Wabunge CCM watetea maslahi binafsi


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 25 April 2012

Printer-friendly version
Makao makuu ya CCM

WIZI wa rasilimali za taifa – kuanzia wizi wa fedha ndani ya Benki Kuu (BoT), uuzaji wa mashirika ya umma, nyumba za serikali hadi viwanda na mashamba –  haukuanza leo.

Lakini kwa muda wote huo, hatukuwahi kusikia hata mara moja, wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakipiga kelele kutaka waliohusika na wizi wafutwe kazi.

Hatujasikia wakitaka wahusika washitakiwe. Badala yake, wametoa kauli za kejeli kwamba, “mwenye ushahidi” juu ya hili au lile alete.

Lakini sasa hawa hapa wabunge wa CCM. Wanamtunga kidole jichoni rais wao na mawaziri. Hili siyo baya. Ni halali kabisa.

Lakini kwa nini haya yanakuja sasa; tena juu ya ufisadi mkubwa unaonuka ambao wamekuwa wakipuuzia?

Jibu liko wazi. Ni vita vya makundi; vya madaraka na ubinafsi. Ni kinyang’anyiro cha urais mwaka 2015 ambacho kilianza miaka saba iliyopita.

Ni miaka karibu minane sasa, tangu kampuni ya Kagoda Agriculture Ltd., ikwapue mabilioni ya shilingi kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya BoT.

Hatujasikia wabunge wa CCM wakihoji serikali na kutaka kushinikiza kumfikisha “Kagoda” mahakamani au kushitaki anayemlinda.

Sasa ukiondoa wabunge watatu wa chama hicho, Deo Filikunjombe (Ludewa), Kangi Lugora (Mwibara) na Ally Mohammed Keissy (Nkasi Kaskazini), wote waliotaka mawaziri wajiuzulu kwa madai ya kukiaibisha chama, walikuwa kwenye kundi moja, lakini lenye malengo tofauti. Keissy ametokea upinzani. Msimamo wake kwenye mambo yenye maslahi ya taifa si wa kudandia. Lugora na Filikunjombe wamekuwa thabiti kwa mambo yenye maslahi kwa taifa.

Lakini Peter Serukamba, mbunge wa Kigoma Mjini, ambaye alitaka wabunge wa chama chake wakafanye kazi ya kuwajibisha mawaziri wanaotuhumiwa kwa ufisadi, haamini katika kuwepo ufisadi.

Hadi anatoa kauli ya kutaka kufukuza wenzake, Serukamba bado anaamini na anaendelea kuamini kuwa Edward Lowassa alituhumiwa bila makosa katika kashfa ya ufisadi wa Richmond.

Lakini ni Serukamba anayedai mawaziri ni wezi. Wamekiaibisha chama chake na taifa. Anasema ili kukinusuru chama na kurejesha hadhi ya serikali inayomomonyoka, sharti wawajibike.

Katika hili, Serukamba hataki ushahidi wala kutoa nafasi ya utetezi kwa wahusika. Hapa yuko kazini. Anakamilisha mradi wa “kusafishana.”

Hata Livingstone Lusinde (Kibajaji), mbunge wa Mtera, ni kutoka kundi la akina Serukamba. Hana na hawezi kuwa na uchungu na CCM wakati ni mdandiaji wa juzi tu.

Kwanza, Serukamba na Lusinde wanajua hatua ya kufukuza mawaziri wanane kwa tuhuma za ufisadi, itaongeza idadi ya wachafu ndani ya CCM na serikali.

Wachafu wapya watakuwa wale ambao walikuwa wanajifanya bora na wanaohaha  kumrithi Kikwete. Hivyo kuondoka kwa hao, kutapunguza kiwingu kwa mgombea wanayemuunga mkono.

Pili, kama mawaziri wataondolewa kwa tuhuma za wizi, itathibitisha kuwa ndani ya CCM hakuna aliyesafi; hivyo kumnyoshea kidole Lowassa itakuwa ni kumuonea.

Tatu, Serukamba anajua kuwa kwa vile uwaziri unatolewa kimkoa; na katika mkoa wake wa Kigoma karibu majimbo yote yamekwenda upinzani; anaweza kubahatika kupata uwaziri au hata unaibu waziri. Hiyo inaweza kuwa ndiyo tofauti kati ya Lusinde na Serukamba.

Wengine waliochangia kwa hasira, walikuwa wanafanya hivyo kwa kushinikizwa na wale wanaotafuta uwaziri.

Taarifa zinasema, hata baadhi ya naibu mawaziri walifurahia kilichokuwa kinatendeka kwa kuwa waliona hiyo ilikuwa fusra pekee ya wao kupanda ngazi.

Baadhi ya mawaziri – wale wanaoamini wametupwa kwenye wizara ambazo hazina mlo – waliona kuondoka kwa mawaziri wenzao, kutawafanya wao kupata “wizara nyeti.” Ni vita vya panzi.

Wabunge wanashindwa au wanakataa kukemea makatibu wakuu waliohujumu taifa. Wanashindwa kukemea taasisi za umma – mifuko ya hifadhi ya jamii, mashirika na watendaji wengine wa serikali – waliotajwa kwenye ripoti.

Kwa mfano,  wabunge hawamshinikizi Rais Kikwete kumfuta kazi na au kumfikisha mahakamani, katibu mkuu wa wizara ya fedha, Ramadhan Khijjah, anayetuhumiwa kwa matumizi mabaya ya madaraka.

Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), inaonyesha Kijjah ndiye alikuwa mwenyekiti wa kikao kilichoidhinisha malipo yenye utata ya Sh. 2.34 bilioni zilizolipwa kwa kampuni ya DRTC ya jijini Dar es Saalam.

Katika taarifa yake – ambayo wabunge ndiyo waliitumia kutaka Mkullo ajiuzulu – CAG anasema, katibu mkuu wizara ya fedha, ndiye aliongoza kikao cha kuamuru kulipwa fedha hizo. Hawamgusi huyo.

Wabunge hawazungumzii “mazingaombwe” ya serikali na kampuni ya Independent Power (IPTL) ambako kila mwezi serikali, inalipa Sh. 15.7 bilioni zikiwa “gharama za kununulia mafuta ya kuendeshea mitambo.”

Hawasemi haya kwa sababu, wanajua huko kutafumua mengi. Kutaingiza hata wake wa mawaziri wa sasa na waliopita. Kutawaanika wake wa viongozi wa juu serikalini na katika chama.

Wabunge wa CCM wana sura mbili. Si wangemweleza rais na chama chake kuwa, hatua ya Andrew Chenge, kuwamo bungeni – kutunga sheria na kupitisha bajeti – inadhalilisha chama machoni mwa jamii?

Hata hivyo, jambo moja ni wazi. Ndani ya chama na serikali, mambo hayako sawa. Mmomonyoko wa maadili ni mkubwa na obwe la uongozi linaongezeka.

Tayari kundi kubwa la vijana, ambalo ndilo nguzo kuu ya uhai wa chama hiki, limeanza kujiondoa ndani ya chama hicho na kujiunga na upinzani.

Wanaojiondoa ni vijana na wazee ambao hawana majina makubwa, lakini ndiyo nguvukazi katika chama. Wanaojiondoa ni wale ambao hawana tuhuma za ufisadi wala hawajahusishwa na wizi wa mali ya umma.

Wanaojiondoa ni wale wanaosema, “…tumechoshwa na rushwa na ulanguzi wa uongozi ndani ya chama.” Hawa wana ajenda ya kueleza yote kwa wananchi.

Alianza James Millya, mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UV-CCM) mkoani Arusha. Wakafuata madiwani wawili wilayani Sengerema, mkoani Mwanza; kadri siku zinavyokwenda ndivyo idadi inavyozidi kuongezeka.

Wengine waliojiondoa ni mwenyekiti wa UV-CCM wilayani Monduli, Julius Kalanga, katibu wa uhamasishaji wa UV-CCM, wilayani Longido; wenyeviti watano wa vitongoji na wanachama 2,402 wilayani Ngorongoro.

Sasa swali la kujiuliza ni hili: CCM imefikaje hapa ilipo? Nini kiini cha haya? Kuna wanaosema kinacholitesa taifa na kuisambaratisha CCM, si vita vya urais wa mwaka 2015, bali uongozi dhaifu wa Kikwete.

Wanaoona udhaifu unaoendelea, wanavutika kuanza mikakati ya kuukwaa urais hata kabla ya wakati.

Ndiyo maana kila wakati minyukano inaongezeka kwa sababu watu wanataka kuziba ombwe.

Kubenea anaandika kutoka Chuo Kikuu cha Christelijke Hogeschoool (CHE) kilichopo mjini Ede, kilometa 130 kutoka Amsterdam, Uholanzi
0
Your rating: None Average: 4.5 (2 votes)