Wabunge, kunani pale Kigamboni?


Paschally Mayega's picture

Na Paschally Mayega - Imechapwa 11 January 2012

Printer-friendly version

KIKUNDI cha muziki wa kizazi kipya kutoka Tanga kilichojulikana kama Wagosi wa Kaya kiliimba wimbo maarufu ulioitwa “Tanga kunani pale?” Natumia falsafa ya wimbo huo kuwauliza wabunge wa Dar es Salaam, “Kigamboni kunani pale?”

Nyongeza ya nauli ya kivuko kutoka Sh. 100 hadi Sh. 200 iliwasha moto siyo kwa wakazi wa Kigamboni tu, bali pia maeneo mengine jijijini Dar es Salaam. Hata wabunge wanaoonekana kuwa tegemeo la wananchi wamejikuta nao wakiingizwa katika sakata hilo pasipo kutegemea.

Mchezo wa bao una majina mengi. Ukicheza kete zikaishia mahali  unapokula hizo huitwa komwe, yaani mtaji. Zikizidi kumi na tano katika tundu moja inakuwa nyumba. Ni kete lakini siyo mtaji. Haili kitu.

Unachoweza kufanya nayo ni kutakata wenyewe huita kusafiri. Baada ya wabunge wa Dar es Salaam kudhani ongezeko la nauli hiyo linaweza kuwa mtaji wao kisiasa walianza kucheza lakini wakajikuta wanasafiri, kutakata au kupwayuka.

Wananchi waishio Kigamboni ghafla wamegeuka ‘dili’ kwa wabunge wa Dar es Salaam. Pamoja na ushawishi wote wa Waziri wa Ujenzi, John Pombe Magufuli, ghafla amegeuzwa kaburu.

Wabunge wanamjua Magufuli kwamba ni mwingi wa masihara. Utani tu kuwa “jamani ee, kama hamuwezi kulipa Sh. 200 pigeni mbizi” umeshupaliwa kwamba ni matusi.

Hivi, mmesahau Magufuli huyu, kwa utani amewahi kusema Chama Cha Mapinduzi kuwa ni Chama Cha Mungu? Likawa zogo bungeni. Safari hii tena wabunge wa chama chake wanapita wanatakata “kawadhalilisha wananchi, kavunja katiba, ajiuzuru” na maneno mengi ya kitoto.

Tuwaulize wabunge, “Mapenzi makubwa kwa waishio Kigamboni yametokana na ile shilingi mia tu ya kivuko kweli?” CCM Mkoa wa Dar es Salaam, nao wakitumia maneno chakavu wametoa kauli iliyofilisika kabisa. Badala ya kumtaka Waziri Magufuli awaombe radhi Watanzania wote kwa kusimamia uporaji wa nyumba za serikali katika awamu ya tatu, wao wanataka awaombe radhi watu wa Kigamboni kwa utani wa kitoto, ambao hauwezi kumuudhi mtu yeyote mwenye akili timamu.

Kwanini CCM hawaoni Sh. 200,000 walizojiongezea wabunge (wakiwemo wa Dar es Salaam) kama posho kwa vikao bungeni kuwa ni mzigo kwa watu wa Kigamboni?

Kwanini CCM mkoa hawakemei Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa kukawiza malipo ya posho za madaktari hadi wanagoma, na ya walimu hadi wakatishia kugoma?

Wakazi wa Kigamboni wana shida lukuki; kuanzia mgawo wa umeme, uhaba wa mafuta baada ya wafanyabiashara wa mafuta kugoma hadi bei ya sukari na mfumko wa bei kwa vyakula na bidhaa zote.

Wabunge na CCM mkoa wanaona ni sahihi kwao lakini Sh. 100 ya Magufuli imewakusanya wabunge wote wa Dar es Salaam. Kunani pale?

Nauli ya kivuko Kigamboni haijawahi kupanda kwa kipindi cha miaka 14. Inapandishwa sasa kwa Sh. 100. Wabunge waliokimbilia Kigamboni kutoa msaada watuambie kwenye majimbo yao nauli za daladala zimepanda mara ngapi tena kwa kiasi gani katika kipindi hicho cha miaka 14?

Kituo cha mabasi Ubungo, ukimsindikiza jamaa yako unatozwa Sh. 200. Hupewi huduma yoyote, kuingia tu. Kwa wabunge hawa Sh. 200 hii ni sawa ila nauli mpya ya Sh. 200 ni dhambi.

Hatua hii itawasukuma wananchi waikumbuke kauli ya Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Masaburi kuwa wabunge wa Dar wanafikiri kwa kutumia…! Muda si mrefu watamwamini na kuona alisema kweli!

Kinachojitokeza hapa ni kwamba tatizo si Sh. 100 ila Magufuri mwenyewe. Machi mwaka jana Waziri mkuu, Mizengo Pinda alifanya ziara ya Mkoa wa Kagera kwa lengo kufuta nyayo za maandamano ya CHADEMA na kujua kiini cha ulanguzi wa sukari katika mikoa ya Ziwa. Safari hiyo ilimfikisha katika Jimbo la Chato ambako alimfunda Magufuli jinsi ya kufanya kazi mbele ya wapiga kura wake.

Pinda alikubali waonekane kama jamaa tu wa mtaani wasio na utaratibu wa kufanya kazi wala ofisi ya kufanyia kazi. Huko alimtaka Magufuli aache kubomoa nyumba za watu badala yake arudi jimboni kuhimiza wananchi kujiletea maendeleo.

Siku chache baadaye, Rais Jakaya Kikwete alimwambia pia Magufuli aache ubabe wakati wa kutekeleza agizo la kubomoa nyumba za watu waliojenga kwenye hifadhi ya barabara. Magufuli alinyong’onyea miezi kadhaa kabla ya kupewa maelekezo mapya.

Magufuli ndani ya chama chake ni moto. Wanamhitaji ili waivishe lakini akiwaka nao wanaungua. Yeyote aliyemtendaji mahiri ndani ya chama chao ni maumivu ya kichwa hasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Hofu.

Magufuli anakuwa katikati ya sakata hili huku kukiwa na sintofahamu kuhusu ujenzi wa mji mpya Kigamboni. Wakazi wa Kigamboni wanatakiwa kuhama ili kupisha ujenzi wa mji mpya. Nani anajenga mji mpya na nani atalipa fidia ni siri kubwa.

Fununu zinasema wakazi wa Kigamboni wanaswagwa kuondoka ili kumpisha aliyekuwa Rais wa Marekani, George W. Bush. Inadaiwa amenunua au atawekeza na yuko tayari kulipa gharama za wanaohamishwa.

Wanasema Bush anawindwa kama faru anavyowindwa na majangiri. Hatembei ovyo duniani lakini hapa kwetu anakuja kama kwake. Kila anapokuja huibuka sekeseke la aina yake kwa wakazi wa Kigamboni.

Alipokuja nchini mara ya mwisho, Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka alitangaza vikao viwili na wakazi wa Kigamboni kwa lengo la kulainisha wakazi. Mpaka sasa serikali imezuia wakazi wa Kigamboni kuendeleza nyumba na viwanja vyao.

Kuna sintofahamu Kigamboni. Habari zinasema Bush awe amenunua eneo hilo au anawekeza tu, yuko tayari kumlipa kila mkazi anayepaswa kuhama kwa fedha anazotaka ili asichakachuliwe maana hataki bugudha baadaye.

Inasemekana serikalini wamegoma. Wanataka walipwe wao halafu watawalipa wakazi. Kama habari hizi ni za kweli, basi wabunge wavalie njuga suala hili ili wananchi wapate haki yao.

Wakati mnunuaji anataka kutenda haki viongozi wa serikali wanataka kuwasukuma wakazi hawa wahame wenyewe. Bila fidia?

Hili ndiyo suala la msingi kuliko hata ongezeko la Sh. 100 katika nauli. Wabunge waibane serikali ikomeshe wizi siyo kwenye kivuko tu bali sehemu zote katika nchi hii ili raslimali nyingi zilizopo zitumike kumboreshea kipato mwananchi wa chini ili aweze kulipia gharama  zilizoongezeka katika maisha siyo nauli ya kivuko tu.

0713334239, ngowe2006@yahoo.cm
0
No votes yet