Wakazi wa Mabwepande na ‘kilio cha samaki’


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 09 May 2012

Printer-friendly version
Gumzo la Wiki

BAADHI ya wakazi 600 waliohamishiwa kijiji cha Mabwepande baada ya kukumbwa na mafuriko Dar es Salaam, tarehe 21 na 22 Desemba 2011, wameilalamikia serikali kwa kuwatelekeza.

Wananchi wamesema hawana hospitali, soko wala maji ya uhakika. Mahema yao yameanza kuchanika na vyoo kujaa na kuhatarisha maisha yao.

Ukitazama eneo hilo kwa mbali kinachoonekana ni utitiri wa mahema mithiri ya yaliyokuwa makambi ya wakimbizi, huko Kigoma na Kagera, na majengo mawili ya kisasa; shule ya msingi ambayo bado inajengwa na kituo cha polisi.

Hayo yamebainika wakati wa ziara ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali, iliyofanyika 3 Mei 2012 –  Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari duniani – kwa lengo la kuibua sauti za wakazi hao.

Katika ziara hiyo iliyoandaliwa na Klabu ya Waandishi Mkoa wa Dar es Salaam (DCPC), ilibainika kuwa wakazi hao wanaendelea kuishi kwenye mahema miezi mitano baada ya kupata mafuriko.

Wakazi hao hawajui ni lini wataachana na makazi ya muda na kupata nyumba za kudumu; wala hawana taarifa kama wataruhusiwa kujenga nyumba wenyewe au watajengewa na serikali.

Msisa Mtimba (28), mwanaume mmoja wa wakazi hao, amesema kadri muda unavyokwenda, ndivyo maisha yao yanavyozidi kuwa magumu.

“Vyoo vimeanza kujaa na kutishia usalama wa afya zetu; na kwa mvua hizi kuna uwezekano mkubwa wa kupata magonjwa ya mlipuko.

Naye Saada Shaban amesema vyoo vya muda walivyochimba vimejaa hadi funza wanatambaa nje ya vyoo.

Amesema hawawezi kuchimba vyoo kila sehemu maana hata maeneo hawajagawiwa rasmi.

Amesema maisha ya Mabwepande ni magumu kwa kuwa serikali haijawagawia viwanja wala kuwaruhusu kujenga nyumba za kudumu. Mahema waliyojengewa, amesema yanashindwa kuhimili upepo na mvua zinazoendelea kunyesha.

“Tulipoletwa hapa tulifurahi sana. Tunaipongeza serikali kwa kutunusuru, maana huwezi kujua yangetupata masaibu gani; lakini hapa hali ni mbaya. Serikali haijatuletea huduma walizotuahidi,” amesema Saada.

Kwa upande wake, Magati Maulid, amesema mara tu baada ya kuhamishiwa Mabwepande, viongozi mbalimbali wa mkoa na kitaifa walikuwa wakiwatembelea kila mara, lakini sasa hawaendi tena.

“Hata misaada waliyokuwa wakituletea mara kwa mara sasa hivi imekoma, wametuacha kila mtu lwake,” amesema.

Kilio cha wananchi hao ni kama cha samaki, alichoimba Marehemu Dk. Remmy Ongara, kwamba hakina machozi au hakuna anayeona machozi yake.

Mwenyekiti wa eneo hilo, Khalid Msuya amesema malalamiko ya wananchi ni mengi, lakini nao wanatakiwa kujishughulisha, ili kujipatia kipato badala ya kutegemea tu serikali.

Akizungumzia hali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana, amekaririwa akisema mipango ya kuwasaidia wakazi hao iko “…kwenye mchakato na tunawaomba wananchi wavute subira.”

Miongoni mwa malalamiko ya wananchi hao ni huduma za umeme na maji. Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) na Mamlaka ya Majisafi na Majitaka wanaendelea kusambaza huduma hizo, lakini hazijawafikia walengwa.

Maulid amesema TANESCO imetumia nguvu na fedha nyingi kuweka nguzo za umeme na kufunga transfoma, lakini wananchi hawawezi kuvuta nishati hiyo kutokana na mahema wanayoishi kutoruhusiwa kisheria kuwekewa huduma hiyo na kipato chao duni.

Meneja uhusiano wa TANESCO, Badra Masoud amesema sheria inaruhusu umeme kuunganishwa tu kwenye nyumba za kudumu.

“Hawa wa Mabwepande wameandaliwa vibao maalum vya kuunganishia umeme (Ready board) ambavyo vinauzwa Sh 47,000. Kama hawajaenda kuvinunua hilo si tatizo letu. Sisi tumeshafikisha umeme kwenye eneo, basi,” amesema Masoud.

Kutokana na hali hiyo, wananchi wanafaidi umeme huo kutoka katika taa zilizofungwa kwenye nguzo za umeme, lakini kwenye mahema yao ni giza. Salum Omari, amesema akitaka kuchaji simu yake hulipia Sh 300 kwa mkazi mwenzao aliyefunga umeme wa jua.

Hawa Ayubu (19) amesema hata taa ndogo za kutumia mionzi ya jua walizopewa kama msaada, nyingi zimeharibika, hivyo “usiku unapoingia ni giza mtindo mmoja.”

Mbali na malalamiko hayo, wakazi hao wameishukuru serikali kwa kuwahamishia  Mabwepande.  Lakini mpango huo umeacha kilio upande wa pili; wenzao wameondolewa kwenye maeneo hayo bila kulipwa fidia.

Kilio hicho kilianza mapema Januari walipohamishwa, lakini hadi leo, wamesema tatizo hilo halijatatuliwa. Wanasema hiyo ni dhuluma na uonevu.

Alipotembelea eneo hilo 13 Januari 2010, Rais Jakaya Kikwete alipokewa kwa mabango na vilio kutoka kwa wenyeji hao. Mabango yalibeba ujumbe wa kudai fidia au kubaki kwenye mashamba yao.

“Tumekuwa wakimbizi, tumekuwa waathirika wapya wa maafa badala ya kuwakaribisha wageni wetu (waathirika wa mafuriko),” mmoja wa wenyeji hao alikaririwa akisema.

Wananchi hao wamesema walifikia hatua ya kuonyesha mabango baada ya kukwama kusikilizwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Dar es Salaam. Hatimaye waliona tingatinga likiingia kwenye mashamba yao kutengeneza barabara.

“Mheshimiwa Rais sisi tupo hapa kwa miaka mingi. Tunashangaa serikali kuja na kuanza kuvunja nyumba zetu bila hata kutulipa fidia,” alisema mmoja wa wakazi hao.

Rais Kikwete aliwataka wapeleke vielelezo vya viwanja vyao kwa Mkuu wa Wilaya au Mkoa ili kutatua tatizo hilo.

Lakini serikali kupitia wizara ya ardhi inasema  ilikuwa imeshatoa fidia kwa wenyeji ili kubadili matumizi ya eneo na kujenga nyumba za bei nafuu.

Mmoja wa wananchi waliohamishwa maeneo hayo, Lucas Japhet (56) amepinga maelezo hayo, akisema yeye amekuwapo pale muda mrefu na hakulipwa fidia yoyote.

Japhet amesema hata maagizo ya Rais Kikwete aliyotoa Januari 2012 hayajatekelezwa hadi sasa.

Mbali na hilo, Rais Kikwete aliagiza Kamati ya Maafa ya Mkoa wa Dar es Salaam, iliyoongozwa na Mkuu wa Mkoa, Said Meck Sadiki kuwapa viwanja pia waliokuwa wapangaji katika maeneo ya mafuriko.

“Ili kuondokana na usumbufu na wapangaji, Mkuu wa Mkoa nakuagiza kutengua maamuzi yenu hasa ya kutowapa viwanja wapangaji, maana hawa wote ni Watanzania wenzetu ambao hawakutamani kuishi hivyo,” alisema Rais Kikwete.

Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, alipoulizwa kuhusu kinachoendelea katika eneo hilo, alisema kupitia barua pepe kuwa suala la maafa lipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alipoulizwa alisema, “Kuhusu Mabwepande hilo silijui, muulize Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Kaimu Mkuu wa Mkoa, Mwantumu Mahiza alipoulizwa Jumamosi, alisema amesikia malalamiko ya wakazi hao, lakini hana majibu yao.

“Mimi udeiwaka wangu nimemaliza leo. Mwenyewe Said Meck Sadik ataingia kesho na bila shaka Jumatatu atakuwa ofisini; mtafute yeye na bila shaka  atakuwa na majibu kwa maswali yako. Mimi siwezi kumjibia,” alisema Mahiza.

Lakini RC Sadik alipoulizwa juzi Jumatatu, amesema bado hajaingia ofisini na angeweza kujibu maswali ya MwanaHALISI kesho Alhamisi.

“Hapa ninapozungumza na wewe niko Mwanza. Bado sijaingia ofisini, maana kuzungumza kabla hujaingia ofisini nalo ni tatizo,” aamesema Sadik.

Mbali na makazi duni, kilio kingine cha wakazi hao ni njaa na malalamiko ya upendeleo katika ugawaji chakula cha msaada.

Boniphace Katimba amewatuhumu viongozi wa eneo kuwa wanafanya udanganyifu katika ugawaji misaada inayopatikana.

“Ni udanganyifu tu. Unga wameiba na mimi sijapata chakula. Wanasema mimi ndio najitokeza kueleza matatizo ya hapa na udanganyifu wao pindi wanapokuja waandishi wa habari…sijapewa chakula hata kidogo,” amelalamika mzee huyo ambaye ni daktari msaafu, aliyehamishwa kutoka eneo la Jwangwani.

Lakini Mwenyekiti wa eneo Msuya amesema hakuna upendeleo wowote unaofanyika, bali msaada wanaoletewa hivi sasa ni mdogo ikilinganishwa na hali ilivyokuwa hapo awali.

Mohamed Abubakar, amesema mwanzoni walikuwa wanapewa chakula mara kwa mara, lakini hivi sasa kinachelewa hadi wiki tatu, mara nyingine hata mwezi unapita.

Tofauti na wenzake, Abubakar anajiingizia kipato kwa kibarua cha kuchimba mitaro ya mabomba ya maji. Analipwa Sh 7,000 kwa siku, ingawa bado anadai kiwango hicho ni kidogo ukilinganisha na stahili yake ya Sh 15,000.

Wakazi wenzake, hasa wasiokuwa na nguvu za kuchimba mitaro wanazidi kulia njaa. Hata wale ambao kabla ya mafuriko walikuwa wanafanya biashara ndogo sasa zimekwama.

Wachuuzi hao wamesema gharama za biashara hizo ni kubwa hasa nauli, kutoka katika eneo hilo kwenda jijini Dar es Salaam na kurudi, hivyo hawawezi kupata faida.

Wamesema bidhaa ndogo zikiletwa katika eneo hilo, hata kama zinahitajika, nyingi zinadoda na kuharibika kutokana na kukosa wanunuzi. Hii ni kwa kuwa hakuna wengi wenye kipato.

Mtimba ambaye alihama kutoka eneo la Magomeni Sunna, amesema anashindwa kufanya biashara kutokana na ukubwa wa nauli ambayo ni zaidi ya Sh 2,600 kila siku.

“Hebu fikiria kutoka Mabwepande hadi Kariakoo; nalazimika kuunganisha magari matatu. Napandia hapa (Mabwepande). Nakwenda hadi Bunju; Bunju-Mwenge; na Mwenge-Kariakoo. Hapo natumia zaidi ya Sh 2,600,” anasimulia.

Amesema hata mabasi maarufu kwa jina la daladala yanakwepa kwenda Mabwepande kutokana na kukosa uhakika wa abiria.

Mamlaka ya Usafirishaji Nchi Kavu na Majini (Sumatra), 3 Mei 2012 ilitangaza kuyafutia leseni mabasi 17 ya abiria kwa kushindwa kutoa huduma katika eneo la Mabwepande.

Hawa Ayubu amesema katika eneo hilo hakuna hospitali baada ya hospitali ya muda iliyoanzishwa mara tu baada ya mafuriko kufungwa, na wakazi wanapata shida kutafuta huduma za afya.

Amesema hawajatengewa maeneo ya ibada wala makaburi; hivyo wanalazimika kufuata huduma hizo mbali na eneo lao.

Abubakar anasema, “…hata lile gari la wagonjwa unaloona pale (la jeshi) halifanyi kazi. Watu wakiugua hapa kuna mwenzetu mmoja ana pikipiki ndiye anajitolea kusaidia kuwapeleka wagonjwa hadi Bunju.”

Katika eneo hilo kila mtu ana kilio chake. Mohamed Nassib (27) analia kwa upweke.

Akiwa amekaa kwenye jiwe chini ya mti huku akisoma kipande cha gazeti, Nassib alisema pamoja na mateso anayopata huko Mabwepande, anamkumbuka mkewe na mwanawe aliotengana nao baada ya mafuriko.

“Nina mke na mtoto wa miaka minne (majina tunayahifadhi). Lakini hapa mimi nakaa peke yangu. Ndugu wa mke wangu walimchukua tulipopata matatizo. Mimi nilikuja hapa peke yangu,” ameeleza.

Amesema ndugu wa mkewe walisema “mtoto wao hawezi kuishi katika shida hizi.”

Alipoulizwa kama amemfuatilia na kuzungumza naye, Nassib alisema, “Tunawasiliana na juzi alinipigia simu, akanipa masharti kwamba nimtafutie kwanza binti wa kazi ili amsaidie kushika mtoto kwa sababu yeye ana shughuli zake.

“Mimi nimeshindwa. Katika hali hii hizo pesa nitazipata wapi?” alihoji Nassib.

Amesema, hata hizo shughuli za ujenzi anazotegemea kujiingizia kipato hazipo katika eneo hilo. Huzifuata maeneo mengine ya jiji la Dar es Salaa na kwamba nauli ni kubwa.

“Fikiria kutoka hapa Mabwepande hadi Bunju ni Sh. 500. Kutoka hapo hadi Mwenge ni Sh. 500 pia. Hadi kurudi unatumia Sh 2,000. Na mara nyingi hapa daladala hakuna, ukichukua bodaboda (pikipiki) kutoka Bunju hadi hapa ni Sh. 2,000,” amelalamika Nassib.

Pamoja na ukimya wa serikali, wakazi wa Mabwepande hawakujengwa kisaikolojia wala kuelezwa jinsi ya kujikwamua kutoka katika hali hiyo. Badala yake wanaendelea kuisubiri serikali kuwajengea makazi ya kudumu.

0
No votes yet