Wachimba madini wadogo: Serikali inapigana na wananchi


Editha Majura's picture

Na Editha Majura - Imechapwa 23 December 2009

Printer-friendly version

WAKILI wa Mahakama Kuu, Tundu Lissu amesema anatafsiri mahusiano ya serikali na wachimbaji wadogo wa madini nchini kama vita vya serikali dhidi ya wananchi wake.

Amesema sheria ya uwekezaji katika uchimbaji madini ya mwaka 1998 haikujadiliwa kwa mapana na mamlaka husika na kwamba sehemu ya sheria hiyo inaagiza wachimbaji wadogo kuondoshwa kwenye maeneo ambayo wawekezaji wakubwa wanakusudia kuwekeza.

Hali hiyo, amesema imesababisha madhila makubwa kwa raia ambao ni wachimbaji wadogo. Aidha, imesababisha balaa kubwa kwa wananchi wanaoishi karibu na machimbo ya madini.

Ingawa vita hivyo ni vya kimya kimya, anasema Lissu, hakuna mtu mwenye akili timamu anayeweza kukanusha kauli hiyo. Anatetea hoja hiyo kwa maelezo kwamba mauaji yanayotokea sehemu mbalimbali za machimbo ya madini nchini, ni ushahidi wa kutosha.

Anayataja baadhi ya machimbo yaliyoweka historia ya kupoteza uhai wa wananchi kuwa ni pamoja na Bulyanhulu na mgodi wa North Mara uliopo Tarime ambao unamilikiwa na kampuni ya uchimbaji madini ya Barrick.

Lissu alikuwa akiongea na wahariri na waandishi wa habari wa gazeti la MwanaHALISI, Ijumaa iliyopita jijini Dar es Salaam, juu ya utajiri wa madini na adha za wananchi.

Anasema endapo sheria zilizowekwa ili kutoa mwongozo wa namna ya kulipa fidia za wanaohamishwa kupisha uwekezaji ingezingatiwa, hakuna kilio hata kimoja ambacho kingesikika kutokana na uhamisho huo.

Lissu alianza kwa kuuliza: Je, madini yanayopatikana ndani ya mipaka ya Tanzania ni mali yetu? Tunanufaika nayo? Tunayamiliki? Ndipo akafuatiza majibu, moja baada ya jingine.

Lissu ni mwanaharakati wa haki za binadamu na mazingira na amejikita katika eneo la madini na manufaa yake kwa jamii ya Tanzania. Ni mkurugenzi wa asasi ya LEAT inayojishughulisha na utetezi katika maeneo ya ardhi, mazingira na madini.

Baadhi ya wananchi na wanaharakati humwita mmisionari wa madini kutokana na uzoefu alionao katika kushughulikia masuala mbalimbali ya madini nchini. Amefanya shughuli hizo kwa miaka isiyopungua10 sasa.

“Kufuatia dhana kwamba madini yanapatikana kwenye ardhi, ndani ya mipaka ya nchi yetu, sina shaka kwamba ni mali yetu. Hata hivyo, hatunufaiki nayo wala hatuyamiliki,” amesema Lissu.

Hali hiyo, anasema inatokana na sheria mbovu pamoja na anachokiita “uhuni wa watawala.”

Anapozungumzia matatizo ya kisheria katika sekta ya madini nchini kihistoria, anasema enzi za utawala wa kikoloni ziliwekwa sheria ambazo angalau zililinda maliasili za nchi.

Sehemu kubwa ya sheria hizo sasa zimerekebishwa na kutoa mianya kwa wenye nia ya kutumia madini ya Tanzania kujinufaisha.

Amesema sheria imebeba tu dhana ya “madini yetu,” huku wanaoyamiliki na kuyafaidi wakiwa wachache wakishirikiana na wakuja kutoka nchi za nje.

Sheria ya madini iliyotungwa na utawala wa Kijerumani Mwaka 1895 ilidhibiti matumizi ya madini na ardhi, rasilimali hizo zilikuwa mali ya rais wa Ujerumani, alisema.

Waingereza nao waliiendeleza sheria hiyo kabla ya utaratibu wa utaifishaji ambapo ardhi na madini vilielezwa kuwa mali ya umma.

Kitendo hicho kinatafsiriwa na Lissu kuwa ni mpango wa kunyang’anya miliki ya wananchi. Kwa mfumo huo, ili mtu achimbe madini sharti apate leseni halali kisheria kutoka serikalini.

Hivi sasa, anasema wachimbaji wakubwa wa madini au wenye leseni za kushughulikia madini na vito vya thamani ni watu kutoka nje ya nchi.

“Njia pekee itakayowezesha Watanzania kunufaika na madini yao ni kuhakikisha miliki yake inarejeshwa kwao.” Anasema Lissu na kuongeza kuwa miongoni mwa sababu zinazolikosesha taifa fursa ya kunufaika na madini yake ni sheria zisizofaa.

Marekebisho ya Sheria ya Madini yaliyofanywa kati ya mwaka 1997 na 1998 yanaelezwa na Lissu kwamba yaliweka kando maslahi ya taifa huku maslahi ya wawekezaji wakubwa yakizingatiwa.

Anasema tangu mwaka 1990 Benki ya Dunia (WB), Taasisi za Fedha za Kimataifa (IMF), wanadiplomasia, wasomi na serikali ambazo makampuni yake yanachimba madini nchini, pamoja na kampuni zenyewe, wamekuwa wakishabikia marekebisho hayo ya sheria.

Ushabiki huo unaelezwa kuwa haukuishia kwenye kuzungumza, bali hata kwa kushurutisha. Alisema madai hayo yanathibitishwa na historia aliyoieleza kuwa tokea mwaka 1993 WB ilianzisha miradi mbalimbali iliyolenga kufanikisha marekebisho ya sheria ya madini nchini.

Mradi wa Maendeleo ya Sekta ya Madini nchini, unatajwa na Lissu kuwa umewezeshwa na WB kwa kila kitu na kwamba benki hiyo imekwenda mbali katika hilo, kwa kutoa hata wataalamu wa kufanya kazi katika mradi huo.

Mwaka 1992, WB ilitoa chapisho lililoelezea mkakati wake kuhusu madini Barani Afrika, lengo likiwa kuweka utaratibu mpya wa kisera na kisheria kuhakikisha milango ya uwekezaji katika sekta ya madini inafunguliwa kwa mataifa ya nje.

Chapisho hilo lilieleza lengo la mkakati huo kuwa ni kuweka utaratibu mpya wa kisera na kisheria ili kuhakikisha milango ya uwekezaji ndani ya sekta ya madini, inafunguliwa kwa mataifa ya nje.

Matokeo ya miradi iliyofadhiliwa na benki hiyo yanaelezwa kuwa ni Sera ya Taifa ya Madini kufanyiwa marekebisho, Sheria ya fedha (kodi) Na. 27 pamoja na Sheria ya Uwekezaji Na. 26.

“Ngonjera” za kisiasa zilizotumika kupamba marekebisho hayo zilieleza kuwa ni katika kuwezesha ongezeko la wawekezaji wakubwa kwenye sekta hiyo, ingawa Lissu anasema historia ya madini nchini inatofautiana na madai hayo.

Anasema kihistoria kizuizi cha wawekezaji wakubwa katika sekta hiyo kuwekeza kwa wingi kilitokana na kuanguka kwa uchumi duniani mwaka 1929.

Sababu nyingine inaelezwa na Lissu kuwa ni sheria madhubuti za kikoloni ambazo zilidhibiti matumizi mabaya ya maliasili za taifa. Hali hiyo inaelezwa kusababisha shughuli za uchimbaji madini kutawaliwa na wachimbaji wadogo.

Anabainisha kuwa sheria hizo ziliendelezwa na utawala wa serikali ya awamu ya kwanza, chini ya Mwalimu Julius Nyerere, na sera ya Siasa za Ujamaa na Kujitegemea alizozitaja kama “uchumi dola.”

Anasema historia ya madini nchini inaeleza kuwa kati ya 1930 na 1970, bei ya dhahabu ilikuwa chini sana. Nchi za Afrika Kusini na Ghana ndizo zinazotajwa kuwa zilikuwa zikiongoza katika shughuli za uchimbaji madini.

Almasi iligunduliwa na kampuni ya kigeni mwaka 1947. Bei yake inaelezwa kuwa ilikuwa kubwa tofauti na dhahabu kwa sababu almasi hutumiwa pia kwenye shughuli anuai za viwandani.

Madini hayo yalitungiwa sheria maalumu na serikali ya kikoloni. Iliamuliwa kuwa zaidi ya nusu ya biashara ya uchimbaji madini hayo imilikiwe na serikali.

Sharti hilo linaelezwa na Lissu kuwa lilikuwa gumu lakini lenye maslahi na malengo chanya katika kudhibiti matumizi ya madini.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: