Wahujumu wabanwe


editor's picture

Na editor - Imechapwa 21 September 2011

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

MWANZONI mwa miaka ya 1980 uchumi wa Tanzania uliyumba hali iliyosababisha baadhi ya wafanyabiashara wakubwa na wadogo kuhodhi bidhaa ili waziuze kwa bei kubwa.

Hata hivyo, serikali haikuwavumilia wafanyabiashara hao waliobatizwa majina ya walanguzi na wahujumu uchumi. Iliandaa utaratibu wa kugawa bidhaa adimu na muhimu kama sukari, nguo aina ya kanga na vitenge, na vifaa vya ujenzi.

Waziri mkuu wa wakati ule, Edward Moringe Sokoine alianzisha na kuratibu kampeni maalum ya kupambana na wahujumu uchumi. Waliokamatwa na kosa hilo walifunguliwa mashtaka.

Tatizo la kuadimika kwa baadhi ya bidhaa muhimu hasa sukari limeanza kuisumbua tena nchi yetu kwani tangu mapema mwaka huu, wafanyabiashara wakubwa walafi na wasio na utu wamekuwa wakilangua sukari.

Baadhi yao, hasa walioko mikoa ya pembezoni mwa nchi, wanadaiwa kusafirisha na kuuza sukari nchi jirani, lakini wengine huuza nchini kwa bei ya juu kuliko iliyoelekezwa.

Bei elekezi inaonesha sukari inapaswa kuuzwa kwa kiwango kisichozidi Sh. 1,700 lakini kuna ushahidi kwamba wafanyabiashara wengi katika maeneo hayo wanauza sukari kwa bei hata kuzidi Sh. 2,500 kwa kilo. Wana visingizio chungu nzima ikiwemo gharama za usafiri.

Jambo zuri ni kwamba Waziri Mkuu Mizengo Pinda amegundua tatizo hilo na akalazimika kufanya ziara mkoani Kagera ambako alikagua uzalishaji katika kiwanda cha sukari.

Wiki iliyopita, alikuwa mkoa wa Mara ambako alikumbana na tatizo hilohilo la bidhaa hiyo kuuzwa kwa bei kubwa kinyume na bei elekezi.

Waziri Mkuu ameagiza mkuu wa mkoa na wakuu wa wilaya kukagua maghala ya sukari na kuamuru iuzwe haraka kwa wafanyabiashara wa rejareja kwa bei muafaka.

Tunamuunga mkono waziri mkuu kwa hatua zake hizi. Na hapa tunazungumzia sukari inayozalishwa na viwanda vyetu ndani.

Kama ilivyokuwa miaka ya 1980, tunahimiza agizo la serikali litekelezwe kwa sheria zaidi kuliko mabavu ambayo yatasababisha mivutano. Wale watakaokataa kushirikiana na serikali, wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria zilizopo tukiamini kuwa kuhodhi bidhaa kwa nia ya kutafuta faida zaidi, ni kuvunja sheria za ushindani katika biashara huria.

Wakati tukihimiza hilo, tunashauri pia serikali iruhusu wafanyabiashara waaminifu waingize sukari kutoka nje ili kufidia uhaba wa bidhaa hiyo na hivyo kunufaisha wananchi.

0
No votes yet