Wabunge wapimwe akili, tuanze meza kuu


Nyaronyo Kicheere's picture

Na Nyaronyo Kicheere - Imechapwa 03 August 2011

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki
Spika wa Bunge, Anne Makinda

MAKADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), waliovikwa majoho ya uspika, naibu spika na uenyekiti wa Bunge wameamua kuligeuza bunge la Jamhuri kuwa jumba la sinema. Hao ni Job Ndugai (naibu spika), na wenyeviti wa Bunge, George Simbachawene, Sylvester Mabumba na Jenesta Mhagama.

Wote hawa kwa namna moja au nyingine wanaendesha Bunge kwa upendeleo. Mifano ipo na tena ni mingi.

Kwa mfano, Ndugai, Simbachawene, Mabumba na Mhagama wamekuwa wakipindisha kanuni za kuendesha Bunge kulinda serikali na wabunge kutoka CCM.

Hili tayari limedhihirika wiki iliyopita baada ya Mabumba kuamuru kutolewa nje kwa mbunge wa CHADEMA katika jimbo la Nyamagana, mkoani Mwanza, Ezekiel Wenje.

Naye, Ndugai siku moja baada ya Mabumba kumtoa nje ya ukumbi wa Bunge Wenje, aliamuru kutolewa nje ya ukumbi wa Bunge, wabunge wengine watatu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Godbless Lema (Arusha mjini), Tundu Lissu (Singida Mashariki) na Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini).

Kanuni na taratibu mbovu za kuendesha Bunge ziliwekwa na wabunge wa CCM ili kuhakikisha uozo unapitishwa bila pingamizi. Mambo mengi mabaya yanapitishwa kwa kisingizio kuwa kanuni haziruhusu.

Kwa upande Simbachawene, ambaye mara nyingi huendesha Bunge kutokana na nafasi yake ya uenyekiti na anayejiita mwanasheria mbali na kubana wabunge wa upinzani, Alhamisi iliyopita, akichangia hotuba ya makadario ya bajeti ya wizara ya mambo ya ndani ya nchi, alinukuliwa akisema, “Law and order (watu kufuata sheria na kuwa watulivu) ni pamoja na kutii amri ya polisi na usipotii unawashwa.”

Kwangu mimi kauli na matendo ya Simbachawene nayafananisha na majigambo ya dereva wa mkurugenzi wa kampuni anayejiona yeye ni mkurugenzi wa madereva wote wa kampuni au vituko vya mke wa rais yeyote anayedhani naye ni rais wa wanawake wote nchini humo.

Katika msimamo huu wa wanaong’ang’ania kuandamana na kupinga amri za polisi “wawashwe” au kwa lugha rahisi wapigwe risasi, Simbachawene hayuko peke yake.

Yalekea kada huyu wa CCM aliyedai kuwa ni mwanasheria hajui kwamba popote pale duniani watu hufuata sheria na kutii amri halali tu, na siyo mradi amri ya mkubwa.

Law and order inafanya kazi pale penye mfumo sahihi wa madaraka na kuwepo sheria zisizo kandamizi. Katika mfumo ambao makamanda wa jeshi na mapolisi wastaafu wanagombea ubunge kupitia CCM huwezi kusema wanatekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria kwa vyama vya upinzani.

Inaonekana Simbachawene amesahau kidogo. Waliokuwa wanawalazimisha raia weusi nchini Afrika Kusini wafuate sheria na kuwa watulivu, hawakuwa na katiba halali kwa  mtazamo wao? Kama ilikuwapo, mbona chama cha African National Congress (ANC) kiliipinga kwa udi na uvumba hadi uhuru wa kweli ukapatikana?

Je, CCM na serikali yake wanaokejeli wapinzani leo hii, hawajui kuwa sheria za makaburu zilikuwa halali kwa mujibu wa katiba yao?

Je, kama Nelson Mandelea na wapigania uhuru wenzake akiwamo Jacob Zuma, Thabo Mbeki, Walter Sisulu, Steve Biko na Chris Hani wangetii sheria hizo na amri zake zilizosheheni ubaguzi, Afrika Kusini ingeondokana na makucha ya utawala wa wachache?

Jingine ambalo Simbachawene anapaswa kuliangalia kama mfano mdogo, ni kuuawa kwa raia watatu mjini Arusha wakati wa maandamano yalioitishwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Kwamba polisi walioua raia wanadai kutii amri ya wakubwa.

Naomba radhi polisi wanijibu swali lifuatalo: Hivi kamanda akitoa amri kwamba – Nyumaa geuka, shusha suruali…polisi watatekeleza amri hiyo? Hawawezi. Ni kwa sababu, amri hii ni ya mkubwa, lakini si amri halali.

Hata Simbachawene hawezi kutekeleza amari kama hiyo, pale ambapo wabunge wenzake watakapomuamuru amri ambazo si halali.

Askari polisi hawezi kumpiga risasi raia kwa kisingizio cha kutii amri ya bosi wake. Je, askari anayelinda zamu ikulu anaweza kuachia lindo kwa kuamriwa na kamanda wake atoke kwenye eneo hilo, lakini bila kuwepo mtu wa kuchukua nafasi yake?

Maelezo haya yanaeleza sababu muhimu kwa nini Watanzania wanavyotakiwa kuzikataa sheria na amri zisizo halali. Wala kwa kufanya hivyo, huwezi ukasema ni uchochezi kama inavyotaka serikali kupitia kwa mwanasheria wake mkuu, Jaji Frederick Werema inavyotaka ieleweke.

Werema ambaye ni miongoni mwa walioonyesha sinema ya bure bungeni kwa hatua yake ya kutaka kutungwa maji kwenye kinu kutokana na kudai eti yeye na wenzake serikalini wana mpango kutunga sheria za kudhibiti maandamano ya CHADEMA!

Tangu lini sheria zikatungwa kuwalenga watu fulani, chama fulani au kikundi fulani cha watu? Au Werema hanakumbukumbu?

Utawala wa Makaburu nchini Afrika Kusini walisimamia sheria za kibaguzi, baadhi ya sheria hizo zinaendelea kuwatesa hadi sasa.

Walowezi wa Zimbabwe waliotunga sheria kulinda wakulima Wakizungu waliowaua Wafrika. Lakini mara baada ya uhuru walinzi wa mmoja wa mawaziri wa serikali ya Robert Mugabe, Edgar Tekere, wakamuua mkulima wa Kizungu. Walipokamatwa na kufikishwa mahakamani, walishinda kesi iile walitumia sheria ileile iliyotungwa kwa walowezi kujikomboa.

Hivyo basi, naweza kutabiri kuwa katika mazingira ya sasa, sheria anayotaka Werema kuileta bungeni, ikatumika kudhibiti maandamano ya CCM mwaka 2016 pale watakapokuwa tayari wametupwa nje ya utawala.

Mhagama ndiye aliyemruhusu mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde kuomba  mwongozo wa kudai kuletwe wataalamu wa akili ili wabunge wapimwe akili. Kauli ya Lusinde ilifuatia mchango wa mbunge wa CHADEMA, Chiku Abwao ambaye alionyesha jinsi gani wabunge wa CCM walivyoshindwa kutofautisha maana ya Bunge la mfumo wa vyama vingi.

Kimsingi, pamoja na Lusinde hakusema anataka wabunge wapi wapimwe akili, lakini bila shaka alilenga wabunge wa upinzani. Je, ingekuwaje kama kauli hiyo ingetolewa na mbunge wa upinzani? Angefukuzwa bungeni.

Binafsi, nakubaliana na Lusinde kwamba wabunge wapimwe akili, lakini tuanzie na meza kuu. Tuanze na wale makada wa CCM waliovaa majoho ya uspika wanaozuia mijadala na kukwamisha hoja zenye tija kwa nchi. Hao ndiyo wapimwe kwanza.

Makada wa CCM wanaofukuza mbunge anayetaka kujadili jambo la dharura kama samaki wenye sumu eti kwa sababu walidhani anataka kueneleza malumbano pia wapimwe.

Mbunge wa CCM anayewafuata wabunge wa CHADEMA nje ya ukumbi wa Bunge na kudai kuwa “wanafanya mambo ya kitoto” naye apimwe akili. Pia wabunge wote na mawaziri wanaokataa uchunguzi wa vifo vya raia waliokufa mikononi mwa polisi nao wapimwe akili.

Watu wanaodai eti kutamka kuwa polisi wameua raia Nyamongo ni uchochezi wapimwe akili. Kusema polisi wameua Arusha na Mbozi si uchochezi na mwaziri na wabunge wanaopinga wakati watu wamekufa kweli wapimwe akili!

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: