Wako wapi wezi wengine wa EPA?


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 06 June 2012

Printer-friendly version

MASWALI haya ni kwa Watanzania wote lakini zaidi kwa waandishi wa habari, wanasheria na wengine wote wanaojua zilikofikia kesi za wizi wa fedha katika akaunti ya madeni ya nje (EPA) katika Benki Kuu (BoT).

Je, kulikuwa na washtakiwa wangapi? Mpaka sasa kesi ngapi zimekwisha na matokeo yake? Na je, bado kuna kesi kortini?

Zilipofunguliwa kesi za watuhumiwa wa wizi wa zaidi ya Sh. 133 bilioni za EPA ilionekana kama faraja kwa Watanzania kwamba serikali yao iliamua kuchukua hatua dhidi ya wahalifu hao.

Lakini kilichowashangaza ni mazingira yanayoonekana wazi yalilenga kulainisha kesi zenyewe na hatimaye kuwaokoa baadhi ya wezi hao.

Kwanza, kuonyesha kwamba katika suala hilo kulikuwa na ‘namna,’ ni jinsi kiongozi wa nchi Rais Jakaya Kikwete alivyoshughulikia kwa kuwapa wezi muda wa kurejesha fedha hizo na kwamba ambao wangeshindwa kurejesha wangepelekwa mahakamani. Huu ulikuwa udhaifu mkubwa kiutendaji na ulilalamikiwa na wengi wakiwemo wabunge.

Pili, baadhi ya wahusika wakuu hawakushtakiwa hadi leo kwa kile  Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na  Rushwa (TAKUKURU) Dk. Edward Hosea anataka Watanzania waamini kuwa ni kutokana na kukosekana kwa ushahidi.

Lakini kama ushahidi haukuwepo, wezi waliwekwaje kwenye orodha baada uchunguzi?  Jambo la ajabu, ni kwamba Hosea na wenzake Mwanasheria Mkuu wa zamani, Johnson Mwanyika na Said Mwema (Inspekta Jenerali wa Polisi) ndio walitangaza majina ya wezi hao. Kumbe hawakuwa na ushahidi?

Kichekesho ni pale mmoja wa watuhumiwa wa wizi huo afisa usalama mstaafu ambaye kampuni zake mbili zilihusishwa na wizi huo. Huyo ndiye alikuwa kwenye Kamati Maalum ya kuchunguza wizi ikidaiwa eti ofisa huyo alipenyezwa ili awanase wezi.

Hivi wizi wa EPA uligunduliwa na Usalama wa Taifa? Kama uligunduliwa na Usalama wa Taifa, mbona serikali ilikataa kuwa hapakuwa na wizi wowote BoT? Mbona hata aliyekuwa Waziri wa Fedha, Zakhia Meghji alitapatapa mara ‘tunachunguza’, mara hakuna wizi na hatimaye akadai fedha hizo zilitumika katika masuala ya Usalama wa Taifa?

Hivi kweli hakuna anayejua aliyekuwa akichukua fedha kwa niaba ya kampuni kama Kagoda Agriculture Ltd ambayo ilikwapua zaidi ya Sh 40 bilioni? Nakala za hundi na saini za wapokeaji wa fedha hizo, yakiwemo mabenki husika yanajulikana, mbona hatuwaoni wezi hao mahakamani?

Pia kuna hundi ambazo zinawahusisha na wizi huo baadhi ya viongozi wa CCM. Nani alikuwa akipokea pesa kwa niaba ya CCM?

Mbona hawa hatuwaoni mahakamani, na kama ilivyo kawaida ya Watanzania tunataka kusahau kashfa hii! Mbona katika moja ya kesi hizo wezi wawili kukopeshana Sh. 500 milioni kwa dhamana ya nyumba kumechukuliwa kama ushahidi wa wizi wa EPA?

Kati ya kampuni 22 zilizotumika kuiba fedha hizo, baadhi zilikuwa za maafisa Usalama wa Taifa na zile zilizoanzishwa kwa makusudi ya wizi huo tu .

Wahusika wengine inadaiwa Dk. Hosea aliwagwaya kwa kuwa walikuwa waratibu wakuu wa wizi huo ambao lengo lake kuu lilikuwa kutafuta fedha kwa ajili ya kampeni za mgombea wa Urais mwaka 2005. Baadhi ya wezi hao ndio walijua mgawo huo ambao ulikuwa asilimia 40 kwa kila pesa aliyolipwa mwizi na BoT.

Kilichomshangaza Rais Kikwete ni wajanja kukwapua mabilioni kwa kutumia mgongo wake na kampeni za CCM huku wakiwemo marafiki zake! Lakini tunaambiwa kilichomuuma zaidi ni kushindwa kwa wezi hao kuonyesha hata hizo pesa zilizopelekwa CCM zilitumikaje! Je, hizo kampuni 22 zilijuaje kwamba kuna pesa huko BoT na ziliteuliwaje?

Katika maelezo ya awali ya wezi hao, tunaambiwa ile kamati aliyounda Rais Kikwete iliwakataza wezi hao kuitaja CCM katika maelezo yao na wengine walilazimika kuandika maelezo mara mbili au tatu lengo likiwa kuhakikisha CCM haionekani.

Kwa mfano, hivi ni siri tena kwamba magari ya aina ya Mahindra zaidi ya 100 kutoka India yalinunuliwa na mmoja wa wezi wa fedha za EPA na ndizo zilizotumika? Magari hayo yaligawiwa kwa makatibu wilaya wa CCM katika wilaya zote za Tanzania kwa ajili ya kampeni 2005.

Lakini jambo linalosikitisha zaidi ni haya mazingira ya sasa ambayo yanaonesha wazi huenda katika wale waliofikishwa mahakamani ni Rajabu Maranda na mpwae Farijala Hussein pekee ndio watasota jela maana hatuoni dalili zozote za kesi za wengine kuendelea mahakamani au wezi wengine kufikishwa mahakamani.

Kila kukicha, kesi pekee tunazosikia ni zile za Maranda na Farijala lakini nyingine chache ambazo zinahusu Wahindi hazisikiki tena.

Watu wanajiuliza, kesi hizo zimekwisha au ni njama za ucheleweshaji ili baadaye zifutwe? Maranda ana karibu kesi nne za EPA, na katika kesi hizo zote mshirika wake mkuu ni Mhindi mmoja na mdogo wake ambao wanadunda mitaani na kuendesha biashara zao za mafuta nchini, biashara na kiwanda cha sukari nchini Uganda na hata biashara na taasisi moja nyeti ya ulinzi nchini.

Tulio mbumbumbu wa sheria tutajiuliza, iweje Maranda afungwe lakini mwenzie ambaye walisafiri naye hadi Ulaya na kufanya kila kitu naye awe huru mitaani? Hizi si lawama kwa mahakama, bali ulivyo uendeshaji wa kesi, maana mahakama inapokea mashtaka iliyopelekewa na kuendelea nayo kama yalivyo.

Hivi mbali ya Maranda na Farijala ni mwizi gani mwingine ambaye ameshahukumiwa katika kesi hizi? Ina maana Maranda peke yake ndiye alikuwa “mjinga” akashindwa kuficha ushahidi?

Tulitajiwa kampuni 22 zilizoiba, mbona zilizofunguliwa hazifiki hata 10?

Je, leo Dk Hosea anaweza kutuambia, ni kampuni na watuhumiwa wangapi wamefikishwa mahakamani? Je, uchunguzi wa wizi huo wa EPA umekwisha au bado unaendelea kama alivyoahidi miaka kadha iliyopita? Hili ni changa la macho, na  tusipoangalia, ni Maranda pekee, ndiye atatolewa kafara wa EPA.

Inafahamika kwamba kazi ya Maranda ambaye alikuwa kiongozi wa CCM mkoa wa Kigoma ilikuwa kuhakikisha jimbo la Kigoma Mjini linarejeshwa CCM kazi ambayo aliifanya kwa “umakini mkubwa” na kufanikiwa kulirejesha jimbo hilo.

Kwa mazingira yaliyopo inaonyesha bila shaka kuna udhaifu wa makusudi kwa upande wa waendesha mashtaka. Mwanya huu ndio umewafanya baadhi ya watuhumiwa ambao walipaswa kuwa mahabusu tunawaona wakitamba mitaani huku wakiendesha biashara zao (tena kwa hela hizo hizo za EPA) bila wasiwasi wowote.

Uendeshaji wa kesi za EPA unatukumbusha kauli ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye alikiri kuwa wezi hao wana pesa nyingi na wangeweza kuyumbisha uendeshaji wa kesi zao. Kama Waziri Mkuu aliwagwaya hao wezi, ina maana serikali imefyata mkia.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: