Wageni haramu wasibembelezwe


editor's picture

Na editor - Imechapwa 15 October 2010

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

HIVI karibuni, Waziri wa Viwanda na Biashara Dk. Cyril Chami alifanya ziara ya kujitambulisha kwa wafanyakazi wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni Tanzania (BRELA) na huko alitoa msimamo wa serikali wageni waliojipa uenyeji.Katika ziara hiyo Dk. Chami alisema wageni wote wanaojishughulisha na shughuli ambazo kimsingi sizo walizoombea kibali walipofika nchini watafukuzwa.

Alisema wageni waliopewa kibali cha kuingi nchini kwa shughuli maalum, wakishakamilisha au wakimaliza mikataba yao, wanapaswa kuondoka kabla ya kuanzisha kampeni ya kuwatimua kwani kuendelea kuishi ni kinyume cha sheria.

Hatua hiyo ya serikali ni nzuri na inastahili kupongezwa na Watanzania wote na tunasema wageni haramu wasibembelezwe. Lakini huo ni uamuzi wa serikali au wa Dk. Chami?

Tunauliza hivyo kwa sababu tumekuwa tukisikia kauli za namna hiyo kila mara, lakini jamii inashuhudia kasi kubwa ya ongezeko la wawekezaji wa kupika ‘chipsi’ na kunyosha mabodi Kariakoo.

Mathalani mawaziri waliotangulia katika wizara hiyo waliwahi kutishia kupokonya na kurejesha serikalini biashara ambazo hazikuendelezwa na walionunua. Vilevile mawaziri walitishia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wawekezaji walionunua kampuni fulani lakini wakabadili matumizi au biashara.

Pamoja na vitisho hivyo, tumeshuhudia waliouziwa mashamba makubwa ya mpunga wakiachana na kilimo hicho na kuamua kulima mibono na mazao mengine ya nishati. Mawaziri waliokemea waligonga mwamba kwa madai hayawahusu mashamba yale ni mali yao.

Waziri mwingine aliwafuata waliobinafsishiwa kiwanda cha kutengeneza juisi akitaka watumie matunda halisi yaliyojaa sokoni badala ya ‘unga’ wa matunda. Waziri huyo aliambiwa si kazi yake. Mbaya zaidi ni kwamba wanaodaiwa kuwa ni wageni na kujihalalishia kubaki, wanalindwa na mfumo mchafu wa rushwa.

Ndiyo maana tunamuuliza Dk. Chami kwamba huo ni mkakati wa serikali au wake binafsi? Kama ni wake basi hata watangulizi wake waligonga mwamba na kama ni wa serikali basi hakuna utaratibu mzuri wa utekelezaji. Kama mfumo utakuwa unafanya kazi vizuri Dk. Chami hatalazimika kufunga safari tena kwenda Brela kueleza wageni haramu waondoke.

Hiyo si ndiyo kazi ya Uhamiaji, Kamisheni ya Kazi, Usalama wa Taifa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) wanafanya nini?

0
No votes yet