Wakali wa kuchungwa kikosi cha Morocco


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 06 October 2010

Printer-friendly version

MAROUANE Chamakh ndiye mchezaji anayetajwa sana na wadau wa soka na vyombo vya bahari nchini kuwa tishio katika kikosi cha Morocco kinachotarajiwa kumenyana na Taifa Stars mwishoni mwa wiki. Huyo ni papa katikati ya nyangumi.

Rekodi za wachezaji mbalimbali wa Morocco katika ngazi ya klabu na timu ya taifa zinaonyesha wachezaji wengine kama Mounir El Hamdaoui, Youssef El Arabi, Youssouf Hadji nao ni tishio.

El Hamdaoui anayeichezea klabu ya Ajax Amsterdam ya Uholanzi amekuwa na mafanikio katika klabu mbalimbali alizochezea kuanzia Excelsior, Tottenham Hotspur, Derby County, Willem II na AZ Alkamaar, kabla ya kujiunga na Ajax, Julai 2010.

Huyu ni mshambuliaji mahiri anayepaswa kuchungwa na mabeki wa Taifa Stars. Katika msimu wa 2008–09 El Hamdaoui alikuwa Mchezaji Bora wa Mwaka Uholanzi na alikuwa mfungaji bora wa ligi daraja la kwanza maarufu kama Eredivisie na aliiwezesha AZ kutwaa taji kwa mara ya pili.

Msimu wa 2007-08 alifunga mabao saba lakini 2008—09 alikwamisha wavuni mabao 16 na kuibuka mfungaji bora. Ajax ndiyo inaongoza ligi ikiwa na pointi 17 huku mshambuliaji huyo akiwa amepachika mabao sita katika mechi saba alizocheza.

El Hamdaoui ameichezea Morocco mechi tano na amefunga bao moja tangu alipoanza kuichezea mwaka jana. Lakini rekodi za mchezaji huyo aliyezaliwa mwaka 1984 kwa ngazi ya klabu inatoa ishara anapaswa kuchungwa.

Youssef El Arabi anaichezea klabu ya SM Caen ya Ufaransa inayoshika nafasi ya nane katika Ligi Daraja la Kwanza ya Ufaransa maarufu kama Ligue 1 baada ya kufikisha pointi 12 kutokana na michezo minane iliyocheza. Amechezea klabu mara 13 na amefunga mabao mawili.

Kocha mkuu wa muda wa Morocco, Dominic Cuperly amemrejesha kundini Adel Taarabt ili kuimarisha timu hiyo iliyolazimishwa suluhu na Jamhuri ya Afrika ya Kati mapema mwezi uliopita.

Taarabt alianza kung’ara miaka minne iliyopita na alipotia saini Tottenham Hotspur tarehe 2 Januari 2007 alisifiwa sana hata kutabiriwa angekuwa Zinedine Zidane mpya. Lakini nyota yake ilififia.

Hivi sasa anaichezea timu ya Queen’s Park Rangers, inayoongoza Ligi Daraja la Kwanza Uingereza. Ameichezea timu ya taifa mechi nane na amefunga mabao matatu.

Mchezaji mwingine aliyerejeshwa ni Houssine Kharja wa klabu ya Genoa ya Italia, ameichezea Morocco mechi 58 na kufunga mabao matano. Geneo iko nafasi ya 10 katika ligi ya Serie A.

Aidha, Ahmed Kantari ameitwa kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2005 kuimarisha beki na Youssef Kadiu Al Idrissi amerejeshwa tangu alipoichezea kwa mara ya mwisho mwaka 2004.

Vilevile Cuperly atamtegemea Youssouf Hadji, ambaye anaichezea As Nancy-Lorraine ya Ufaransa, inayoshika nafasi 18 katika msimamo wa timu 20. Youssouf ambaye ni mdogo wake Mustapha ameichezea timu ya taifa mara 51 na amefunga mabao 15.

Hata hivyo, Morocco itamtegemea zaidi Chamakh (26) ambaye ameichezea timu ya taifa mechi 53 amefunga mabao 14.

Chamakh alianza kupata umaarufu alipokuwa Bordeaux ya Ufaransa ambako uchezaji wake ulimkuna Arsene Wenger akamsajili kwa ajili ya Arsenal.

Hadi Jumapili iliyopita alikuwa amecheza mechi saba na amepiga mabao mawili yaliyochangia Arsenal kushika nafasi ya nne katika chati ya Ligi Kuu ya England ikiwa na pointi 11.

Mshambuliaji huyo, ambaye hakung’ara katika kikosi kilicholazimisha suluhu na Jamhuri ya Afrika Kati mapema mwezi uliopita ndiye nahodha wa Morocco.

Mabeki wa Taifa Stars, Nadri Haboub ‘Cannavaro’, Shadrack Nsajigwa, Aggrey Morris, Stephano Mwasika watapaswa kusoma mbinu za wachezaji hao wadhibiti mashambulizi yoyote
Japokuwa Morocco ina mafanikio ya kihistoria ya kutwaa Kombe la Mataifa ya Afrika na kufikia kucheza fainali za Kombe la Dunia, haijawa tishio tangu mwaka 2004 iliposhika nafasi ya pili katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika.

Mwaka 2006 na 2008 iliondolewa hatua ya makundi na mwaka 2010 haikufuzu kabisa. Timu hiyo inashuka taratibu na haina ubora ulioiwezesha kutwaa Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 1976.

Baada ya kupangwa Kundi D pamoja na Tanzania, Algeria na Jamhuri ya Afrika Kati, Morocco imejikuta ikikosa mteremko iliofikiria na sasa imeweka kambi yake Uholanzi kwa ajili ya mechi dhidi ya Stars iliyoko chini ya Jan Borge Poulsen.

Baada ya Taifa Stars kujijenga vizuri chini ya Mbrazil, Marcio Maximo, sasa ina uwezo wa kudhibiti timu ngumu kama Morocco na ilionyesha uwezo huo ilipolazimisha sare ya bao 1-1 na Algeria mjini Blida.

Matokeo ya hivi karibuni ya Stars yameimarisha ari ya Stars ambayo inawania kufuzu kwa mara ya pili kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2012.

0
No votes yet