Wabunge 'wakwepa' kodi


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 14 April 2009

Printer-friendly version

WABUNGE wa Bunge la Tanzania hawalipi kodi ya mapato katika posho zao zote wanazolipwa zinazokaribia mara tano ya mshahara wao, imefahamika.

Kwa mujibu wa taratibu zilizobuniwa na serikali tangu utawala wa awamu ya tatu, posho pekee ambayo mfanyakazi hakatwi kodi ni ya nyumba.

Serikali ilipitisha utaratibu huo wakati wa utawala wa Rais Benjamin Mkapa kwa lengo la kuzuia ukwepaji wa kodi iwapo watu watalipwa mshahara mdogo na mlolongo mrefu wa posho zisizokatwa kodi.

Tangu wakati huo, posho zote ziliunganishwa kwenye mshahara na kukatwa kodi ambazo zilisaidia serikali kupata mapato zaidi ya kuendesha majukumu yake.

Wabunge ni miongoni mwa watumishi wa umma wanaopata mafao manono, ikilinganishwa na makundi mengine yanayolipwa na serikali huku mapato yao kwa mwezi yakifikia Sh. 6 milioni.

Katika mapato hayo, fedha pekee inayokatwa kodi haizidi Sh. 2 milioni, ikihesabiwa kama mshahara.

Pamoja na mambo mengine, wabunge nchini hulipwa posho ya mafuta jimboni, posho ya dereva na posho za vikao.

Taarifa zinasema mbali na kutolipa kodi, bado wabunge wanalipwa posho ya mafuta ya takribani Sh. 3,000 kwa lita moja, huku bei ya mafuta ikiwa haizidi Sh. 1,300 kwa sasa.

Kinachoendelea kwa wabunge kwa sasa ni juhudi za kukusanya fedha wakilenga mwakani kwenye uchaguzi mkuu.

Kwa hivyo, hatua yoyote ya kutaka kupunguza posho zao kwa njia ya kodi inaweza kuibua mjadala mkali bungeni na kwa jamii.

Mbunge wa Karatu na Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilbrod Slaa anasema kwamba wabunge wamewahi kuishauri serikali itoze kodi posho wanazoliwa wabunge, lakini hafahamu sababu ya serikali kutofanya uamuzi hadi leo.

Dk. Slaa ameanza kulalamikia mapato makubwa ya wabunge wa Tanzania na kushauri yapunguzwe ili kuendana na hali halisi ya uchumi wa nchi.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: