Wafugaji wa Loliondo hawana kosa


Onesmo Olengurumwa's picture

Na Onesmo Olengurumwa - Imechapwa 05 January 2011

Printer-friendly version

WAKAZI wa Ngororo, mkoani Arusha wako hoi kiuchumi. Wapo wanaosema, “Kesho hatujui itakuwaje.” Wengine tayari wamekata tamaa ya maisha wao na familia zao.

Kisa: Ni serikali kutaka kufurahisha mwekezaji – kampuni ya Ortello Business Corpotion (OBC)- ambayo inadaiwa kumilikiwa na mtawala wa Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu (UAF).

Serikali kupitia kampuni hiyo inatenda mambo mawili. Kwanza, inakula njama ya kutaka kufuta historia ya wananchi hawa, pamoja na mazingira yao.

Pili, inabariki uharibifu wa mandhari tulivu yaliyozoeleka na wenyeji wa maeneo ya pori la hifadhi ya wanyamapori la Loliondo.

Katika siku za hivi karibuni kumeibuka hata upotoshaji unaofanywa na baadhi ya vyombo vya habari na waandishi wa habari mmojammoja wanaotekeleza matakwa ya muwekezaji.

Kwamba wafugaji wa Ngorongoro wanaharibu mazingira kwa kuwaruhusu watoto wao kuchunga ng’ombe, ilihali baba zao wakichoma nyama na kunywa pombe.

Historia ya Ngorongoro ilianza miaka 60 iliyopita ambapo serikali ya kikoloni iliwaomba wananchi wa Ngorongoro waliokuwa wakiishi maeneo ya Serengeti ambayo kwa sasa ni Hifadhi ya Taifa ya Wanyamapori, kuhamia eneo la bonde la Crater na Loliondo.

Kwa mujibu wa wazee wa enzi hizo, wakati wakazi hao walipotakiwa kuhama waliahidiwa kuwa wale watakaokubali kwenda huko hawatabughudhiwa tena.

Serikali ya kikoloni iliahidiwa wananchi hao kuwapatia maendeleo mengi kupitia mchango utokanao na maliasili iliyopo.

Lakini hali ilivyo sasa ni tofauti. Kila kukicha wanaendelea kufukuzwa na kurudidhwa nyuma ili hatimaye watoke nje kabisa ya maeneo hayo.

Hakuna anayejali njia za kinguvu zinazotumika kuwaondoa walikozoea kuishi na kulisha mifugo yao. Hakuna anayejali wapi wananchi hao wanasukumwa kwenda kuishi.

Yote hayo si muhimu kwao. Wanachokijua wale wachache wanaowalazimisha kuondoka walipozoea, ni kupatikana nafasi kwa wenye fedha kujitanua zaidi na kufaidi raslimali wasiyoijua ilikuaje kabla ya kufika kwao.

Ukweli ni kwamba wananchi hawana chembe ya maisha bora. Zaidi ya asilimia 90 ya jamii ya watu wanaoishi karibu na pori la Loliondo, hawana elimu wala uhakika wa maisha baada ya mifugo yao kufa kwa ukame.

Wao ndio wanaopakaziwa kuwa waharibifu wakubwa wa mazingira ndani ya pori. Kila anayewapinga hawezi kuthubutu kusema kwamba watu hao wa jamii ya wafugaji wa kabila la Masai, ndio watunzaji wakubwa wa misitu, mbuga, mito, milima na wanyama katika hifadhi na mbuga zilizo jirani.

Wamasai wanaheshimu kupita kiasi mazingira kwa sababu asilimia 90 ya maisha yao hutegemea rasilimali hizo. Hawakuwa kero kabla ya kuja wenye fedhaa, eti wawe kero miaka hii ya 1990. Nini kama siyo kituko?

Wamasai hawahitaji kula wanyamapori, hawajengi maghorofa, hawachomi mkaa na hawalimi mashamba makubwa zaidi ya vibustani vya kupata mboga.

Utamaduni wa Wamasai hauruhusu kukata mti mbichi maana kufanya hivyo ni kuua maisha na malisho ya mifugo. Bado wasiowapenda wanathubutu kuwaita wafugaji wa Loliondo “Waharibifu wa mazingira.”

Tatizo ni kwamba wafugaji, ambao wana mengi ya kusema kuhusu maisha yao na hisia zao, hawapati nafasi katika vyombo vya habari kujieleza. Wakiipata ndogo, wenye fedha wanatosa mamilioni ya shilingi kutuma waandishi wanaojua kutengeneza taarifa.

Kwa waandishi hao, la muhimu zaidi, ni kile wanachokipata kutoka kwa wanaowatuma kukandamiza haki za wananchi ndani ya nchi yao.
Ni nini kama siyo uandishi wa kiwendazawazimu mwandishi kuripoti kuwa kengele za mifugo ndio hufukuza wanyamapori?

Hawafikiri akilini mwao kujua kipi kina mshindo mkubwa zaidi hata kuogofya wanyamapori kati ya kengele za ngo’mbe na mbuzi na zile zitokazo kwa ndege kubwa zenye uwezo wa kubeba magari hata kumi kila moja zikitembea umbali wa kilometa 100 ndani na katikati ya pori tengefu la Loliondo?

Kwa uzoefu wangu na mandhari ya maeneo ya hifadhi ya wanyamapori, milio ya ndege kubwa inaleta hofu kwa wanyama na viumbe wengine kama inavyokuwa kwa wanadamu.

Sheria za nchi haziruhusu ndege kubwa kutua karibu na wanyama lakini hakuna anayeuliza uvunjaji wa sheria hii unaofanywa kila wakati Loliondo.

Upo uzoefu mwingine wa kihistoria. Mifugo yote inayofugwa na binadamu ni rafiki wakubwa kwa wanyamapori. Wamasai wanajua fika wanyama kama pundamilia wanapowindwa na wakali wao, hukimbilia yalipo makundi ya mifugo kutafuta kinga dhidi ya wavamizi.

Je, waandishi waovu wanajua kuwa nyakati za jioni wanyama wote kama tembo, twiga na punda hupenda kufuata yalipo maboma ya Wamasai kwa ajili ya kulala?

Imani yao ni kwamba ndiko kwenye usalama. Hata wanyama kama nyumbu huwa hawazai kwenye mapori bali mbugani kwa sababu ya kujilinda na wanyama wakali.

Nani kasema wafugaji katika pori tengefu la Loliondo huharibu mazalia ya nyumbu kama siyo kichaa?

Asilimia zaidi ya 80 ya ardhi ya Ngorongoro ni mbuga, hifadhi au mapito ya wanyamapori na pia ndiyo malisho ya wanyama hao. Na kwa miaka mingi wanyama na mifugo wamekuwa wakila, kunywa na kulala pamoja.

Hakuna majangili katika jamii ya Wamasai maana Wamasai hawali nyama za porini wala si wafanyabiashara wa nyama hiyo.

Sasa wanapataje utashi wa kuua wanyamapori? Je, ni Wamasai hao wanaoua faru kwenye Hifadhi ya Serengeti?

Laa, tuseme wafugaji wa Kimasai ni majangili. Hivi kwa miaka yote ya maisha yao ya ujangili, zama hizi kungekuwa na mnyama gain aliyenusurika na mishale yao kwa namna walivyo jasiri kama wanavyoshuhudiwa wanapomsaka mnyamapori aliyeua mtoto au mwanamke wa Kimasai?

Na je wanyama hao wa pori wangethubutu kwenda kulala na mifugo au kulala karibu na yalipo maboma ya wafugaji wa Kimasai? Nani anayeikaribia hatari ya adui anayemjua kwamba atatamani kumvamia na kumla?

<p> Mwandishi wa makala hii, amejitambulisha kuwa msomaji wa MwanaHALISI. Anapatikana kwa imeili: ndusa2008@gmail.com</p>
0
No votes yet