Wakiwalipa Dowans, tuwalipishe


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 25 January 2011

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala

NINAZO habari mbili; moja mbaya nyingine nzuri. Kwanza, ni mkataba ambao Shirika la Umeme la Taifa (TANESCO) ilifunga na kampuni ya Richmond na kujiweka chini ya usuluhishi wa Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi (ICC) bila ya kuwa na nafasi ya kukataa rufaa.

Kutokana na hali hiyo, ni wazi kuwa kampuni ya Dowans S.A iliyorithi mkataba huo, italipwa karibu Sh. 100 bilioni ikiwa ni tuzo kufuatia ushindi wake kwenye ICC.

Kiasi hicho kitakuwa ni nyongeza ya zaidi ya Sh. 100 bilioni ambayo kampuni hiyo imekwishalipwa hadi sasa, tangu sakata la Richmond/Dowans kuibuka.

Hadi Juni 2007 tayari Dowans ilikwishalipwa na serikali zaidi ya Sh. 44 bilioni na hadi mkataba unavunjwa mwaka 2008, kampuni hiyo ilikuwa imejipongeza kwa mabilioni ya fedha za Watanzania.

Hii yote ilitokana na uongozi wetu kushindwa kununua majenereta yale yale kutoka kwa watengenezaji ambayo jumla ya gharama yake – mauzo na usafirishaji –  ingekuwa chini ya Sh. 60 bilioni!

Kama ilivyokuwa kwenye ununuzi wa rada ambapo tulilipia zaidi ya Sh. 21 bilioni (karibu Sh. 40 bilioni) na kwenye ndege ya rais tulikolipa zaidi ya Sh. 20 bilioni, serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imeendelea kuonesha kuwa “fedha zipo” na hakuna tatizo kuzigawa kwa mafisadi kila wanapozihitaji. 

Ikiwa Dowans watalipwa kiasi hiki cha fedha, mkataba wa Richmond utakuwa ni miongoni mwa mikataba iliyoligharimu taifa fedha nyingi kuliko wakati mwingine wowote.

Kimsingi tutakuwa tumelipia majenereta ya Sh. 60 bilioni zaidi ya Sh. 150 bilioni na kisha wenye majeneta hayo watang’oa majeneta yao na kuondoka.

Uwezekano pia (naendelea bado na habari mbaya) uko kwamba baada ya kuwalipa kiasi hicho cha tuzo, serikali itaingia mkataba mwingine (kupitia Tanesco) na kampuni nyingine iliyonunua majenereta hayo toka Dowans ili tuweze kuyakodisha sasa “upya” kutoka kampuni hiyo au “kuyanunua” kabisa.

Sakata la Dowans limegeuzwa kuwa ni jogoo la taifa ambalo tutazungushiwa nalo hadi tutakapopata ujasiri wa kusema hapana; uongozi wa juu wa CCM hauoni tatizo lolote la malipo hayo kufanyika.

Habari mbaya ni kuwa tunaelekea kuwalipa Dowans kama ambavyo chama tawala kilichopigia wananchi magoti miezi michache tu iliyopita kuomba kuongoza imekubali “kosa” na kuwaachia “Watanzania wengine kupinga hukumu” hii.

CCM hakina mpango, nia, wala sababu ya kuonesha kuwa malipo haya ni kufuru kwa taifa.

Habari nzuri ni kuwa tunajua tumeingizwa mjini na watawala wetu na kwamba malipo ya Dowans yangeweza kuzuilika mapema endapo watendaji wetu, na viongozi wengine wa kisiasa wangekuwa makini.

Madai haya ya Dowans hayakushushwa na shetani na hayawezi kuondolewa kwa kupiga magoti kama aina ile ya “mapepo.” Kuingia kwa Dowans nchini na hatimaye kufanikiwa kuingizwa kwenye mkataba wa kifisadi hakukuletwa kwa bahati mbaya. Kuna watu walihusika na watu hao wapo na wanajulikana.

Hivyo, basi ni wajibu wa wananchi kuwawajibisha wale wote waliohusika na mkataba huu. Wakwanza kuwajibishwa, ni mbunge wa Igunga, Rostam Aziz.

Huyu tayari amekiri kuwa alishawishi Dowans kuja nchini, huku akijua kuwa ni kampuni iliyoandikishwa kwa kutumia ulaghai wenye lengo la kulinda wamiliki wake halisi na kumpachika Bernal Zamora Arce kama rais wake huko Costa Rica.

Jambo hili ni muhimu kwa kuwa wakati Tanesco wanaingia mkataba kutoka Richmond kwenda Dowans 23 Desemba 2006, tayari Dowans S.A ambayo Rostam amepewa nguvu za kisheria, ilikuwa tayari imechukua mkataba huo toka Richmond 14 Oktoba 2006 kinyume cha utaratibu.

Rostams akiwa ni raia wa Tanzania na mbunge alitakiwa wa kwanza kuweka maslahi ya taifa.

Mwingine anayepaswa kuwajibishwa ni Nazir Karamagi aliyekuwa waziri wa nishati na madini ambaye aliicha Tanesco taarifa sahihi juu ya ukweli kwamba mkataba wa Richmond/Tanesco ulikuwa umeshahamishiwa Dowans S.A.

Naye kama Rostam alikaa kimya na kuiacha Tanesco wakisaini “mkataba hewa” 23Desemba 2006.

Mwingine ni wamiliki wa Dowans S.A na Dowans Tanzania Limited ambao walificha ukweli kuwa tayari walikuwa wamekwishachukua mkataba wa Richmond/Dowans kinyume cha sheria.

Mkataba ulitaka Tanesco wakati wa kuhamisha mkataba na wasaini kwa maandishi. Hivyo kwa kitendo chao kuiacha Tanesco kusaini mkataba hewa, raia wote wa Dowans S.A serikali inatakiwa kuwaondoa nchini mara moja.

Endapo Dowans S.A italipwa na ikajulikana wamelipwa (kwani fedha zilikwisha tengwa) basi Dk. Harrison Mwakyemba na Samwel Sitta hawapaswi kuendelea kuwapo katika serikali iliyoidhinisha malipo hayo.

Katika ripoti yake kwa Bunge Dk. Mwakyembe aliishangaa bodi ya wakurugenzi ya Tanesco kukubali kuburuzwa na wizara na kusema, “…inashangaza kuwa baada ya kudhalilishwa na wizara kwa kiwango hicho, chombo kikuu cha maamuzi cha Tanesco, yaani Bodi ya wsakurugenzi, haikuchukua hatua ya heshima ya kujiuzulu.”

Ninaamini kabisa kuwa malipo ya Dowans yatamdhalilisha Sitta na Mwakyembe; hivyo machoni mwa wengi wataweza kuonekana kuwa wasaliti.

Uamuzi pekee wa “heshima” itakuwa ni kwa wao kutangaza kujiuzulu kama namna ya kupinga malipo hayo.

Naye Rais Jakaya Kikwete kama kiongozi mkuu wa serikali hiyo ni lazima aje na kuomba radhi taifa kwa kushindwa kuweka maslahi ya taifa mbele kuanzia mwanzo wa sakata hili hadi mwisho. Aeleze sababu za kushindwa kuonesha uongozi unaostahili.

Rais hawezi kutafuta kisingizio; tunalo zigo la Dowans kwa sababu ya uongozi wake.

Ni lazima wananchi wanapoanza mwaka huu mpya watambue kuwa tunaishi na matokeo ya uchaguzi ambao tumeufanya.

Ni kweli uchaguzi umekwisha, lakini muda wa uamuzi haujapita na wala haujaisha. Tunaitwa na historia, na dhamira zetu kufanya uamuzi kila siku. Tayari wengine wanajutia uamuzi walioufanya 31Oktoba 2006 na wanatamani wangekuwa sehemu ya mabadiliko.

Kwa vile hakuna anayeweza kubadili historia, ni wazi kuwa uamuzi mpya unahitajika kufanyika. Ninaamini tayari tunajua uamuzi huo upendelee chama gani na viongozi gani.

Ninatoa mwaliko kwa wale ambao bado hawajakata shauri la kuachana na utawala ulioishiwa maono kuamua kuunga mkono mabadiliko ya kweli. Wasisubiri hadi 2015 kufanya uamuzi huo. Wakati ni sasa kwani wakishalipa, na sisi tuwalipishe.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: