Wagonga meza, wazomeaji CCM kutunga katiba mpya


Nyaronyo Kicheere's picture

Na Nyaronyo Kicheere - Imechapwa 27 July 2011

Printer-friendly version
Jamvi la Weledi

MKAKATI mahsusi wa kuwezesha kupitishwa kwa muswada wa marekebisho ya katiba kupitia Bunge hili la sasa lililojaa wazomeaji na wagonga meza wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) umeandaliwa.

Sasa muswada huo umefanyiwa marekebisho na unatarajiwa kurejeshwa bungeni ukiwa katika lugha ya Kiingereza na Kiswahili, lakini katika hali mbaya zaidi ya ule ulioondolewa.

Ukiusoma muswada uliorejeshwa utagundua mambo manne ya kutisha: Kwanza, Tume ya sasa ya uchaguzi ndiyo itasimamia na kuendesha kura ya maoni kama Watanzania wanaikubali katiba itakayotungwa au la.

Pili, mawaziri wa katiba na sheria pamoja na wanasheria wakuu wa Tanzania na Zanzibar watakuwa wajumbe wa bunge maalum la katiba.

Tatu, kulingana na muswada uliofanyiwa marekebisho, madaraka ya rais katika mchakato mzima wa kutunga katiba mpya ni makubwa mno. Nne rais ndiye atateua wajumbe wa Bunge maalum la katiba.

Ukiusoma kwa makini muswada huu utagundua kwamba yamewekwa mazingira ya kupigwa kura mara tatu kati ya sasa na Desemba mwaka 2015. Mara ya kwanza ni kupata wajumbe au wabunge wa bunge maalum la katiba, ya pili ni kura ya maoni (referendum) kama wananchi wanaikubali katiba mpya au la, na tatu ni uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na rais utakaofanyika Oktoba mwaka 2015.

Muswada uliorekebishwa umetamka kutakuwepo bunge la katiba na kura ya maoni ili katiba mpya iwe imepatikana kabla ya uchaguzi mkuu wa 2015.

Sasa jambo la kwanza la kutisha ni la Rais kuunda bunge la katiba. Hivi ataliundaje au atateuaje wajumbe wake? Historia inaonyesha kuwa mwaka 1962 Bunge la Tanganyika ndilo lilijigeuza kuwa Bunge la Katiba na kupitisha katiba ya Jamhuri ya mwaka 1962.

Pia historia inaonyesha mwaka 1977 Mwalimu Nyerere aliteua wabunge wote wa Bunge la Muungano kuwa wajumbe wa bunge la katiba lililopitisha katiba yetu inayotumika hadi leo.

Hatari kubwa iliyopo mbele yetu ni ya Rais Jakaya Kikwete kuteua wabunge wa sasa kuwa wajumbe wa bunge maalum la katiba litakalopitisha katiba mpya kabla ya mwaka 2015 akiiga yaliyofanyika 1977.

Maana yake ni kwamba bunge hilihili lililosheheni wabunge ambao sifa yao pekee zaidi ya kujua kusoma na kuandika ni kuzomea na kugonga meza ndio watakaotutungia katiba. Hili ndilo jambo la kutisha la kwanza linaloletwa na muswada huu wa marekebisho ya katiba.

Tena Kikwete atatamba kuwa amewateua wabunge wote bila kubagua. Na atajigamba kuwa bunge hilo maalum lina wabunge wote wa CCM, CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi. Lakini nani asiyejua kuwa akina Zito Kabwe, David Kafulira, Wenje, Hamad Rashid, Freeman Mbowe, John Mnyika na wenzao katika upinzani ni asilimia 20 tu ya wabunge wote?

Katika mazingira hayo nani atasema bunge maalum la katiba limewakilisha matakwa ya wananchi wakati sote tunajua wabunge hawa walipatikanaje na chini ya sheria gani na katika uchaguzi uliosimamiwa na Tume ipi? Ndiyo maana nasema wananchi waachane na kushabikia vituko vya bunge wajadili muswada isije kutokea Kikwete akateua wabuge wa sasa kututungia katiba.

Sababu ninayoiona itakayotolewa na Kikwete kuhalalisha uteuzi wake wa wabunge ni kwamba muda hautoshi kufanya uchaguzi wa wajumbe wa bunge la katiba na pia atasema uchaguzi ni ghali sana na hivyo hakuna pesa za kutosha kufanya uchaguzi wa bunge maalum la kuendesha kura ya maoni na baadaye kufanya uchaguzi mkuu mwaka 2015.

Mimi nasema ni afadhali kama ikibidi kuahirisha utungaji katiba hata baada ya uchaguzi mkuu wa 2015 ili tuweze kupata katiba ya kweli ya Watanzania badala ya katiba ya kuchakachua. Ni afadhali kusubiri tukapata katiba mpya badala ya katiba ambayo haitawakilisha matakwa ya wananchi.

Jambo la pili linalotisha la Tume ya Uchaguzi Tanzania (NEC) halihitaji maelezo marefu. Tume ya Jaji Lewis Makame imefanya mambo mengi yasiyoelezeka hata na wajumbe wenyewe wa NEC. Mfano yawezekanaje matokeo ya Nyakanazi wilayani Biharamulo yakapatikana kabla ya matokeo ya Tabata hatua kadhaa kutoka ilipo ofisi yao.

Mbaya zaidi taarifa za tume ya Jaji Makame zinaonyesha sehemu nyingine wapiga kura walikuwa wengi kuliko kura zenyewe wakati mwingine kura zinakuwa nyingi kuliko idadi ya watu waliopiga kura. Naambiwa hadi leo tume ya Makame haijui ni Watanzania wangapi walipiga kura na wagombea urais walipata kura ngapi kila mmoja!

NEC hii haifai kusimamia na kuendesha kura ya maoni kuamua kama Watanzania wanaikubali katiba mpya au hapana. Tunataka tume inayotenda haki na inayoongozwa na mtu mwenye umri wa mtu mzima mmoja na siyo tume isiyotenda haki na inayoongozwa na mtu mwenye umri wa watu wazima watatu.

Jambo la tatu linalotisha kuhusu muswada uliorekebishwa ni mawaziri wa katiba na sheria wa Tanzania na Zanzibar pamoja na wanasheria wakuu Tanzania na Zanzibar kuwa wajumbe wa bunge maalum la katiba. Hapa inaonyesha jinsi gani serikali ya Kikwete isivyotaka Watanzania watunge katiba yao.

Kuweka kifungu cha sheria kinachotamka kuwa fulani na fulani watakuwa wajumbe wa bunge maalum la katiba ni kusema kwamba Watanzania hawatakuwa na haki ya kuchagua wajumbe watakaopitisha katiba hiyo. Kama wajumbe wanatamkwa na sheria iliyotungwa na bunge la CCM je wajumbe hao watapiga kura wakimwakilisha nani kama siyo CCM?

Ni makosa makubwa kuwachagulia wananchi wa Tanzania mtu wa kuwawakilisha katika bunge la katiba. Weledi unataka wananchi wenyewe wachague mtu wa kuwawakilisha siyo kifungu cha sheria kitamke nani mjumbe na nani si mjumbe wa bunge la kupitisha katiba?

Uhalali wa kisheria na kisiasa wa katiba mpya utapatikanaje kama wajumbe wengine wa bunge la katiba wanatamkwa na sheria badala ya kuchaguliwa na wananchi?

Haya ndiyo mambo ya kujadili sasa ili kuepusha hatari ya kutungiwa katiba na CCM hao hao wanaopinga Mzee wa Vijisenti kupelekwa mahakamani au wanaokataa kuundwa kamati kuchunguza Meremeta.

La nne ni hili la rais kuwa na madaraka makubwa na hivyo kufanya anachokitaka kiwemo kwenye katiba mpya badala ya kile wanachokitaka wananchi yaani wenye katiba wenyewe. Hii ni hatari kubwa sawa na kutunga katiba ya rais na chama anachotoka badala ya kutunga katiba ya Tanzania.

Muswada unampa rais madaraka ya kuuridhia muswada huo kuwa sheria, kuunda tume ya kuratibu marekebisho ya Katiba, kuteua wajumbe wa tume ya kuratibu marekebisho ya katiba na kuandaa hadidu za rejea za tume hiyo.

Pia muswada umempa rais madaraka ya kupokea ripoti ya Tume na hatimaye rais huyo huyo ndiye atateua wajumbe wa bunge maalum la katiba kutokana na rasimu ya katiba iliyoandaliwa kutokana na maoni yaliyoratibiwa na Tume aliyoiteua yeye!

Madaraka yote haya yanafanya katiba itakayotungwa kuwa katiba ya rais na chama chake tawala na siyo katiba iliyotungwa kwa matakwa ya wananchi wa Tanzania. Mungu aepushe mbali.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: