Wabunge watuma salamu kwa JK


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 25 April 2012

Printer-friendly version

LINI serikali ya Rais Jakaya Kikwete itavunjika ni suala tu la muda! Mkakati wa wabunge kutaka kumng’oa madarakani Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kutokana na ulegevu wa mawaziri ni salamu kwake.

Wabunge wamechoshwa na falsafa ya kuchelewesha uamuzi ili watu wasahau au upepo mbaya upite. Sasa wameamua kuchukua hatua hiyo wakijua Rais Kikwete hufanya maamuzi baada ya kuwepo shinikizo.

Hadi juzi, wabunge 73, sawa na asilimia 20 ya wabunge wote walitia saini kutekeleza matakwa ya Ibara ya 53A ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano na kifungu cha 133 cha kanuni za Bunge.

Ikiwa wakati wa kupiga kura hoja hiyo itaungwa mkono na asilimia 51 ya wabunge wote, Pinda atakuwa waziri mkuu wa kwanza kuondolewa kutokana na wabunge kutokuwa na imani naye. Lakini atakuwa wa pili katika serikali hii kuondolewa kwa shinikizo la wabunge.

Wabunge wanasema hawana nongwa na Pinda bali ni kumwajibisha kutokana na udhaifu wa mawaziri ambao kikatiba anapaswa kuwasimamia. Wanajua kuwa Pinda hakuteua mawaziri, lakini wanajua kuwa wakimwondoa masikio ya Rais Kikwete yatafunguka.

Kwa hiyo, anayetafutwa katika kadhia hii si Pinda ila Rais Kikwete ambaye alichaguliwa na Watanzania wote na akakabidhiwa nchi alinde raslimali zake kwa faida ya Watanzania siyo mawaziri wachache fisadi.

Rais Kikwete asipofukuza mawaziri kumwokoa Pinda atakuwa anamtosa kama alivyofanya mwaka 2008 kwa Lowassa ilipoibuka kashfa ya Richmond. Hakika hilo likitokea, rais hawezi kupata amani moyoni.

Utetezi wa dakika saba tu alioutoa kwenye mkutano wa Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwishoni mwa mwaka jana, Lowassa alisema Rais Kikwete anajua ukweli kuhusu Richmond ingawa yeye Lowassa ndiye aliyebebeshwa lawama.

Lowassa alikuwa anamaanisha ametoswa na swahiba wake. Kama hivyo ndivyo, haitashangaza kuona Pinda anatoswa kama katika sakata la Katibu mkuu wa Nishati na Madini, David Jairo.

Pinda hapendi ufisadi; alipoteuliwa kuwa waziri mkuu mwaka 2008 kuchukua nafasi ya Lowassa alidhani wote walikuwa na nia thabiti kupambana nao lakini amekuja kujiona yuko pekee; akarudi nyuma.

Hebu jiulize, rais ndiye anateua mawaziri, wakurugenzi wa halmashauri na viongozi wengine, anashindwaje kuwafuta kazi pale wanapobainika ni wezi, wabadhirifu, mafisadi au wabovu?

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ametoa ripoti inayoonyesha ufisadi wa hali ya juu katika wizara, idara za serikali na halmashauri, kwa nini rais hachukui hatua? Kwa nini hajamfuta kazi hata waziri mmoja?

Rais ana maslahi gani na mawaziri fisadi maana tangu alipoingia madarakani mwaka 2005 hajamfuta kazi hata mmoja japokuwa haachi kulia eti kwenye halmashauri kuna mchwa. Hajauona au hajanunua dawa? Jibu rahisi hapa tatizo si Pinda, ila mfumo wa kifisadi uliolelewa na Serikali ya CCM.

Mwaka 2007 kabla Pinda hajateuliwa kuwa waziri mkuu  viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani na wananchi walimsaidia Rais Kikwete kutaja mawaziri na viongozi watuhumiwa wa ufisadi na aina ya ufisadi walioufanya, lakini hakuchukua hatua.Alipuuza akisema ni kelele za mlango ambazo hazimzuii mwenye nyumba kulala.

Hakufika mbali. Februari 2008 alilazimika kuunda upya na kupunguza ukubwa wa Baraza la Mawaziri. Hiyo ilikuja baada ya serikali yake kuvunjika bungeni kufuatia ripoti ya Kamati Teule ya Bunge chini ya uenyekiti wa Dk. Harrison Mwakyembe (Mbunge wa Kyela – CCM) kutaja waliohusika katika ufisadi kupitia kampuni feki ya kufua umeme ya Richmond.

Lowassa alijiuzulu nafasi ya uwaziri mkuu pamoja na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi na wa Afrika Mashariki Dk. Ibrahim Msabaha kutokana na kuhusishwa na kashfa ya Richmond. Rais Kikwete alitakiwa kuwachukulia hatua watendaji wengine waliohusika lakini aliwaacha.

Rais aliweka kinga kwa watendaji wengine wasiadhibiwe kwa vile kashfa ile ilikuwa inaishona ikulu. Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri lililobariki Richmond alikuwa rais mwenyewe.

Ikulu ndiyo ilihusika kuhamisha mkataba wa Richmond na kuipa Dowans na baadaye ikahamishia kwa Symbion Power. Pinda amekuwa shuhuda tu wa madudu haya.

Nafasi ya Rais Kikwete kukingia kifua watuhumiwa wa ufisadi ilifichuliwa na mtandao wa Wikileaks uliomkariri bosi wa Takukuru, Dk. Edward Hoseah akilalamika kwamba ameambiwa na bosi wake asiwachunguze watu maarufu. Miongoni mwao ni Kampuni ya Kagoda iliyochotewa Sh. 40 bilioni kati ya Sh. 133 bilioni zilizotafunwa kwa msaada wa serikali.

Rais Kikwete mwenyewe aliwaita watuhumiwa wa wizi wa fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) akanywa nao chai ikulu akawaomba warudishe fedha na akawasamehe.

Katiba ya Jamhuri Ibara ya 45 inampa Rais mamlaka ya kusamehe mtu yeyote aliyepatikana na hatia mbele ya mahakama, lakini si anayetuhumiwa. Kama mawaziri fisadi wanakingiwa kifua na mtu aliyekabidhiwa nchi, Pinda ana ubavu gani kufanya maamuzi yanayomuudhi bosi wake?

Mwaka jana, wabunge walichachamaa na kumtajia Rais baadhi ya mawaziri dhaifu ili wapumzishwe, wakiwemo Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkullo na wa Nishati na Madini, William Ngeleja, lakini Rais alipuuza. Hadi leo Mkullo ameshindwa kutaja kampuni zilizopewa ‘Stimulus Package’ kiasi cha Sh. 1.7 trilioni; hata Spika Anne Makinda aliposhinikiza katika vikao vya Januari 2012, Mkullo amegoma. Je, kuna nini?

Katika kipindi cha bajeti Ngeleja aliwasilisha makadirio ya ovyo huku wizara ikiwa imeandaa ‘kiziba midomo’ kwa baadhi ya wabunge. Kashfa ikaibuka ya wizara kupitia kwa Katibu mkuu, David Jairo kukusanya fedha za kuhonga, kufanya sherehe na posho kwa watendaji.

Pinda akamsimamisha Jairo lakini ikulu ikatengua; siku iliyofuata akarudishwa likizo. Ikulu ikamtuma CAG ili amsafishe, haraka akarejeshwa kazini, lakini baada ya wabunge kuchachamaa akapelekwa ‘likizo’ nyingine.

Kamati Teule ya Bunge chini ya Injinia Ramo Makani ilipofanya ukaguzi ilitoa ripoti iliyomshona siyo Jairo tu bali pia Ngeleja, lakini ikulu imekinga kifua.

Kipindi cha Bajeti yakaibuliwa madudu mengi kama ya utoroshwaji wa nyara za serikali na ujenzi wa mahoteli maeneo yasiyotakiwa katika hifadhi ya Ngorongoro. Mwenyekiti wa bodi ya hifadhi hiyo akatajwa wazi wazi lakini serikali imekaa kimya.

Kumbuka mara baada ya kuteuliwa kuwa waziri mkuu mwaka 2008 Pinda alimfungia kazi Mzee wa Vijisenti, Andrew Chenge akajiuzulu uwaziri wa miundombinu na akang’oa watendaji Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo na akatangaza wanaoua maalbino wauawe. Tujiulize, nani alipunguza kasi hiyo?

Wabunge wanajua udhaifu wa Pinda na utendaji kazi wake, hivyo watapiga kura siyo kumwadhibu ila kumpa salamu Rais Kikwete kwamba anayetafutwa ni yeye. “Mwenzako akinyolewa wewe tia maji kichwa,” hatua inayofuata itakuwa ya kutumia Ibara ya 46A kupiga kura ya kutokuwa na imani rais.

0789 383 979
0
No votes yet