Wajawazito wanavyoongezewa machungu Amana


William Kapawaga's picture

Na William Kapawaga - Imechapwa 27 January 2010

Printer-friendly version

JOYCE Mwalukasa ni mmoja wa wanawake walioathirika na huduma duni wanazopata wajawazito katika Hospitali ya Wilaya ya Ilala, Amana, Dar es Salaam.

Mkazi huyu wa Kiwalani Bombom amepoteza mtoto wakati akibishana na wahudumu wa Amana waliokuwa wakisita kumpokea na kumhudumia kwa sababu hakupaswa kujifungulia hapo.

Anasema, “Kwa kweli niseme tu kwamba yaliyonifika nilipokwenda kujifungua Amana yatabaki kwenye kumbukumbu maishani mwangu. Wahudumu ndio waliosababisha mtoto wangu afariki mara tu baada ya kujifungua.”

Malalamiko kama hayo anayatoa Mwanaisha Omary, mama anayekaribia kujifungua, akisema amefokewa na wahudumu wa hospitali ya Amana kwanini amekwenda kujifungulia hapo.

Mwanaisha na Joyce wanasema ni mtindo kwa wahudumu wa Hospitali ya Amana kusimanga wajawazito watokao maeneo ambayo kuna zahanati za kuwahudumia.

Wanasema wahudumu wamekuwa wakishikilia wajawazito walioko karibu na zahanati maeneo mbalimbali ya manispaa wajifungulie huko, labda tu kwa yule aliyeelekezwa mapema na madaktari kuwa ajifungulie Amana.

Hapo ndipo kinamama wanaposhangaa na kuhoji, “Kwanini watung’ang’anize kujifungulia kwenye zahanati wakati wanajua zahanati nyingi hazina madaktari na vifaa.”

Mama anayeishi Ukonga analalamika kuwa yupo karibu na zahanati hiyo, lakini imekuwa na tatizo sugu la ukosefu wa vifaa na wafanyakazi wenye ujuzi na kwamba “siko tayari kuhatarisha maisha yangu.”

Mkazi wa Kinyerezi, Chausiku Mshindo anatoa ushuhuda wa matatizo yanayowapata wajawazito wanapokwenda kujifungua hospitali ya Amana. Anasema wajawazito wanadharauliwa, wananyanyaswa na kusimangwa na wahudumu na mara nyingi wanatelekezwa.

Anasema, “Nilipojihisi nipo tayari kujifungua niliita sana wahudumu waliokuwa katika chumba chao lakini hakuna aliyekuja kunipa msaada mpaka nikajifungua bila ya msaada huku wakiendelea kupiga soga.”

Ni bahati kwamba alijifungua salama na mtoto wake anaendelea vizuri akiwa na umri wa mwaka na nusu sasa.

“Hali inatisha hospitali ya Amana… ni hatari wanatung’ang’aniza tutibiwe kwenye zahanati ambazo wanajua hazina madaktari wajuzi na zinakosa vitendea kazi… unapohitaji huduma ya upasuaji utaipata wapi.”

Anasema uongozi wa hospitali hauzungumzii upungufu wa vitanda kwenye wodi na vipi wanatatua tatizo hilo ambalo linalazimisha wazazi kulala hata watatu kitanda kimoja.

“Ni ustaarabu gani huu kuwalaza wajawazito wawili au watatu katika kitanda kimoja wakati mwingine pamoja na watoto wao baada ya kujifungua,” anahoji.

Nimeshuhudia msongamano huo nilipofuatilia malalamiko ya wanawake kuhusu huduma duni katika Hospitali ya Amana. Baadhi yao nilikuta wamelala chini kwa ukosefu wa vitanda.

Afisa Tawala wa Hospitali ya Amana, Christopher Shemchambo anasemaje kuhusu malalamiko hayo?

Anakiri upungufu wa madaktari lakini anatetea haja ya wale wajawazito wasio na matatizo kubaki wanakoishi ili wajifungulie kwenye zahanati zilizoko maeneo wanayoishi.

Shemchambo anasema zahanati hizo zina uwezo na zimekuwa zikihudumia wajawazito wengi tangu uchanga wa mimba zao.

Anasema ni pale tu mjamzito anapogundulika ana matatizo ndipo huelekezwa kujifungulia hospitali ya Amana.

“Utashangaa wajawazito wanahudhuria kliniki katika zahanati hizohizo, lakini wakitaka kujifungua wanakimbilia Amana hata kama mtu hana matatizo.

“Hili tunalipinga lakini hakuna mzazi aliyerudishwa baada ya kufika kwetu kwa ajili ya kujifungua. Hatuwezi kufanya hivyo kwani ni kukiuka miiko ya kazi yetu,” anasema.

Anasema zipo zahanati 15 katika wilaya ya Ilala zinazotoa tiba kwa magonjwa mbalimbali pamoja na kuhudumia wajawazito ikiwemo kuzalisha.

Bali anakiri nyingi haziwezi kuendesha huduma za upasuaji na anashauri wajawazito kukimbilia Amana wanapopata matatizo wakati wa kujifungua. Anasema madaktari na wauguzi kwenye zahanati wanalijua vizuri suala hilo.

Anasema wodi ya wazazi hospitalini Amana ina vitanda 110 wakati ile ya watoto ina vitanda 52. Shemchambo anakanusha taarifa za kuwepo wajawazito wanaolala chini.

Anasema hospitali ya Amana ina daktari mmoja tu maalum kwa ajili ya kuhudumia watoto. Anakiri kwamba hatoshelezi mahitaji kwani siku nyingine huwa ana kazi ya kutoa chanjo kwa watoto wanaozaliwa hivyo kukosa muda wa kuhudumia wajawazito.

Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk. Meshack Shimwela pia anakiri upupungufu wa madaktari kwani “idadi ya wagonjwa wanaofika kila siku inazidi.”

Kuhusu malalamiko dhidi ya wauguzi, Dk. Shimwela anasema wanayasikia lakini “Tumekuwa tukisisitiza wananchi wafike ofisini kulalamika.”

Anasema katika kila hospitali hiyo kama ilivyo kwa hospitali nyingine, kuna masanduku maalum kwa ajili ya watu kutoa maoni yao ikiwa ni pamoja na malalamiko kama hayo ya huyduma duni au kudharauliwa na mfanyakazi.

Anasema, “Wakishalalamika rasmi hatutasita kuchukua hatua tunaporidhika kuna uzembe umesababisha madhara yoyote.”

Dk. Shimwela anasema hospitali hiyo imejengwa kwa lengo la kuhudumia wananchi na kwamba haitakuwa na maana yoyote ikiwa wagonjwa wanafika kutaka huduma lakini wanazikosa.

Anasema ipo mipango ya kuimarisha hospitali hiyo kwa upanuzi wa majengo kwa kwenda juu kwa sababu hakuna eneo la kutosha la kufanya upanuzi kwa kujenga majengo mapya.

Anasema wameanza kuandaa michoro ili kuionyesha kwa mfadhili atakayekubali kusaidia kutekeleza mradi wa kuigeuza kuwa hospitali ya kisasa.

Hospitali ya Amana inapokea wagonjwa kutoka Tabata, Buguruni, Kinyerezi, Ukonga, Vingunguti, Kitunda, Kivule na Kiwalani pamoja na maeneo mengine yaliyo karibu nayo.

Mbunge wa Ilala, Musa Azan Zungu analo la nyongeza kuhusu mipango ya kuimarisha huduma katika hospitali hiyo. Anasema anashirikiana na uongozi wa hospitali kusimamia maombi yaliyopelekwa wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ya kutaka madaktari zaidi.

Zungu anasema wanasubiri majibu ya wizara ambayo imeshatangaza kwamba inakusudia kuongeza idadi ya madaktari katika hospitali tatu za manispaa katika Mkoa wa Dar es Salaam ambazo ni Amana, Temeke na Mwananyamala.

0
No votes yet