Wahujumu walianza zamani Zanzibar


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 14 March 2012

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

MTU mmoja ameniambia, “Unaandika kimafumbo ilhali unajua nani wanaiibia nchi na nani wanafuja raslimali zetu. Si uwataje.”

Huyu ni msomaji wa makala za safu hii. Yawezekana wengine mnafikiri kama yeye. Ni rahisi kutaja majina ya watu wakiwemo viongozi serikalini na watu binafsi, kwa sababu “wanatajwatajwa” kila mahali.

Kweli, wamekuwepo watu wawili watatu wanaotajwa hadharani na wananchi na kuelezwa kuwa ndio wanyonyaji uchumi wa nchi.

Lakini, katika kazi ya uandishi wa habari na hata wa vitabu, kutaja majina ya watu kwa kuwatuhumu ubaya, kunamaana pana zaidi ya hiyo.

Ukitaja mtu unaeneza mawasiliano; unasambaza ujumbe na ukitaja unafahamisha watu wengi zaidi na kuwaweka katika kujiuliza kulikoni juu ya hao uliowataja.

Swali kubwa linakuwa, “Hivi hawa ni wahujumu kweli.” Ni swali hilohilo chombo cha habari kitatakiwa kueleza kwa kina kitapoitwa mahakamani.

Hatuogopi mahakama. Mimi siiogopi; na wenye taasisi ninayofanyia kazi hawaiogopi. Wanaodhani kuishitaki MwanaHALISI ndio njia ya kujihami, wanakwenda. Wao wataeleza yanayowakuta huko.

Nimekuwa nikijadili masuala ya ufisadi serikalini tangu nilipoingia kwenye uandishi wa uchokonozi – miaka ya 2000. Kabla ya hapo, nililenga zaidi kasoro za utawala bora na utawala wa sheria.

Ni hapo nilikumbusha wajibu wa viongozi kwa umma. Nililaumu viongozi waliokuwa wakifanya maamuzi yasiyoidhinishwa na mahakama, na wale waliokuwa wakidharau amri za mahakama zinapotolewa.

Nakumbuka nilishutumu kwa hoja nyingi uamuzi wa serikali kumhamisha kwa nguvu Nassor Cholo aliyekuwa na mgogoro wa kibiashara na washirika wake lakini baadhi ya viongozi waandamizi serikalini wakakutwa kuhusika kutia shinikizo afukuzwe nchini.

Kilichothibitika haraka na kwa mujibu wa maelezo ya mwenyewe Cholo, kijana mzaliwa wa Zanzibar anayeishi nchini Oman, ni kwamba eneo la biashara ambalo aliwekeza mamilioni ya shilingi, lilivutia vigogo hao kitamaa tu, na kulenga kumpora.

Ubaya wa sakata hilo la mwaka 2005, ni kuwa viongozi hao walivunja sheria na amri ya mahakama iliyotaka Cholo asiondoshwe nchini kwa kuwa kulikuwa na madai dhidi yake yaliyowasilishwa na mshirika wake.

Kwa mujibu wa sheria za Zanzibar, hakuna mtu ataruhusiwa kuondoka nchini iwapo kwenye mahakama ya kisheria kuna shauri lililofunguliwa dhidi yake.

Hapa maana yake ni kwamba viongozi wa serikali walivunja sheria. Walistahili kushitakiwa kwa mujibu wa sheria kama wanavyoshitakiwa watu wengine wanapobainika kuvunja sheria.

Dharau ya kutii sheria na amri za mahakama kama hiyo, ilionyeshwa pia na viongozi wa serikali ya mkoa wa Mjini Magharibi na wasaidizi wao katika wilaya ya Magharibi pale walipopeleka mabuldoza na kuvunja nyumba za wananchi eneo la Tomondo, ilhali hakuna mahakama iliyotoa amri ya kuvunjwa nyumba hizo.

Mpaka leo hakuna ushahidi uliowasilishwa mahakamani kuonyesha “amri” ya kuvunja makazi ya wananchi ilitolewa na mahakama ya kisheria. Wale viongozi walioamuru na kusimamia uvunjaji makazi ya raia walipaswa na wangali wanastahili kushitakiwa.

Hata sasa, ningali nashangaa kuona serikali imeendelea kunyamazia uvunjaji wa sheria unaotokana na kutotekelezwa kwa amri nyingi za mahakama za kuondolewa wavamizi wa ardhi katika shamba la Mzee Abdalla Shariff wa Shakani.

Amri hizo zimetolewa na mahakama mara kadhaa tangu pale mahakama ya mkoa wa Mjini Magharibi ilipotoa uamuzi wa kumpa haki mzee huyo aliyefungua madai ya kurejeshewa ardhi yake iliyovamiwa na watu kadhaa wakiwemo viongozi waandamizi wa serikali.

Viongozi hao ni pamoja na Mansour Yussuf Himid, ambaye anakabiliwa na kesi ya madai katika Mahakama ya Ardhi ya kuvamia eneo lisilokuwa lake.

Pale uvamizi wa ardhi ya mtu unapohusishwa na mtu wa hadhi ya waziri, achilia mbali viongozi wa ngazi nyingine za chini, ni hatari. Inaonyesha kwa kiwango gani uvunjaji sheria unavyoongezeka Zanzibar.

Niliwahi kujadili hapa tatizo la mali za serikali, yakiwemo majengo ya enzi na enzi, zinavyouzwa au kukodishwa kifisadi.

Lakini ni kadhia hiihii ikamsukuma Rais Dk. Ali Mohamed Shein, akiwa ndiyo kwanza amerudi ziarani nchini Ujerumani, kutamka mbele ya waandishi wa habari wa serikali kuwa serikali ikitaka kuuza chake haina wa kumuuliza.

Waweza kusema ni vizuri mwisho wa tamko lake, Rais alisema wasioridhika wafungue kesi mahakamani, lakini katika hali kama hiyo, kiongozi wa serikali akiwa ameshatia neno lake, nani atathubutu kupeleka kesi mahakamani?

Hata ile kauli ya rais katika suala hilo ni uvunjaji wa misingi ya utawala bora. Tamko lake lilikuwa ni kitisho kwa mtu yeyote anayedhani anaweza kutumia haki yake ya kikatiba kulalamika kisheria.

Wachunguzi wa serikali bado wanaweza kutafuta nani hasa aliyelipa maofisa wa serikali waliofungia kwa makufuli ghala la kuhifadhia bidhaa zilizotamkwa kuwa hazifai kutumika kwa sababu vimeshaharibika.

Mkemia Mkuu wa Serikali alichunguza shehena ya mchele wa mapembe ulioingizwa nchini na kampuni ya Bopar Enterprises Ltd, na kuthibitisha ulikuwa mbovu.

Lakini, licha ya kuwa ulihifadhiwa ghalani eneo la Mombasa Kwa Mchina kwa ajili ya kuja kuharibiwa, asubuhi ilikutwa ghala limefunguliwa na mchele wote kutoroshwa. Mchele huo ulipelekwa Tanga kupitia Pemba ambako uliingizwa sokoni.

Ile hatua ni kuvunja sheria. Nani alishughulikiwa kama si ofisa mdogo wa idara ya kumlinda mlaji. Kwanini mfanyabiashara mwenye mali hakuhojiwa? Nani hasa alifungua ghala na kuruhusu mchele kutoroshwa?

Kitendo hicho kilitekelezwa kwa msukumo wa mlungula. Umma ungependa kuona wahusika wanachunguzwa na kushitakiwa mahakamani.

Akili yangu mpaka leo inanikataza kudharau unyama wa kuvunja makazi ya wananchi eneo la Mtoni Kidatu, karibu na kituo kikuu cha umeme. Kitendo kile kilikuwa kibaya kisheria na hata kibinadamu. Nani alichukuliwa hatua?

Hata wanaotengeneza kesi dhidi ya wananchi nao wanavunja sheria na miiko ya uongozi. Pale mwandishi wa habari anaporipoti tukio lililoko kwenye mahakama anamkosea nani kisheria?

Basi viongozi wa serikali kwa sababu ya dhamana walizopewa, wanazitumia vibaya kubambikiza kesi waandishi wa habari kwa kuwa wameandika ukweli mtupu.

Mwandishi wa Nipashe, Mwinyi Sadallah, ni mfano mzuri. Hadi leo anakwenda na kurudi Mahakama ya Mkoa Vuga akisikiliza kesi dhidi yake iliyofunguliwa kwa sababu alinukuu nyaraka za Mahakama ya Ardhi katika kesi iliyofunguliwa na mwananchi wa Chwaka, dhidi ya kampuni ya mafuta, Gapco.

Mwananchi huyo anadai kuporwa ardhi ya familia eneo la Kipilipilini, Chwaka, bila ya idhini yao, na sehemu iliyoporwa imejengwa kituo cha mafuta cha Gapco. Alipouliza kampuni hiyo anadai kujibiwa kuwa waliidhinishwa kutumia eneo hilo na Rais Mstaafu Amani Abeid Karume.

Hapo mwandishi amefanya kosa gani? Ingawa halipo, Mwinyi angali analazimika kutupa muda kusubiri upande wa mashitaka utoe ushahidi uliokusudiwa kumfunga. Huu ni mwaka wa sita kesi hiyo haijamalizika.

0
No votes yet