Wafanyakazi wanastahili wanachodai


editor's picture

Na editor - Imechapwa 04 May 2011

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

MPAKA wakati inaandaa bajeti yake ya mwaka mpya wa fedha wa 2011/2012, haina sababu hata moja au kisingizio cha kukataa madai ya wafanyakazi nchini ya kutaka maslahi bora.

Serikali imeshindwa kujibu kwa ufasaha hoja mbalimbali za matumizi mabaya ya fedha za kodi na vile inavyopuuza ushauri wa kitaalamu wa kufuta misamaha holela ya kodi kwa wawekezaji wageni.

Kuna ushahidi usio shaka kwamba ndani ya serikali kunafanywa matumizi makubwa kupindukia mpaka na hakujaonekana dhamira hasa ya serikali kukomesha uovu huu.

Serikali imeshindwa kurekebisha dosari katika namna inavyotoa misamaha ya kodi; inasita kupanua wigo wa vyanzo vya mapato; inazidi kutumia fedha nyingi kwa mambo ya anasa ikiwemo kugharamia warsha, makongamano, mikutano na semina.

Pia serikali haijaonyesha kuchoka kununua magari ya kifahari; haijapunguza ukubwa wa misafara ya viongozi wa kitaifa wanapofanya ziara ndani na nje ya nchi; na haijabana wafujaji na wezi wa mapato ya serikali kwa kiwango kinachoridhisha.

Takwimu zinaonyesha katika kanda ya Afrika Mashariki, Tanzania inaongoza kwa kutoa misamaha holela ya kodi na hivyo kusababisha ikose mapato ya karibu Sh. 6 trilioni katika miaka 10 kuanzia mwaka 2000. Ripoti zinaonyesha ingepunguza misamaha ya kodi, ingeongeza mapato ya Sh. 600 bilioni kila mwaka.

Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi nchini (TUCTA) linataja takwimu zinaonyesha matumizi yasiyo lazima kwa mwaka wa fedha 2009/2010 yaligharimu taifa Sh. 530 bilioni na Sh. 537 bilioni kwa mwaka unaokwisha wa 2010/2011.

Madai ya wafanyakazi kutaka kuongezewa maslahi na mazingira bora ya kazi, siyo tu yanapaswa kuzingatiwa, bali pia lazima yatekelezwe kwa vitendo kwani ni ya haki.

Tunaiona hatari mbele iwapo serikali haitabadilisha mwenendo wake katika matumizi. Mara nyingi wafanyakazi wanapochoka na kukata tamaa, huungwa mkono na umma hasa unapokuwepo ushahidi wa fedha zinazoibwa serikalini kutajirisha viongozi.

Tatizo ni kwamba kadiri serikali inavyoruhusu matumizi mabaya ya fedha za wananchi, ndivyo inavyotilia mbolea kiwango cha ukuaji wa pengo la kipato kati ya matajiri na masikini.

Pengo hili husababisha wananchi kuchukia viongozi wao na hatimaye kuchochea machafuko kama Watanzania wanavyoshuhudia nchi mbalimbali duniani zikiwemo za Afrika.

Tunawasihi viongozi wakuu wa serikali kujitazama upya kuhusu matatizo haya kwani kutoyatafutia dawa ya kudumu, kunasababisha hatari kwao wenyewe.

0
No votes yet