Wabunge, hasira haziijengi Bajeti


editor's picture

Na editor - Imechapwa 20 June 2012

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania juzi jioni lilitibuka. Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) walitibua hali ya hewa kwa kutoa lugha chafu.

Baadhi yao walidai wabunge wote wanaoiponda Bajeti ya Serikali ya mwaka 2012/ 2013 wana mapepo.

Eti wanaopinga bajeti hiyo ni vichaa hivyo walitakiwa wakapimwe kwanza katika Hospitali ya Mirembe ndipo warudi kuendelea na vikao bungeni.

Katika kuonyesha dharau, mbunge huyo alitupilia mbali kitabu cha makadirio ybadala ya kambi ya upinzani akidai ni utumbo mtupu, halafu akashika skafu yake ya chama na kuonyesha juu halafu akashangiliwa na wenzake.

Halafu mbunge mwingine alisema iwapo milango ya jengo la Bunge itafungwa ana uhakika watawachapa wabunge wa upinzani maana wao CCM ni wengi kuliko wale wa upinzani.

Kwa kiasi kikubwa, mbunge huyo alilenga kambi ya upinzani iliyokosoa bajeti hiyo kwa nguvu ya hoja huku ikitoa mapendekezo namna ya kuboresha. Hata mbunge mmoja mmoja aliposimamia alikosoa vikali.

Waliokosoa bajeti hiyo na kukataa kuiunga mkono hadi maeneo kadhaa yarekebishwe si wapinzani tu, hata wabunge wa CCM.

Inasikitisha kuona kwamba hata baada ya miaka 20 ya mfumo wa vyama vingi nchini, wabunge wa CCM bado hawajui wajibu wa vyama vya upinzani linapofika suala la bajeti.

CCM hawajui kwamba wajibu wa upinzani si kusifu na kushangilia kwa makofi na vigelegele bungeni, bali ni kukosoa na kutoa mawazo mbadala ili kuboresha Bajeti.

Jambo zuri ni kwamba mambo mengi mazuri katika bajeti mbadala yamekuwa yakichukuliwa na Serikali na kutekelezwa japo si kwa ukamilifu wake.

CCM waliokabidhiwa nchi na kuunda serikali walipaswa kujua kujadili au kujibu hoja kwa jazba, hasira, vitisho hakusaidii kutetea, kujenga na kuboresha bajeti bali ni hoja.

Aidha, ieleweke kwamba kampeni za uchaguzi zilikoma miaka miwili iliyopita, lakini kila siku chama kinapaswa kufanya kampeni za kujijenga ndani na nje ya Bunge. Anayedai kampeni ni wakati wa uchaguzi tu hajui siasa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: