Wafugaji wa Mbarali wametekelezwa?


Ndimi Jidawaya Kazamoyo's picture

Na Ndimi Jidawaya ... - Imechapwa 06 May 2008

Printer-friendly version

INAJULIKANA mwaka 2007 Serikali iliendesha operesheni ya kuondoa mifugo yote iliyokuwa ikichungwa eneo la Ihefu (Hifadhini) na kuipeleka mikoa ya Lindi na Pwani. Operesheni hii ilitokana na amri ya Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohamed Shein.

Baada ya hapo, kilichofuatia ni Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Hawa Ngulume, kuamuru Jeshi la Polisi kukamata ng'ombe wote kokote kule watakopatikana hata kama ni nje ya Hifadhi ya Ihefu kwenye vyanzo vya maji.

Operesheni hiyo ilijaa kila aina ya ufisadi: rushwa, magendo, dhulma dhidi ya haki za binadamu, ulanguzi na ukiukaji wa haki za wanyama.

Kuhusu rushwa, hili lilitendeka kwa njia mbili: ya kwanza ni kwa viongozi wa serikali wilayani kutaka na kupokea rushwa kutoka kwa wafugaji kwa kuwatoza kilichoitwa faini ya Sh. 10,000 kwa kila ng'ombe. Kiasi hiki kilipandishwa baadaye kuwa Sh. 50,000 kwa kila ng'ombe. Faini hizi zilitajwa kuwa ni kutokana na uharibifu wa mazingira uliofanywa na wenye ng'ombe.

Hili ni tatizo kwa sababu uharibifu wa mazingira wilayani Mbarali haukuletwa na mifugo tu bali ni hata kilimo kisichofuata utaratibu mzuri, mabadiliko ya hali ya hewa na kadhalika.

Kitendo hiki kilisababisha umasikini kwa wafugaji na familia zao na kikawajengea viongozi wa serikali utajiri wa harakaharaka. Mfano mzuri ni DC wa Mbarali, Hawa Ngulume na viongozi wa kata ya Mapogoro waliokuwepo wakati huo.

Inanikera kuona baadhi ya viongozi hawa wamebadilika kimaisha haraka ikijionyesha hasa kwamba wamenufaika na operesheni ile. Kiongozi mmoja wa Kata amenunua magari manne kutokana na fedha alizowanyonya wafugaji; ana gari la kutembelea lenye thamani ya zaidi ya Sh. 8 milioni; ana Coaster na Hiace ambazo zinatumika kama daladala kati ya Tunduma na Mbeya.

Kiongozi huyu pia anamiliki nyumba eneo la Mswiswi, Kata ya Igurusi (Mbarali), yenye thamani ya zaidi ya Sh. 15,000,000. Ni mshahara kiasi gani anaopata kiongozi wa ngazi ya kata hata kumwezesha kumiliki mali zote hizi kwa muda mfupi aliokaa madarakani?

Upande mwingine wa rushwa ulihusu mtu mmoja mmoja. Kwa mfano kiongozi wa juu katika Kata, alihadaa wafugaji kwa kutaka wampatie kiasi fulani cha fedha akidai kuwa ni kwa ajili ya kufanya mpango kuwezesha ng'ombe wao wasafirishwe haraka, si hivyo, atawaachia.

Miongozi mwa wafugaji walioingia katika mtego wa kiongozi huyu, ni Kazamoyo Kona na Kongwa Laluka. Kila mmoja akamlipa kiongozi wa kata Sh. 1,500,000 alizodai kuwa ni za kusaidia mpango wa kusafirisha ng'ombe wao haraka kuwafikisha kunakotakiwa. Hakuna alichokifanya na wafugaji walishindwa kumfuatilia kutokana na vitisho alivyokuwa ametoa.

Dhambi nyingine iliyofanywa na kiongozi huyo ni kudhulumu ng'ombe 30 wa mfugaji Kashinje Salawi. Huyu alikutwa na ng'ombe 70 na baada ya kushinikizwa kutoa fedha kwa kutarajia ng'ombe wake wasafirishwe haraka, kiongozi husika aliuza ng'ombe 30 kuchukua fedha zote huku akimtishia mfugaji kuwa atakamata ng'ombe wengine akimfuatafuata au kwenda kambini walikohifadhiwa.

Ukiukwaji wa haki za binadamu pia ulikuwa umeenea wakati wa operesheni. Watu walichukuliwa kama wasiokuwa na haki ya msingi ya kumiliki mali. Mfano mzuri ni wafugaji wengi walipokwenda kuangalia ng'ombe wao walipokamatwa, walipigwa sana.

Binafsi nilifuatilia kwa karibu matukio yalivyokuwa yakitendeka wakati wa operesheni na nilimfikia Mkuu wa Wilaya na kumsihi awape wafugaji uhuru wa kikatiba wa kumiliki mali na wasaidiwe kuokoa mali zao.

Baadaye nililazimika kuondoka Mbarali ili kusaidia kupeleka ng'ombe wa baba yangu mkoani Lindi. Ni kipindi hiki nilipata fursa ya kukutana na waandishi wa habari na kuelezea niliyoyaona kama ukiukaji haki za watu. Hatua hizi zilimkera Mkuu wa Wilaya.

Niliporudi Mbarali, nilikutana na wakati mgumu na kuanza kusongwasongwa na Polisi nikiambiwa nimemdhalilisha Mkuu wa Wilaya. Ng'ombe wengine wa baba wapatao 500 walikamatwa tena na nilipokwenda kambini kufanya utaratibu wa kuwasafirisha hadi Lindi, nilikamatwa na kupelekwa Kituo cha Polisi.

Nilifunguliwa shitaka la kutaka kupora kwa kutumia silaha katika kesi ambayo mpaka sasa iko Mahakama ya Wilaya ya Mbarali.

Kuna siku nikaitwa Bungeni ambako watu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu cha Dar es Salaam waliteuliwa kusimamia kesi hiyo wakati huo Kamati ya Bunge ya masuala ya Katiba na Sheria wakifanya mpango wa kuifuta kwani nilikuwa bado kidato cha nne wilayani Sumbawanga, na wao waliridhika na maelezo yangu ndio maana waliamua kesi ifutwe.

Mpaka sasa hakijatokea chochote kiasi cha kunipa imani kuwa labda wamepanga kuniangamiza pamoja na harakati zangu za kutopenda maovu.

Kingine kilichojadiliwa Bungeni ni kuhusu kuundwa kwa Tume huru itakayochunguza upotevu wa mali za wafugaji ili serikali iweze kuwafidia. Tume hiyo ilikuwa na wajumbe watano akiwemo Mkuu wa Mkoa mstaafu, Stephen Mashishanga, Mbunge wa Mbarali na mbunge mwingine wa mkoani Rukwa, Chrisant Mzindakaya.

Tume ilifanya uchunguzi wake Mei hadi Julai na ikakabidhi taarifa yake kwa Rais Jakaya Kikwete. Kuanzia hapo, wafugaji hawajaelezwa lolote hata ile haki yao ya kufidiwa kutokana na upotevu wa mifugo yao.

Familia yangu ilipata hasara ya zaidi ya Sh. 100 milioni kutokana na kadhia yote hiyo, na mpaka sasa haifahamu cha kufanya hata kupata uwezo wa kunisomesha wakati natakiwa kujiunga na Chuo Kikuu baada ya kumaliza vizuri kidato cha sita.

Wafugaji wa Mbarali wanajiuliza imekuaje wamedhulumiwa na viongozi wa serikali inayojinasibu kulinda haki za watu na mali zao? Je wafugaji hawa si raia wa Tanzania wenye haki ya kufidiwa kutokana na upotevu wa mali zao? Mbona wanasikia mara kwa mara raia wenzao sehemu nyingine wanafidiwa na serikali kutokana na uharibifu uliofanywa wa mali zao?

Pamoja na wafugaji wa Mbarali kutaka majibu ya maswali yao, pia wanauliza serikali imetoa ridhaa kwa viongozi wa wilaya hadi kata kudhulumu raia kama hawana haki ya kumiliki mali. Je viongozi waliohusika kufisidi wafugaji, wanachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kuwachunguza au ndio nchi ya "wenyewe na wenyewe ndio hao."

0
No votes yet