Wafugaji wafanyiwa unyama wa kutisha


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 28 July 2009

Printer-friendly version
Ni katika mbuga ya 'Loliondo ya Mwarabu'

WAMEPOTEZA tabasamu. Nyuso zimekunjamana. Macho yanabubujika machozi. Hawana hamu na mgeni. Wewe waweza kuwa "haramia" anayerudi kumalizia uhai wao.

Ni wanaume, wanawake na watoto ambao nyumba zao zimechomwa moto. Hawana pa kulala. Baadhi ya watoto hawajapatikana tangu walipokimbia milio ya mpasuko wa risasi na moto mkubwa uliotafuna nyumba zao kwa kasi isiyomithilika.

Hiyo ni sura unayokumbana nayo eneo la Loliondo, mkoani Arusha, lililoko zaidi ya kilometa 400 Kaskazini Magharibi mwa mji wa Arusha. Hapa wafugaji wanalazimishwa kuhama ili kupisha "utalii wa uwindaji."

Njia ambayo wahamishaji wameamua kutumia ni ile ya kuchoma moto nyumba, maghala ya vyakula na maboma ya mifugo – ng'ombe, mbuzi na kondoo.

Mkazi wa kitongoji cha Kirtalo-Karkarmoru katika kijiji cha Soitsambu anasema askari "waliovaa sare ya FFU" wakiwa na magari matatu ya aina ya Land Rover, moja likiwa na bendera nyekundu, ndio waliteketeza makazi kitongojini hapo.

Anasema walifika na kufyatua risasi angani huku wakiamuru wafugaji waondoke na ng'ombe wao. "Kufumba na kufumbua, askari wakaanza kuchoma moto nyumba zetu (pote hapa, anaonyesha) na maboma ya ng'ombe."

Unaonyeshwa lundo la majivu: Hapa ilikuwa nyumba ya baba. Hapa ya sisi watoto wake. Hapa lilikuwa ghala la chakula…Ndivyo ilivyo kote ambako moto umetumika kushinikiza wafugaji kuhama makazi yao. Ni msiba mkubwa.

Mzee Orkoskos Yiele anasema ana umri wa miaka 100. "Kaburi la baba yangu liko hapa. Kaburi la mama yangu liko hapa. Niondoke niende wapi?" Anauliza huku machozi yakimdondoka.

Ana familia ya zaidi ya watu 60. Wote hawana mahali pa kulala. Wanakoka moto. Wanapika kilichopatikana. Wanakula. Wanalala hapohapo nje wamezunguka meko – watoto kwa wakubwa.

Wiki mbili kabla ya kuchomewa nyumba, Mzee Orkoskos alikuwa na ugeni. Mmoja wa wageni alikuwa mwandishi Mussa Juma wa gazeti la Mwananchi aliyeko Arusha.

Mussa anakumbuka, "Hapa (akionyesha lundo la majivu), kulikuwa na nyumba nzuri tu kwa viwango vya huku. Tulikaribishwa na mzee Orkoskos, akatupa maziwa tukanywa na kuongea kwa muda mrefu."

Leo hakuna nyumba. Hakuna maziwa. Hakuna maboma ya ng'ombe, mbuzi wala kondoo. Hakuna furaha na vicheko. Ni kiza kisichobanduka nyusoni na ndani ya mitima ya wanakaya.

Orkoskos aliyeonekana kusononeka sana anasema, "Sijapotelewa fahamu; nimejawa hasira. Sina hamu ya kula. Wazazi wa watoto waliochoma mali zangu ni kama wajukuu zangu ambao hawana mahali pa kulala, mh…" (anashusha pumzi).

Anaeleza kuwa mtoto wake wa kike alikuwa mjamzito wa miezi minane au tisa. Wakati anakimbia moto na risasi, mimba ilitoka na kichanga ambacho kilikuwa cha kiume kimefariki. "Nani anajua kingekuwa nani katika jamii yetu au nchi nzima?" anauliza.

Kati ya ng'ombe 1,000 wa mzee Orkoskos, 100 wamepotea (hadi Jumatano iliyopita). Alikuwa anaendelea kuthibitisha mifugo iliyopotea kati ya mbuzi 800 na kondoo 700 aliokuwa nao awali.

Moto haukuchoma nyumba na mazizi peke yake. Ulichoma pia imani na utamaduni wa Wamasai. Mahali pa kufanyia tambiko, ambako ni moja ya sehemu muhimu kwa imani za jamii hii, napo palibakizwa majivu matupu.

Katika kitongoji cha Karkarmoru, Masambe Nguya anasema askari mmoja alipoona anatetemeka kwa woga, akammwagia mafuta ya petroli na "kunisukuma kwenye moto. Nilianguka chini kabla ya kuingia motoni; kutoka hapo nilikimbia bila kutazama nyuma."

Anasema pamoja na mali nyingine, mbuzi wake wawili na mbwa wachanga wanne waliungulia kwenye nyumba yake.

Hadi mwishoni mwa wiki, taarifa zilisema zaidi ya maboma 160 yalikuwa yameteketezwa katika eneo lote la Loliondo linaloitwa "Loliondo Game Controlled Area."

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Isidory Shirima anasema wafugaji wanatakiwa kuondoka kwenye maeneo hayo na "kurudi walikotoka." Anasema walipewa miezi mitano ya kuondoka lakini wamekaidi.

Anawaonya waandishi kutoandika habari zinazolenga kuwachochea wafugaji na kwamba yeye ana jukumu la "kulinda na kutekeleza sheria iliyopo hadi itakapofutwa."

Laiti Shirima angekutana na mzee Orkoskos aliyekuwa analea makaburi ya wazazi wake ambao inaaminika walikufa wakiwa na umri mkubwa; angejua kuwa kaya hiyo ina karibu karne mbili pale wanapoifukuza.

Ukoo huu na koo zingine, umekuwa katika eneo hili hata kabla wakoloni wa Kiingereza hawajalitangaza kuwa mbuga ya wanyama.

Kawaida Wamasai hawali nyama ya pori. Hivyo wamekuwa walinzi wa wanyama ambao dunia inakuja kuona, kupiga picha na kuwinda.

"Loliondo Game Controlled Area" ni eneo la ukubwa wa kilometa za mraba zipatazo 4,660. Hivi sasa eneo liko chini ya kampuni ya Ortelo Business Corporation (OBC) Limited ya Umoja wa Falme za Nchi za Kiarabu (UAE) ambayo mmiliki wake ametajwa kuwa Brigedia Mohamed Abdulrahim Al-Ali.

Kama mkoloni wa Kiingereza, kama mwekezaji Ortelo Business Corporation Limited. Walichotaka na wanachoendelea kuhitaji ni wanyama tu. Siyo binadamu.

Eneo la hifadhi, ambalo lina baadhi ya makazi yaliyoandikishwa kisheria kama vijiji, ni kubwa mno. Hata makao makuu ya wilaya, polisi, magereza, halmashauri, mji mdogo wa Wasso, vyote vimo katika eneo hili.

Kwa mujibu wa "miliki" hii, mtawala wa Ortelo anaweza kuchukua kijiko na kung'oa makao makuu ya wilaya au polisi, au hata kuyachoma moto kama askari walivyochoma makazi ya wafugaji.

Jeuri hiyo inajidhihirisha kwa tangazo linaloingia moja kwa moja katika simu yako ya mkononi ya kampuni ya Zain, pale unapoingia eneo hili.

Ghafla unasikia ujumbe wa simu unaingia na ukifungua unakuta yafuatayo kwa lugha ya Kiingereza: "Karibu Umoja wa Falme za Nchi za Kiarabu (UAE). Furahia kuwa kwako hapa kwa kutumia mtandao wa zain…" Hakika ni UAE ndani ya Tanzania.

Ni kuwepo kwa kampuni hii ya Arabuni ambako kunafanya wafugaji wawe na maoni makali dhidi ya Ortelo na serikali. Kila kitongoji unakokwenda, wahanga wanalaumu "Mwarabu" kuwa ndiye anashinikiza wahame.

Leina Koipa wa kitongoji cha Olorien katika kijiji cha Ololosokwan anasema mtoto wake wa miaka sita, Meirish Koipa, alimaliza siku mbili vichakani akiwa amekimbia moto baada ya kuona makazi yao yanachomwa na askari.

"Huyu Mwarabu ndiye chanzo cha matatizo yetu. Hii ni mara ya pili ninachomewa nyumba. Wanachoma hapa nasogea pale. Sasa angalia nimeishaanza kujenga hapa. Itakuwa hivi mpaka watuue sote..." anaeleza Koipa kwa sauti ya uchungu.

Julius Yiele (28) anasema, "Yote haya ni Mwarabu. Amehonga serikali na serikali sasa inatufukuza." Nilipomwambia kuwa kauli hiyo ni kali na yenye madai makubwa, alijibu haraka, "Ndivyo ilivyo. Sisi ni wakazi wa hapa."

Naye Ormeron Narikai wa kitongoji cha Olorien anakumbuka kuwa alikuwa na Sh. 1,150,500 nyumbani. "Ziliungulia humo pamoja na sanduku langu jipya. Acha Waarabu watuue tubaki historia, lakini hatuhami," anasema. Hapa unagundua uchungu uliokithiri.

Bali kivumbi cha kauli kilikuwa katika kijiji cha Ololosokwan, kwenye mkutano wa hadhara ambako wanakijiji walijadili uchomaji moto nyumba zao.

Mzee Yohana Sinyiu (60), baada ya kuambiwa kuwa kuna waandishi wa habari, alianza kwa kuuliza iwapo wana uwezo wa kuandika ukweli ili taarifa zifike kwa watawala na nje ya nchi. Nilitakiwa kujibu swali hilo. Nilisema, "Uwezo tunao."

Mzee Sinyiu alisema, "Tanzania ni mwanachama wa Umoja wa Mataifa. Imeridhia mikataba ya kimataifa ya haki za binadamu. Ina Katiba. CCM ina ilani yake ya uchaguzi. Vipi serikali itutendee unyama jinsi hii?"

Kwa sauti ya ukali alisema, "Andikeni. Ishawishini serikali itutendee haki; itupe usalama kama ilivyokuwa. Sisi hapa ni CCM tangu wakati wa Nyerere, Mwinyi, Mkapa na sasa Kikwete," akitaja jina mojamoja la marais.

Kama anayekaribia kudondokwa machozi, mzee Sinyiu anasema, "Hatujawahi kukaribisha upinzani hapa… Tunashangaa CCM kututendea hivi…"

Mkasa katika eneo hili unaelezwa vema katika ripoti ya kijiji yenye kichwa kisemacho, "Uharibifu uliofanywa na Operesheni ya OBC na FFU dhidi ya wanakijiji cha Ololosokwan, tarehe 4 Julai 2009 saa 1 asubuhi hadi saa 4 asubuhi."

Ripoti inataja majina ya wahanga wa operesheni: mkuu wa kaya na wote katika kaya husika. Jumla ya kaya 44 zilikumbwa na kimbunga hicho na watu 137 ama wamepoteza vifaa, vyakula, fedha, dawa za mifugo au mifugo. Ni hasara ya mamilioni ya shilingi.

Mjadala wa ripoti hii ulikuwa mzito kutokana na kauli za wanakijiji. Babu Olonyo alisema, "Tunashangaa kuona mtu anatoka Arabuni anapewa ardhi, sisi hatuna mahali pa kuchimba choo, kupumzikia na hata kuzikana."

"Sasa andika haya: Tumechoka kuishi… Mwambie mkuu wa wilaya na rais watupige bomu tufe tuishe," alisema Olonyo akichuruzika chozi kutoka jicho la kushoto.

Kanyo Ndoinyo (74) alisema, "Walikuja watawala wa Kiarabu, Kijerumani na Kiingereza. Wakatoka. Tukapata uhuru. Sasa ukoloni umerudi. Uhuru wetu umekwenda wapi?"

Ephraim Kaula (54) anauliza, "Kumetokea nini katika awamu ya nne ya utawala," na kuongeza "Tumekosa nini? Tumekaidi nini? Tuitwe wahanga wa nani… Sasa tutaendelea kulima. Tutajenga bila kujali kama tutakufa au tutapona."

Msembi Ndoinye alisema, "Wanyama ambao Wazungu na Waarabu wanakuja kuona, kuwinda na hata kubeba na kupeleka kwao, tumewatunza sisi, lakini sasa shukrani ni kufukuzwa."

Nasha Leitura aliwakomalia waandishi wa vituo vya televisheni vya Channel Ten na Star TV watangaze kuwa kitendo cha kuwachomea nyumba na mali kimewafadhaisha; ni ukatili mkubwa na uvunjaji wa haki za binadamu.

"Wewe mama (akimweleza mwandishi wa Channel Ten), usitangaze kidogokidogo. Toa yote kama ulivyoyaona na kuyasikia," alisisitiza Leitura.

Naye Koya Timan alisema serikali imeanza kuzungumzia suala la fidia kwa waliopoteza mali. Mwanamke huyo aliuliza, "Fidia ni kitu gani? Watuache na ardhi yetu ili watoto hawa na watakaozaliwa wapate mahali pa kuishi. Inatosha tu kubakiwa na ardhi yetu."

"Mwambie rais arudishe Waarabu wake huko alikowatoa. Fikisha maneno haya kwamba sisi wanawake tumekutuma," alisema Timan.

Kauli ya Mwalimu Lukuine ilikuwa kavu na kali. "Serikali inatupeleka kama nyani; inaturudisha katika umasikini…hatuna imani na serikali hii."

Mwenyekiti wa kijiji cha Ololosokwan, Julius Kaura anasema, "Utaratibu wote wa ardhi umefuatwa. Kijiji kipo kisheria. Sisi tumezoea kufuata sheria. Lakini sasa serikali ndiyo haifuati sheria. Hii siyo sahihi," alisema Kaura.

Hiki ndicho kijiji pekee wilayani Ngorogoro ambacho kinajivunia wahitimu wawili wa chuo kikuu na ambacho kimetumia mapato yake yapatayo Sh. 146 milioni kusomesha wanafunzi 128 katika miaka minne iliyopita.

Eneo lililo chini ya Ortelo lina uwanja wa ndege kwenye eneo linaloitwa Mumbarashani. Kuna madai kuwa ndege huingia na kutoka bila kukaguliwa hasa wakati wa msimu wa kuwinda. Lakini mkuu wa mkoa anasema kama hilo lina mashaka "basi wizara husika italiangalia."

Katika mbuga hizo, kwenye kilima cha Masiendilo, ndiko kuna jumba kubwa la mfalme wa UAE ambako huwa anakaa wakati amekuja kuwinda.

Pia ipo kambi kubwa ya kufikia wageni wa mfalme na wengine wanaokwenda kuwinda, pamoja na karakana kubwa ya magari katika eneo la Limawani ili kukamilisha madoido yanayohitajika kumhudumia mfalme wa UAE na wageni wake.

Tangu mwaka 1992, mfame kutoka UAE na wageni wake, wamepata uhondo katika Loliondo, huku wafugaji wakipata kibano cha ama kusogezwa au kufukuzwa kabisa katika maeneo haya.

Msukumo wa sasa wa kufukuza wafugaji, hadi kuchoma moto makazi yao, unatokana na sheria mpya ya wanyamapori ya kutaka kutenganisha mbuga na makazi ya wananchi.

Katika hili, bila shaka Ortelo watapenda lifanyike haraka kabla sheria haijaanza kutumika ili eneo lake libaki pana.

Kuna taarifa kuwa Rais Jakaya Kikwete aliishafika kwenye jumba la mfalme kwenye kilima cha Masiendilo.

Wengi nilioongea nao walitaja ziara ya kustukiza ya Kikwete kwenye makazi ya mfalme, jambo ambalo linaweza kuongeza ugumu au kuleta wepesi wa kushughulikia maisha, mali na makazi ya wafugaji.

Kwa sasa mbuga ya wanyama ya Loliondo inabaki sehemu ya UAE kama tangazo la Zain linavyosema. Maana yake ni kwamba Wamasai wafugaji na raia hawana chao; kwenye ardhi yao na ndani ya nchi yao.

Kuna haja ya kuchukua hatua, hata kufuta sheria na mikataba – vyote vya kilafi na kifisadi – inayoharamisha makazi ya wazawa na kutukuza fedha za mwekezaji. Shabaha iwe kuheshimu na kulinda haki za wananchi wafugaji na wakazi.

Rais Kikwete ana uwezo mkubwa wa kuelewa hili; labda kama hataki na bila sababu yoyote. Kilio cha wananchi kilichorekodiwa hapa ni maarifa tosha kwa mwenye nia ya kuona haki inatendeka.

0
No votes yet