasa.

Somo hili la wananchi haliishii kwa Dowans na Richmond. Wabunge wanatakiwa wachepuke, kutoka darasa la Anna Makinda, ili waonyeshwe mengi ya kubomoa.

Wananchi wanaagiza wabunge wajitahidi kupata macho ya nyongeza, masikio ya nyongeza na sauti za nyongeza katika kutafuta huyu aitwaye Kagoda Agriculture Limited. Ni nani huyu?

Serikali, kwa miaka sita sasa, imekataa kusema Kagoda ni nani – huyu aliyekwapua zaidi ya Sh. 40 bilioni kutoka akaunti ya madeni ya nje katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Lazima apatikane wa kubomoa ufisadi ili wananchi wapate nafuu. Mbunge wa kukaba serikali kutoboa siri ya Kagoda – kampuni iliyoiba BoT, ikapitia CRDB na kutokomea.

Na siyo kweli kwamba serikali haijui nani aliiba. Hata kamati ya rais kuhusu walioiba benki itakuwa iligundia Kagoda ni nani.

Somo la leo ni bomoa ufisadi ili wananchi wapumue. Wakati wabunge wakikaririshwa kanuni na taratibu nyingine za bunge, kwa siku 10, fukuto ndani ya nyoyo zao linapaswa kupanda na kujiuliza: “Kama hatubomoi hili, sisi ni wa faida ipi?”

Karibu wabunge wote safari hii wanajua kilio cha wananchi kuhusu makampuni ya Meremeta na Deep Green ambayo yalichota mabilioni ya shilingi na kutokomea.

Siyo kweli kwamba serikali haijui makampuni hayo na wamiliki wake. Siyo kweli kwamba kama haiwajui haiwezi kuwapata. Inaweza. Kwa nini imekaa kimya? Jeuri tu.

Serikali ilifikia hatua ya kudai kuwa Meremeta ni kampuni ya jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kwamba serikali inaimiliki kwa asilimia 100.

Utafiti zaidi ulipogundua kuwa Meremeta ni kampuni iliyosajiliwa nje ya nchi na kwamba ilikuwa inaruhusu kurithiwa na “wapwa,” serikali ikaumbuka.

Aliyeishikisha masikio alikuwa Dk. Willibrod Slaa aliyeuliza mara kwa mara: “Mpwa wa serikali ni nani?” Hata hivyo serikali ikakata ulimi.

Wabunge someni ya spika Makinda. Ni muhimu kujua vianzio katika jumba la wananchi. Lakini ni muhimu zaidi kuneemesha fukuto akilini na vifuani – maarifa na ujasiri.

Wananchi wanataka kuona wabunge wakitoka jasho huku wakibomoa ngome ya ufisadi ili maisha yao yasiwe magumu zaidi; ili wasife wakati wachache wanaendelea kujiongezea umri na hata uhai.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: