Wahafidhina serikalini pambazuko laja


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 09 March 2011

Printer-friendly version
Tafakuri

KUNA wakati taifa hili lilifikia viwango vya juu sana kwa uelewa wa watu wake kujua kusoma, kuhesabu na kuandika ‘KKK.’ Haya yalikuwa ni mafanikio makubwa ambayo Tanzania ilijivunia miaka ya mwisho wa sabini na miaka ya themanini.

Leo tunaelezwa kwamba kiwango hicho kimeporomoka mno, tupo kwenye asilimia hamsini na ushei hivi. Tumedondoka! Kwa wakubwa wanalalama kuwa ni pamoja na kufa kwa elimu ya watu wazima, yaani elimu ya ngumbaru, lakini kwa wengine wanafungamanisha anguko hilo na sera za kiuchumi za dunia.

Kwamba kila wakati tunapokea maelekezo, fanya hiki na kile, kama taifa hatuna tunachoamua wenyewe kwa utashi wetu. Wakubwa ulimwenguni – Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha Duniani (IMF) – wakisema  acha kutoa ruzuku kwa wakulima, unaacha. Wakisema acha kugharimia elimu ya watu wako, unaacha, vinginevyo watakushughulikia!

Ingawa inawezekana kuna chembe ya ukweli katika maelezo hayo, lakini bado binafsi napata kigugumizi cha fikra kuyameza mazima mazima bila kuyatafuna. Nachelea kudhuru koromeo langu.

Nasema haya kwa sababu kwa ufahamu wangu, pamoja na juhudi zote za serikali katika kugharimia elimu kwa mfano, hakika haijawahi kuwa ni nia yake ya dhati kukomboa watu wake kielimu.

Ndiyo maana wakati wote nimekuwa najenga hoja kwamba tatizo kubwa la mfumo wetu wa elimu, achilia mbali masuala ya mitaala na mbinu nyingine za kufundishia, bado tunaitazama elimu kama matumizi ya kawaida, badala ya kuangalia kama uwekezaji.

Kwangu mimi sioni tofauti ya kujenga barabara au jengo lolote, au daraja na kuwekeza kwenye elimu. Tunajenga madaraja au barabara au reli ili kuwezesha shughuli za kiuchumi zifanyike; yaani tunawekeza katika mbiundombinu vitu. Kwa elimu ningesema ni miundombinu watu. Kwa lugha ya kitaalam wanasema rasilimali watu kama vile ilivyo rasilimali vitu!

Kwa mfano, wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu Shirika la Utangazaji la Tanzania (TBC1) lilifanya kazi kubwa sana. Binafsi niliwawapongeza kwa kazi waliyofanya. Walimwaga waandishi wake kila kona ya Jamhuri ili kuwataarifu wananchi kinatokea.

Kwa waliokuwa wanaifuatilia TBC1 wakati huo, watakubaliana nami kwamba wale vijana walijitahidi sana kufanya kazi yao kwa weledi wa hali ya juu.

Walijua wanachokifanya, niongeze kusema kwamba kwa mara ya kwanza nilifurahishwa na taasisi ya umma kutekeleza wajibu wake bila kujidhania kwamba wanawajibika ama kusaidia chama tawala au kuibeba serikali hata kama mbeleko ya kufanya kazi hiyo haipo.

Tangu uchaguzi wa mwaka jana nimekuwa nawasiliana mara kwa mara na marafiki zangu walioko TBC1. Kikubwa ambacho nilikuja kugundua juu ya nafanikio ya utendaji wa waandishi wa habari wale wakati wa uchaguzi ni kuwapo kwa mafunzo maalum kwa kazi hiyo yaliyofanywa kwa msaada mkubwa wa Taasisi moja ya BBC iliyokuwa imeingia mkataba na TBC1. 

Kwa hakika habari zinasema kwamba taasisi hiyo ya BBC ambayo hivi karibuni tulielezwa mkataba wake wa TBC1 ulivunjwa, walijitolea fedha zao, wataalam wao na hata vifaa kuwafundisha waandishi wa  TBC1. .

Lakini wahenga walisema ng’ombe wa masikini hazai, ikitokea akazaa basi huzaa dume! Matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana baada ya tu kuonyesha wazi kuwa Watanzania wameanza kuiva, na kwa kweli watu sasa wanazidi kupata ujasiri wa kuzungumza mambo kwa uwazi na kutaka uwajibikaji; wahafidhina wachache serikalini wenye mawazo ya kufia kwenye nafasi wanazoshikilia, wanamtafuta mchawi wa pambazuko hili jipya.

Wa kwanza kabisa aliyetoshwa ni aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa TBC1, Tido Mhando. Mkataba wake ukakatizwa kinyama tu, lakini baada yake kwa dhambi ile ile ya kutokutaka watu waelemike, Taaisi ya BBC nayo imeambiwa ifungashe virago. Kisa? Kwa nini inafundisha vijana wa TBC1 kuwa waandishi mahiri!

Katika mkanganyiko huu, nikajikuta ninafananisha dhana na msimamo huu wa serikali kuhusu TBC1 na ile elimu yetu ya KKK tuliozoezwa na pambazuko hili jipya la uelewa wa waandidhi wa TBC1 na utoaji wa elimu ya kweli kwa wananchi, na uthubutu wao katika kuandika yale ambayo hakika yasingeandikwa.

Kwa tukio hili la juzi nikajipa majibu mengine ya ziada kwamba ndiyo maana tangu uhuru ulikuwa ni mkakati wa serikali wa kukataa kuwa na waandishi wa habari werevu, nguli, jasiri na wanaoweza kuhoji na kusaidia jamii kutambua iko wapi.

Nikajua vilivyo kuwa ni kwa nini wakati wote serikali imetumia matangazo kama silaha ya kuangamiza na kunyong’onyesha vyombo vya habari, hasa vya binafsi, ili kuzima moto wowote wa kuamsha uelewa wa wananchi.

Kwamba vyombo vya habari vishindwe kukua na kuenea nchi nzima, viishie tu mijini, lakini vijijini ambako kuna kura nyingi zaidi, visifike kwa sababu kimkakati nguvu zao za kiuchumi zimevunjwa vunjwa kwa nyezo ya kodi za wananchi, lakini hakuna pa kuhoji.

Mwenye kiherehere kama cha Tido na TBC1 yake anakatwa makali mapema. Hakuna sababu wala nia ya kuwajengea waandishi uwezo wa kiuandishi, wabakie tu kuwa watu wa kuisifu serikali na viongozi wake; ili wananchi wabaki gizani.

Ndiyo maana kusema hata pale tulipojisifu kwa mafanikio ya  KKK bado hatukuwa tumepiga hatua yoyote ya maana kwa maana ya kuijenga jamii yenye utambuzi mzuri wa mambo. Kwa maana ya kuwajengea watu wetu uwezo wa kutafakari na kupambanua maamuzi ya serikali na kuwapa changamoto viongozi juu ya wajibu wao katika dhamana walizopewa.

Ni kwa muonekanao huo, waandishi waliovuka kikwazo hicho cha KKK, na kuwa watu wa kuisaidia jamii kuijitambua si kwa kuwaletea matukio kuwa viongozi wao wako wapi tu, ila kwa kuwafungua wananchi wajitambue na kujiuliza maswali magumu katika mustakabali wa taifa lao, serikali imewaondoa.

Kwa kuwa sasa mbinu ya wahafidhina ndani ya serikali ni kuikata makali TBC1, mtu anajiuliliza serikali ina sababu gani basi ya kusumbuka na kuhangaika eti kiwango cha KKK kimeshuka wakati hiyo ndiyo nia yao miaka yote?

Kwamba wananchi waachwe gizani ili watawalike? Lakini wote wanaoendedeza udhaifu huu ndani ya serikali wakae wakijua kwamba hata kama TBC1 itakatwa makali, simu za mkononi ambazo zimeenea kila kona ya nchi watazifanya nini kwa kuzizima kuamsha mwamko mpya na mkali wa kuiwajibisha serikali?

Ujumbe wangu kwa wahafidhina ni huu, acheni kuwaza kizamani, anguko lenu litakuwa la kishindo kibaya.

0
No votes yet