Wabunge waliobebwa ni batili


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 01 September 2010

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala

WABUNGE 20 wamepita bila kupingwa. Miongoni mwao yumo waziri mkuu, Mizengo Pinda. Taarifa zinasema kupita kwa wabunge hawa kumetokana na kile kinachodaiwa, “Vyama vya upinzani kushindwa kusimamisha wagombea.”

Hata hivyo, jambo moja ni wazi: Kwamba katiba ya Jamhuri ya Muungano haitambui wabunge wa aina hii: Katiba inataja wabunge wa aina tatu tu – wale wa kuchaguliwa, kuteuliwa na mwanasheria mkuu wa serikali ambaye anaingia kwa wadhifa wake.

Kwa mfano, ibara ya 66 (1) inasema, “…kutakuwa na wabunge waliochaguliwa kuwakilisha majimbo ya uchaguzi; wabunge wanawake, watakaochaguliwa na vyama vya siasa vinavyowakilishwa bungeni, kwa mujibu wa ibara ya78, na kwa kuzingatia masharti ya uwiano wa uwakilishi baina ya vyama hivyo.”

Aidha, “kutakuwa na wabunge watano waliochaguliwa na Baraza la Wawakilishi kutoka miongoni mwa wajumbe wake; mwanasheria mkuu wa serikali; na wabunge wasiozidi kumi walioteuliwa na rais kwa mujibu wa ibara ya 67.”

Kimsingi wabunge wa kuchaguliwa wanaangukia katika makundi makubwa matatu: Waliochaguliwa majimboni, waliochaguliwa kwa uwiano wa uwakilishi wa vyama (katika viti maalum) na wanaochaguliwa na baraza la wawakilishi.

Wabunge wa kuteuliwa ni wale kumi tu, ambao rais anaweza kuwateua. Hivyo, hakuna mbunge anayeweza kuingia bungeni bila ya kuchaguliwa au kuteuliwa.

Kuruhusu watu wasio na sifa hizi kuingia bungeni kwa kisingizio cha “kupita bila kupigwa,” ni kwenda kinyume cha katiba.

Si hivyo tu: Kitendo hicho kinadhoofisha demokrasia na kinapora haki ya wananchi ya kuchagua viongozi wanaowataka.

Wala hakuna mashaka kwamba baadhi ya wanaojitapa kuwa wamepita bila kupigwa, wametumia ulaghai, vitisho na hadaa kufanikisha “ubunge wa dezo.” Wanafahamika hata kwa majina.

Kutokana na ukweli huo, wale wanaosema “wamepita bila kupingwa” hawezi kuwa wabunge, kwa kuwa wananchi hawakupewa nafasi ya kupinga kura ya kuwakubali au kuwakataa.

Kwanza, Katiba katika Ibara ya 63:2 inasema, “…Bunge ndicho kitakuwa chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano kitakachokuwa na madaraka, kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri serikali na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake….”

Kama Bunge ndicho chombo kikuu cha Jamhuri “kwa niaba ya wananchi” wabunge hawa watakuwa wanamwakilisha nani?

Pili, Ibara ya 21 ya Katiba inatoa haki kwa wananchi kushiriki katika utawala wa nchi yao moja kwa moja au “kwa kupitia wawakilishi waliochaguliwa na wananchi kwa hiari yao.”

Je, kwa kukubali watu waliosimama peke yao kuwa ndio wawe “wawakilishi” huko si uvunjaji mkubwa wa haki na mwanzo wa kufungulia “watu wasiowaadilifu” kushika madaraka bila ya kuchaguliwa?

Wala katiba hairuhusu kuwapo kwa wawakilishi wa wananachi wanaopita bila kuchaguliwa. Ni lazima kwa namna moja au nyingine wawakilishi wa wananchi wachaguliwe.

Tatu, hatua ya kuruhusu watu wapate ubunge “kwa njia ya mkato” kunaweza kuingiza taifa katika matatizo. Ni kwa sababu, mfumo huo unaweza kuingiza watu bungeni kwa njia ya hila, hadaa na ghiriba kama ambavyo tayari imetokea sasa.

Nne, kuruhusu watu kuingia bungeni bila kuchaguliwa, kuna wafanya wahusika kukosa uhalali wa kuitwa “wawakilishi wa wananchi.” Hivyo basi, taifa litakuwa linaruhusu utawala wa kujipachika na siyo wa kuchagulika.

Tano, uchaguzi wa namna yoyote ile unawapa wananchi fursa kukataa; demokrasia hujengwa pale ambapo nafasi ya kukataa inakuwepo na kutumika.

Kuruhusu kivuli cha “kupita bila kupingwa,” kunaondoa haki hiyo ya kidemokrasia – ile kupigakura – hata kama kwa kukataa. Ni lazima nafasi ya kukataa (dissent) itolewe.

Hivyo, kuingia bungeni kwa njia hii, kunaondoa utaratibu wa demokrasia unaotoa uhuru kwa wananchi kutoa sauti yao.

Sita, hata katika mfumo wa chama kimoja wananchi walipata nafasi ya kuchagua vingozi wao – hata kwa kupigakura za ndiyo au hapana.

Hata katika kiti cha urais, iwapo mgombea anakuwa mmoja, katiba inataka apigiwe kura za ndiyo au hapana.

Sasa kama haya yote yanafanyika kwa kiti cha urais na yalifanyika hata katika mfumo wa chama kimoja, kwamba mgombea anapobaki pekee yake anaopigiwa kura za ndiyo au hapana, iweje taifa hili litumbukizwe katika matatizo sasa kwa kuruhusu “wabunge wa mizengwe?”

Hata wakati wa uhai wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, pamoja na kwamba alikuwa na uhakika wa kupita bila kupigwa, lakini bado wananchi walipewa nafasi ya kupigakura.

Hata mara moja, haikuwahi kutokea, Mwalimu kutangazwa mshindi bila kupigiwa kura.

Saba, mchakato ambao umewaacha wabunge wateule kuwa peke yao haukuwa na lengo la kutoa wabunge, bali “wagombea ubunge.”

Hivyo, kwa usahihi hawa wanatakiwa kuwa ni "wagombea pekee" na siyo "waliopita bila kupingwa." Hapa bado hawajipigiwa kura.

Nane, kinachotokea sasa, ni kutafsiri kura za maoni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa kura za uchaguzi. Kwamba, kwa vile mgombea ameshinda kura za maoni, basi sasa ni mbunge anayepita bila kupigiwa kura. Hii si sahihi.

Kura za maoni za watu wa chama kimoja hata hazipaswi na hazitakiwa kuchukuliwa kama ni kura za wananchi wote. Wana CCM walipopiga kura walikuwa hawachagui mbunge, walikuwa wanachagua mgombea.

Hivyo basi, si haki kwa NEC kutoa mamlaka kwa watu wa chama kimoja kutoa uamuzi wa mwisho wa nani anakuwa mbunge kabla ya kura kupigwa. Ni lazima wagombea waletwe kwa wananchi ili wapate nafasi ya kusikika uamuzi wao.

Tisa, kwa makusudi kabisa sijagusia suala la sheria ya uchaguzi au hata taratibu ambazo zimeruhusu hali hii kuendelea.

Ni kwa sababu, ibara ya 66 ya Katiba haitoi mwanya au nafasi hata chembe ya kupitisha sheria itakayosababisha watu waingie bungeni bila kuchaguliwa.

Katiba inasema wazi, “ni lazima wabunge wanaotoka majimboni wawe ni "wale waliochaguliwa" tena kama inavyosema katika sehemu nyingine kuwa "kwa hiari."

Kutokana na hali hiyo, ni lazima watu ambao wamepitia bila kupigwa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) iweke utaratibu ili wananchi wawapigie kura ili kupata uhalali wa wao kuingia bungeni.

Hili ni muhimu kwa maslahi ya sasa na siku zijazo. Tusijiruhusu watu kuhoji mahakamani uhalali wa wabunge hawa.

Kwa mfano, iwapo Kikwete atashinda uchaguzi na kuamua kumrejesha tena katika kiti chake Mizengo Pinda, wakati huku akiwa mbunge aliyepita bila kupigiwa kura, huku katiba ikisema waziri mkuu sharti atokane na wabunge wa kuchaguliwa, nani ataweza kunyooshea vidole wananchi?

Ni kwa njia hii tu, ndipo tunapoweza kuminya mianya ya wananchi kwenda mahakamani kutafuta tafsiri ya katiba. Ni kwa njia hii, tunaweza kuzuia wabunge wetu kupoteza ubunge wao na hata ulaji mwingine utakaofuata baada ya uchaguzi.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: