Wahafihina wameanza kuachwa nyuma Zanzibar


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 14 April 2010

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

MIPANGO ya ujenzi wa “nyumba yetu Zanzibar,” inakwenda vizuri kwa sasa. Kasi inaridhisha japo umakini zaidi unahitajika ili kila lililopangwa litimie.

Wenye nia ya kukwamisha mipango ya Wazanzibari kuishi kwa amani ya kweli, utulivu na katika kushirikiana kuleta maendeleo, taratibu wanaachwa nyuma.

Mivutano ipo wazi miongoni mwa wananchi wanaoamini siasa za vyama, lakini wapingaji mipango ya ujenzi wa mama yetu Zanzibar, wanaongozwa na wanasiasa wahafidhina.

Bado wapo watu, na nguvu yao kubwa ni baadhi ya wanasiasa wasiotaka mabadiliko. Miongoni mwao wapo wanasiasa wakubwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Hawapendi kuona mipango ya wengi inakwenda vizuri.

Wala siyo kwamba hawapendi tu kuona mema, bali pia wanapanga kuhujumu hiyo mipango ya wengi. Wanakusanya fedha hadi mbali nje ya Afrika, wanazitumia kwa ajili ya kulaghai watu wakiwemo wasiojua mchele na pumba. Wanachotaka wahafidhina ni kukidhi maslahi binafsi.

Historia inaonyesha wazi kuwa wanasiasa kama hawa huweza kushinda muda mrefu matakwa yao, lakini hufika siku wakakwama. Na hapo hukwama kwelikweli.

Ukweli, wahafidhina wa Zanzibar wameshinda sana huko nyuma, sana tu kiasi kwamba madhara makubwa yametokea kwa watu na mali zao. Hata mali ya umma haikusalimika maana imekuwa ikitumika kuwasaidia kifedha kutimiza dhamira zao mbaya.

Muda wa kukwama umewadia na inaonyesha wenyewe wameanza kuamini kwamba tayari wanaachwa nyuma masafa marefu. Wazanzibari wanaendelea mbele.

Wahafidhina wanapitapita majimboni kushawishi wananchi wakatae kura ya maoni itakapokuja. Wameshindwa kuizima kwani tayari imepitishwa na Baraza la Wawakilishi.

Sheria ya kura ya maoni inasubiri tu kuridhiwa na rais ili ianze kutumika rasmi kama moja ya sheria ziliopo Zanzibar. Sheria hii inaruhusu kuitishwa kwa kura ya maoni kwa suala lolote linalotakiwa kuamuliwa na wananchi. Maana yake itaendelea kuwepo kwa siku za usoni.

Pongezi nyingi ziende kwa baraza la wawakilishi kwani lilipitisha kwa kauli moja muswada mbele ya wahafidhina ambao waliukacha muswada barazani.

Ajabu hata wale wajumbe wa majimboni (waliopigiwa kura na wananchi) wanaojulikana kwa ufundi wa kujadili kila jambo linalofikishwa barazani, walikaa kimya wakati wenzao wakijadili muswada.

Ni uthibitisho kuwa katika siasa za Zanzibar, lipo genge baya. Linafikiri kinyume na wanavyofikiri walio wengi. Mipango yao ni kinyume na matarajio ya dhamira njema ya kuijenga upya Zanzibar.

Genge hili linajumuisha wanasiasa wakubwa na wadogo. Wengine hata hawajapata kuchaguliwa kwa kura za wananchi. Wao ni kuteuliwa tu rais. Wapo.

Baadhi yao walitangazwa washindi na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ilhali walizidiwa kura masandukuni wakati wa uchaguzi.
Walipata kura kiduchu au “kura zao hazikutosha” kama baadhi yao wasemavyo.

Hakika walishindwa na wagombea wa CUF. Matokeo yaliyowaingiza barazani ni yaliyopelekwa makao makuu ya Tume kwa mtutu wa bunduki – siyo yale halali yaliyotokana na kura zilizorekodiwa vituoni.

Kila palipotangazwa matokeo haya palitanguliwa na uhuni usio sababu uliohusisha vikosi vya FFU waliotumwa kurushia wananchi mabomu ya machozi ili waondoke maeneo ya kutangazia matokeo.

Niseme tu kwamba wote hawa watalipa maana walikubali dhulma kutendeka. Waliwadhulumu haki wale wagombea wa upinzani walioshinda kihalali. Watawalipa maana haki ya mtu haipotei mbele ya muumba wetu.

Wajumbe kukacha muswada wa kura ya maoni, ni uthibitisho kuwa wapo wanasiasa wanapinga mpango wa Rais Amani Abeid Karume wa kusimamisha msingi wa kuwepo siasa za maridhiano kati ya wananchi wa Unguja na Pemba waliogawika mno kiitikadi juu ya vyama viwili – CCM na CUF.

Sina maana kuwa kila mtu anaamini katika moja ya vyama hivi. Laa hasha. Wapo wasiopenda siasa za vyama, wapo wanaovutika na baadhi tu na misimamo ya vyama hivi na wapo watazamaji tu.

Wapo wanasiasa waliojadili muswada wa kura ya maoni kwa mbinu za kujaribu kuficha dhamira zao mbaya. Hawapendi maridhiano lakini wanautaka urais, wengine wanataka uwakilishi au ubunge.

Hofu yao ni kwamba maridhiano yakisimama sawasawa, na mambo yakienda vizuri kama yalivyopangwa, wamezimwa matumaini yao. Watajiju!

Wazanzibari wanajenga nyumba yao. Nia yao ni kujenga nyumba imara kama chuma. Wanataka nyumba itakayokuwa na amani ya kweli. Itakayokaliwa na kila mmoja wao bila misuguano inayozingatia asili, rangi wala itikadi ya kisiasa.

Zanzibar inajengwa nyumba ambayo kila mtu atakuwa na haki na uhalali wa kujinasibu kuwa ni nchi yake na serikali inayochaguliwa inamwakilisha yeye.

Ila nikiri kwamba safari bado ni ngumu. Hivi kura ishapitishwa maana yake itapigwa siku ikifika. Serikali na vyombo vyake wataandaa mazingira ya kura hii kupigwa.

Kura yenyewe, nadhani, itakuwa ni ya kuuliza wananchi kama wanataka au hawataki mabadiliko ya kiutawala ya utaratibu wa kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa. Nasisitiza ni upotezaji muda tu lakini twendeni mbele.

Kwa mujibu wa muswada uliopitishwa, watakaoshiriki kura hiyo ni watu waliojumuishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura (DKWK) la Zanzibar.

Mtu ataingia kwenye daftari hili iwapo tu ameandikishwa kama mpiga kura wa Zanzibar. Na mtu ataandikishwa tu kama mpiga kura iwapo anamiliki kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi.

Hili ndilo suala linaloleta mshangao mkubwa kipindi hiki hasa kwa watu wanaofikiri vizuri na kwa nia njema ya kusaidia ujenzi wa nyumba yetu, Zanzibar.

Tume ya Uchaguzi ndiyo inayoandikisha wapiga kura. Lakini kitambulisho kinatolewa na Ofisi ya Usajili na Kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi.

Zote ni taasisi za serikali, ambazo viongozi wake wakuu wanateuliwa na rais, yule ambaye ameonyesha ujasiri wa kukaa meza moja na kinara wa CUF Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad na kukubaliana kujenga msingi wa siasa za maridhiano.

Sasa tangu awamu ya pili ya uandikishaji wapiga kura ianze, mdudu mbaya – mizengwe na mikingamo – anaendelea.

Hali ya mambo kwenye vituo vya uandikishaji wananchi inatisha na kusikitisha. Wapo watu wanaojiuliza kama kweli kuna dhamira ya kweli upande wa Rais Karume.

Wanayo sababu ya kuhoji. Rais Karume ndiye aliyeteua wakuu wa taasisi hizo mbili. Hawa walitarajiwa kuongoza taasisi kwa namna ya kuhakikisha zinatoa huduma kwa wananchi bila ya mizengwe. Sivyo ilivyo.

Nimeshuhudia mizengwe michache. Mingine mingi nimesimuliwa. Nimekutana na wahanga wa mizengwe: watu ambao wamekosa kuandikishwa.

Watu wengi – wakubwa kwa vijana waliotimia umri – wamepigwa pande. Maana yake hawakuhudumia ipasavyo kulingana na vielelezo walivyonavyo. Wiki ijayo tuje tuingie pamoja chumba cha uandikishaji.

0
No votes yet